USHAURI WA DAKTARI: Vichochezi na dalili za kawaida za kupata hedhi

Leo nitawapa ufahamu juu ya kazi zinazofanywa na homoni za kike na dalili zinazojitokeza kabla na wakati wa hedhi.

Kichochezi cha Estrogen ni muhimu kwa afya ya uzazi wa mwanamke ambacho hufanya kazi ya kuchochea ujenzi wa tando laini za mji wa mimba.

Kwa kawaida kiwango cha kichochezi kingine kijulikanacho kama Progestrone huwa juu baada ya yai lililopevuka kuchoropoka katikati mwa mzunguko (siku ya 14) kwa wanawake walio wengi wenye mzunguko wa siku 28 hadi 30.

Hali hiyo ndiyo inaisaidia kichocheo cha Estrogen kuendelea kuufanya utando laini wa kuta za mji wa mimba kuwa pana tayari kupokea kiyai kilichotungishwa.

Kushuka kwa kiwango cha Progestrone sambamba na Estrogen husababisha tando hiyo kuvunjika vunjika na ndipo hedhi huanza kutiririka na kutoka.

Mabadiliko ya kiwango cha homoni mwilini yanaweza kuathiri mzunguko ama uwezo wa kubeba mimba.

Mfano ni wasichana wenye umri mdogo huwa wana kawaida ya kuwa na kiwango kidogo au mabadiliko ya kiwango cha homoni ya progestrone katika miili yao.

Vivyo hivyo kwa wanawake ambao wako karibu kufikia ukomo wa mzunguko wa hedhi hupata mabadiliko ya kichochezi hiki.

Hii ndiyo sababu ya wasichana na wanawake walio katika umri wa miaka 40 kuwa na hedhi nyingi ya ghafla na kubadilika urefu wa mzunguko wa hedhi au kuwa na mzunguko unaoyumba.

Vilevile yapo mambo mengine yanayoweza kusababisha mzunguko wa hedhi kubadilika ambayo ni utumiaji wa vidonge vya uzazi wa mpango, mwili mwembamba sana, kupoteza uzito sana, kuwa na uzito uliopitiliza.

Msongo wa mawazo na kufanya kazi ngumu au mazoezi magumu pia huchangia mabadiliko hayo.

Ingawa kwa kawaida uwepo wa mimba ndio chanzo cha kukosekana kwa hedhi na ndiyo maana mzunguko usipotokea hatua ya awali ni kuchunguza kama kuna ujauzito.

Kwa upande wa dalili za kupata hedhi si wanawake wote wanaozipata na wengine huzipata kabla na wakati wa kuingia katika hedhi.

Wiki moja kabla ya hedhi kutua wanawake wengi hupata dalili kabla ya kuanza kutoka.

Dalili hizo ni pamoja na kupata hasira, hofu, woga, kukosa furaha, kujihisi mvivu au mzito kuhisi tumbo kujaa, matiti kuuma na kujaa, uwepo wa chunusi kadhaa maeneo ya usoni na mgongoni.

Vilevile ukosefu wa nguvu za mwili, siku moja au mbili kabla unaweza kuhisi maumivu chini ya tumbo, mgongoni, kiunoni, miguuni, kuumwa kichwa, kukosa utulivu, kuhisi kuwa mzito au uchovu.

Inakadiriwa asilimia 85 ya wanawake wanapata dalili hizi, huku asilimia mbili hadi 10 hupata dalili kali kuliko kawaida.

Mara nyingi maumivu haya hupungua au kuisha baada ya siku ya kwanza ya hedhi kupita.

Unaweza pia kupata maumivu chini ya tumbo pale kijiyai cha kike kinapokuwa tayari kurutubishwa.

Katika kipindi hiki ni kawaida kuona vitone vya damu hali hii haizidi siku moja.

Vizuri kufika katika huduma za afya pale unapoona una dalili zisizo za kawaida.