USHAURI WA DAKTARI: Uhai wa mimba unaanzia wapi?

Ni kawaida kukutana na swali la kichwa cha habari hapo juu kwa wanaharakati wasiokubaliana na baadhi ya njia za uzazi wa mpango na kwa baadhi ya wenye imani za kidini.

Wapo wanaodhani uhai huaanza baada ya mtoto kuzaliwa na kulia lakini ukweli wa kisayansi, uhai wa mimba ni mara tu mbegu ya kiume iliyokomaa inapounganika na kijiyai cha kike (ovum). Kwa mwanamke yeyote ambaye tayari ameshavunja ungo ni kiashiria kuwa anaweza kubeba ujauzito, hata anayevunja ungo na miaka tisa anaweza kupata ujauzito.

Kwa wastani mwanamke aliye katika umri wa kushika mimba huweza kutengeneza kijiyai kilichopevuka kila mwezi na kikikutana na mbegu ya kiume iliyokomaa mimba inaweza kutungwa.

Zipo njia mbalimbali zinazoweza kumfanya mwanamke kupata ujauzito, lakini wanawake walio wengi hupata mimba kwa njia za asili.

Mwanamke anapokutana kimwili na mwanaume hitimisho lake huwa ni kwa mwenza huyo kufika kileleni kutoa maji maji (manii) yaliyobeba mamilioni ya mbegu za kiume (sperms).

Inakadiriwa kwa mwanaume mwenye afya hutoa kati ya mbegu milioni 15-20 kwa mshindo mmoja. Ingawa ni mbegu moja tu inayohitajika kupandikiza kijiyai cha kike kilichopevuka.

Wakati wakikutana kimwili wenza wawili, mwanaume hufika kileleni na kumwaga maji maji yaliyobeba mbegu za kiume ndani ukeni. Mbegu hizo huwa na kama mkia unaowezesha kusafiri kwa kasi ndani ya uke kupitia mlango wa nyumba ya uzazi hadi kufika ndani katika nyumba ya uzazi.

Kwa kukadiria mshindo mmoja huwa ni ujazo wa mililita 3.7 au sawa na kijiko cha chai kisichojaa.

Mwanamke huwa na mirija inayosafirishia kijiyai kilichokomaa hadi katika eneo maalum katika mirija hiyo. Mbegu za kiume huweza kutembea mpaka kufika katika mirija katika eneo maalum la upandikizaji.

Mbegu bora iliyo na kasi na nguvu ndiyo huwa na uwezo wa kupandikiza kijiyai cha kike ili kutungisha mimba. Inapotokea mbegu zaidi ya mbili kupandikiza kijiyai au vijiyai ndiyo aina mojawapo ya mapacha hutokea.

Baada ya mbegu ya kiume kufanikiwa kupenya katika kijiyai cha kike na kulirutubisha hapo baadaye muunganiko huo hutoka katika mrija na kubingirika kwenda kujihifadhi eneo maalum katika nyumba ya uzazi.

Katika hatua hii ndiyo tunasema mimba imetungwa na ndipo uhai wa mimba unapoanza, muunganiko huo wa mbegu ya kiume na kijiyai cha kike (mimba) hujipachika katika eneo maalum katika mji wa mimba na kuanza kupiga hatua mbalimbali za ukuaji.

Kwa kawaida mbegu ya kiume huweza kuishi kwa siku mbili ndani nyumba ya uzazi mazingira yakiwa rafiki. Tafiti za kitabibu za karibuni zinaonyesha pia mbegu hizo zinaweza kuwa hai kwa siku tatu hadi tano.

Hivyo hata kama kijiyai cha kike kitapevuka na kuchoropoka baada ya saa 24 uwezekano wa kukutana na mbegu ya kiume iliyoingia saa 48 yaliyopita na mimba ikatungwa.

Mwanamke anayeweza kushika mimba ni yule ambaye hatumii njia zozote za uzazi wa mpango ikiwamo kuzuia mbegu za kiume kuingia (matumizi ya kondomu), vidonge, sindano na vitanzi.

Kama hakuna sababu yoyote ya kiafya itakayoharibu uhai wa mimba basi muunganiko huo utaendelea na kupiga hatua mbalimbali za ukuaji kwa kipindi cha miezi tisa mpaka kufika kuzaliwa kwa mtoto.