USHAURI WA DAKTARI: Msongo wa mawazo unavyoibua maradhi

Msongo wa mawazo au kwa Kiingereza stress, ni hali ya mwili kujihami kwa kujibu mapigo baada ya kupata tishio fulani.

Shinikizo la akili lisipodhibitiwa linaweza kusababisha kujitokeza kwa magonjwa kadhaa ya mwili kama ya moyo, hasa shinikizo la damu.

Msongo wa mawazo unakuweka katika hatari pia ya kupata magonjwa ya akili, ukosefu wa hamu ya tendo la ndoa, ugumba, kupata kichaa asilia, kujiua, kujikataa na kufanya mambo yasiyotarajiwa na kupata makunyanzi ya ngozi.

Miaka ya nyuma shinikizo la damu lilikuwa likionekana zaidi kwa watu wenye unene uliokithiri au wenye wadhifa na uwezo wa kifedha.

Lakini miaka ya sasa hali imekuwa ni tofauti kidogo, kwa kuwa hata wenye uwezo mdogo na kutokuwa na wadhifa wamejikuta na maradhi ya shinikizo la damu yaani high blood pressure.

Shinikizo la damu maana yake ni kuwa na msukumo ambao unazidi kile kiwango cha kawaida ambacho ni 120-140/70-95 na huweza kuwa la kawaida, la kati, kali na kali iliyokithiri.

Ukiacha chumvi, uwepo wa mafuta mengi, uharibifu wa mishipa ya figo kulikotokana na kisukari kama chanzo cha shinikizo la damu, lakini karibuni msongo wa mawazo umekuwa ukichangia pia uwepo wa shinikizo kubwa la damu na magonjwa mengine kama kiharusi, kusahau (alzheimers disease) na shambulizi la moyo.

Uwepo wa shinikizo la kiakili na msongo wa mawazo mwilini, husababisha mwili kutiririsha kemikali ambazo husababisha kuuongezea mapigo ya moyo kudunda kwa nguvu.

Mifarakano, ugumu wa maisha, kuchanganyikiwa, kufiwa, kutokuwa na ajira, kuumwa maradhi sugu, kukosa mwelekeo kimaisha na kukata tamaa ni moja ya mambo yanayochangia kuwepo kwa msongo wa mawazo.

Moja ya mambo ya msingi kwa mtu mwenye msongo wa mawazo uliopitiliza ni kuwaona wataalam wa afya ya akili au wanasaikolojia ili kumpatia tiba ya kurekebisha hali hiyo.

Kujihusisha na shughuli za kila siku, kufanya mazoezi, kujiweka mbali na jambo linalokuletea msongo wa mawazo ni moja ya njia za kuepusha tatizo hilo.

Ni vema kuepuka mifarakano ya kijamii na kifamilia ili kuepusha misongo ya mawazo.