Uchoraji wa Tattoo unaweza kukunyima fursa hizi

Sunday May 12 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

kila mchoro (tattoo) unaowekwa mwilini huwa na maana yake.Wengine wanachora kwa kujifurahisha lakini wakati mwingine huashiria furaha, huzuni au kumuenzi mtu.

Japo ni urembo uliodumu kwa miaka mingi, kila mtu kuchora na wengine kuthubutu kufanya hivyo ili kudhihirisha upendo kwa wale wawapendao lakini wakati mwingine inaweza kuwapatia madhara na kuwanyima fursa siku za usoni.

Mara nyingi watu huonekana kuchora tattoo kifuani, mkononi, mgongoni sehemu zinazoonekana au wakati mwingine huchorwa katika sehemu ambazo ni ngumu kuonekana.

Unapozungumzia tattoo inamanisha uwekaji wa wino kwenye ngozi ya ndani kitaalamu kama ‘dermis’ kwa kutumia kitu chenye ncha kali.

Mfano mzuri wa watu waliochora tattoo na kufanya ngozi za miili yao kubadilika ni mwanamuziki kutoka nchini Marekani, Lily Wayne ambaye amechora tattoo karibu kila sehemu ya mwili wake hadi usoni.

Hapa nchini watu maarufu na wasanii wameonakana kuchora tattoo katika miili yao miongoni mwao wakiwemo Nasibu Abdul, Irene Uwoya, Shilole, Wema Sepetu, Jackline Wolper na wengine wengi.

Suala hilo limewafanya kuonekana tofauti na watu wengine hasa katika soko la muziki na filamu wanaoufanya.

Lakini baadhi ya vijana wanaoiga kuchora tattoo za maisha wamekuwa wakikosa fursa walizozitamani na wengine wamekuwa wakiponea chupuchupu.

Mfano katika mashindano ya ulimbwende hayaruhusu mtu mwenye tattoo inayoonekana kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.

Suala hilo liliwahi kudhihirika kwa Rachel George ambaye alikuwa akishiriki mashindano hayo ngazi ya wilaya jijini Dar es Salam.

“Ilibaki kidogo nitolewe lakini nikawahi kuifuta na kwa sababu haikuwa kubwa sana kovu halikuleta shida na rangi ya ngozi yangu nyeusi ilisaidia katika kuficha uangavu wa kovu lile,”

“Nilikuwa naogopa kufuta kwa namna yoyote ile lakini nikakumbuka kuwa dawa ya nywele ikiwekwa kichwani huwa tunaungua nikaamini inaweza kufuta, nikafanya hivyo na matokeo yakawa kama nilivyo tarajia,”

“Kiukweli ilinipa wakati mgumu, nilifikiria mazoezi yote niliyofanya sawa, muda pesa vyote ni sawa na kazi bure sikutamani iwe hivyo bali kufuta ikawa chaguo sahihi,”

Rachel anasema japokuwa hakubahatika kushinda katika kinyang’anyiro hicho lakini alitwaa taji la Miss Personality.

Lakini siyo huko tu bali zipo hata sehemu nyingine kama jeshini, lakini pia kuna kampuni mbalimbali zinazoendeshwa kwa imani za madhehebu ya dini huwa ni ngumu kutoa fursa za ajira kwa watu wenye michoro hiyo.

Lakini hakuna asyejua kuwa msanii wa TMK Wanaume family, Amani Temba ni miongoni mwa watu waliowahi kutolewa katika kazi yake

Kwa mujibu wa simulizi za maisha yake kabla na baada ya kuhitimu mafunzo yanayoonyesha alikuwa akipenda kuwa mwanajeshi, ukweli ni kwamba Temba, alifanya kila awezalo na kufanikiwa kujiunga na mafunzo ya jeshi zaidi ya mara tatu, na mara zote alifanikiwa kuhitimu mafunzo, lakini mara nyingine kabla hajakabidhiwa ajira anajikuta anaachishwa au anaacha na kisha anarudia tena mafunzo.

Huu ni ushahidi kwamba alikuwa akiipenda kazi hiyo kutoka moyoni lakini kwa sababu ya tattoo aliyonayo ilikuwa ikimkwamisha na sababu hii inaweka bayana kwamba kamwe hataweza tena kuwa mwanajeshi kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kimataifa.

Lakini watu waliochora tattoo hukosa pia fursa ya kuchangia damu hata ikiwa ni kwa dharula hiyo ni kutokana na uwepo wa hatari ya kusambaza ugonjwa kwenda kwa mtu mwingine, kimsingi mtu aliyechora ndani ya muda mfupi ndio haruhusiwi lakini kwa sababu wakati mwingine sio rahisi kutofautisha tattoo mpya na ya zamani.

Daktari kutoka hospitali ya Anglikana Buguruni, John Nelson anasema watu wenye tattoo mara nyingi wanakataliwa kuchangia damu kwa sababu wengi huusishwa na utumiaji wa vilevi pamoja na madawa.

Mbali na hilo pia katika uchoraji wa tattoo kwa sababu vitu vyenye ncha kali ndiyo hutumika huenda mhusika asizingatie suala usalama wa vifaa vyake vya kazi

Kitaalamu

Mbali na kuweka makovu yasiyofutika katika mwili pia kwa mujibu wa Dk John Haule uchoraji wa tattoo huweza kuleta magonjwa ya ngozi kwa wachoraji ikiwemo vipele katika michoro yao, allergy (mzio).

“Miongoni mwa madahara hayo pia wnaweza kupata saratani, kwa sababu unapotoboa layer ya juu ya ngozi ya binadamui na kuweka wino wenye kemikali huweza kuleta madhara tofauri kati ya mtu mmoja na mwingine,”

Jamii haikubali tattoo

Ingawa katika maeneo ya mijini utamaduni huu unakuwa, kwa kiasi fulani jamii duniani kote haikubaliani na utamaduni huo na wachache wanaofanya hivyo huonekana watukutu.

Zipo baadhi ya kazi huwezi kupata nafasi hata kama haijaandikwa katika miongozo ya taaluma fulani.

Advertisement