Ugonjwa wa moyo unaua wanawake zaidi kuliko wanaume

Dar es Salaam. Wanawake wamekuwa wakikumbwa na tatizo la vifo vya ghafla. Umeshawahi kujiuliza sababu? Kama unataka mama, mke au ndugu yako wa kike aishi miaka mingi, kuna ushsuri wa kisayansi.

Tatizo hili linaweza kusababishwa na tukio linalogusa hisia. Inaweza kuwa kifo cha mpendwa au talaka, kuvunjika kiungo au kukatika, kukataliwa au kusalitiwa na mpenzi na hata furaha kama ya kushinda bahati nasibu.

Uchunguzi wa wanasayansi na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo duniani, unaonyesha kuwa tatizo ugonjwa mshtuko wa moyo utakanao na hisia, ambao unaitwa broken heart syndrome na umekuwa ukiua wanawake wengi duniani.

Utafiti uliofanywa na wakfu wa British Heart Foundation nchini Sweden, ulioangazia matokeo ya wagonjwa 180,368 waliokumbwa na mshtuko wa moyo kwa miaka 10 umeonyesha idadi ya wanawake wanaokufa ni mara tatu zaidi kuliko wanaume.

Wakfu huo ulisema kuwa mshtuko wa moyo mara nyingi huonekana kama tatizo la wanaume, lakini wanawake hufa zaidi kutokana na magonjwa ya moyo hata kuliko saratani.

Watafiti wa chuo cha Leeds na taasisi ya Karolinska ya Sweden walikusanya takwimu zilizoonyesha kuwa wanawake walikuwa na uwezekano mdogo wa kupata matibabu yanayostahili baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo ikilinganishwa na wanaume.

Prof Chris Gale, wa Chuo cha Leeds aliyefanya utafiti huo anasema hali hiyo ni ya kushtua.

Mkuu wa kurugenzi ya tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Delila Kimambo ameieleza Mwananchi sababu za wanawake wengi kuwa katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya moyo.

Mshtuko wa moyo

Dk Kimambo anasema saratani inawakumba sana wanawake ni shingo ya kizazi, lakini kuna tatizo kubwa la wengi kufariki vifo vya ghafla vinavyotokana na mshtuko wa moyo na mara nyingi wengi chanzo chake ni moyo kuathirika kupita kiasi, au brokenheart syndrome.

“Ugonjwa huu unawapata wanawake waliopata matatizo makubwa. Anaweza kuwa amefiwa na mume, roho ikamuuma sana; amepoteza kazi akapata matatizo; mambo ya kifamilia au mahusiano. Unakuta moyo wa mwanamke unabreak kupita kiasi,” alisema.

“Wanaume huwa hawapati sana hili tatizo la broken heart syndrome.”

Anasema kwa Tanzania, baadhi ya wanawake wamekuwa wakifika hospitalini wanapopatwa na tatizo hilo na hivyo kushughulikiwa mapema, lakini wengi huchelewa na hufariki ghafla.

“Wanawake wanaopata mshtuko mkubwa wa moyo utokanao na tatizo hili, akirudi nyumbani hasemi au ataishia kusema tu ‘nasikia nimechoka’, analala au kukaa na kupoteza maisha,” anasema.

“Kinachochelewesha wagonjwa wa aina hii kupata matibabu ni kuwa hakuna anayeona tatizo zaidi ya mhusika kulalamika amechoka. Akisema hivyo, wanaomzunguka humwambia anafanya kazi nyingi hivyo apumzike badala ya kuonana na wataalamu kujua ana tatizo gani.

“Au wengine hawalali vya kutosha. Mtu anatakiwa alale saa nane lakini hafanyi hivyo. Unakula sana vitu visivyopangiliwa basi unaishia kupata matatizo na kuna magonjwa yanayowapata wanawake wengi yatokanayo na uzito uliopindukia, anaweza kuwa na tatizo la moyo na asitambue.”

Anasema wamekuwa wakiwashauri wanawake kupunguza uzito, kula vyakula kwa mpangilio na kupata muda kupumzika.

“Kikubwa ni kuacha kutiana moyo kipindi cha matatizo kwamba ‘wewe utakuwa vizuri’,” anasema.

“Wale wanaokuwa na presha kipindi cha ujauzito inatakiwa warudi kuangalia presha kama imeisha. Lakini (mara nyingi) akishajifungua anafurahia mtoto na anasahau alikuwa na presha. Anakula vyakula vya uzazi tatizo linazidi kukua ndani kwa ndani.”

Dk Kimambo anasema unyonyeshaji kuwa ni sehemu nzuri iliyowezesha wanawake kujiepusha na magonjwa ya moyo.

“Mama akinyonyesha mtoto atapungua uzito, hatari ya kupata maradhi ya moyo itapungua,” anasema.

Dk Kimambo anataja suala la kupunguza uzito, maarufu kwa jina la diet, ni chanzo kikuu cha kusababisha magonjwa ya moyo kwa wanawake wengi.

“Wanawake wengi hivi sasa wanafanya diet ila changamoto ni za muda mfupi na kitu chochote cha muda mfupi hakina matokeo mazuri na huathiri mwili kwa namna nyingi,” anasema.

Mbinu za kupunguza magonjwa ya moyo

Dk Kimambo anasema unaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo kwa kufuata mtindo bora wa maisha ikiwamo kutumia mafuta kidogo na kuepuka yale yatokanayo na wanyama.

Kuongeza matumizi ya nafaka hasa zisizokobolewa kama unga wa dona, unga wa atta, ulezi na mtama. “Kuongeza pia ulaji wa vyakula vya jamii ya kunde, mbogamboga na matunda na kufanya mazoezi ya mwili angalau dakika 30 kila siku,” anasema.

Vihatarishi

Dk Kimambo. ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, pia anasema mfumo wao wa maisha ni sababu nyingine inayowafanya wanawake na wanaume kuwa hatarini kupata magonjwa ya moyo.

“Wote wana hatari, isipokuwa kuna utofauti mdogo ikiwamo ugumu wa kumgundua mwanamke kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

“Mtu anapolalamika kuchoka, huambiwa anafanya kazi nyingi hivyo apumzike,” anasema.

Dk Kimambo anasema mtu huyo ni muhimu kushauriwa aonane na daktari ili kujua chanzo halisi cha tatizo lake.