Ukeketaji na mapambano ya kumnasua binti

Sunday May 26 2019

 

By Jonathan Musa, Mwananchi

Mara nyingi neno ukeketaji linapotajwa, wengi huelekeza akili na fikra zao mkoani Mara.

Idadi kubwa ya watu wameubadilisha mkoa huo na kuupa jina la unyanyasaji kutokana na baadhi ya mila na vitendo vya kikatili vinavyoripotiwa mara kwa mara, ingawa mapambano ya kumnasua binti kutoka katika desturi za ukeketaji zimekuwa zikifanyika.

“Sidhani kama ni mkoa wa Mara tu, hii ni kwa sababu walikuwa wakilifanya mchana kweupe na watu wanakuwa wanaangalia.”

Hiyo ni kauli ya Hosea Malama ambaye ni mwanasaikolojia anayeishi katika Mji wa Tarime. Anasema mkoa huo umekuwa alama ya ukeketaji kutokana na baadhi ya watu kufanya vitu hivyo vinavyopigwa vita duniani kote.

Ofisa maendeleo ya jamii mkoa wa Mara, Neema Ibamba, anasema mila potofu zimekuwa zikiwalazimu walezi na wazazi kuwakeketa watoto wao.

Ametaja mila hizo kuwa ni pamoja na kuzuiwa kufungua zizi, kutowasalimu wazazi wakati wameamka na pia kujihusisha na shughuli zozote kama za sherehe.

Advertisement

“Mabinti wengi wanazielewa mila hizi kwamba kama hujakeketwa na umebahatika kuolewa hapa ndani ya hii jamii, kuna baadhi ya vitu huwezi kuvifanya. Huwezi kuwatangulia wenzako kuamka, kwa maana ya kufungua geti. Huwezi kuamkia wazazi (mama na baba mkwe) na mambo mengine,” anasema Ibamba.

Anaongeza kwamba kuna baadhi ya wazazi wanatoa vitisho vya laana na kusitisha huduma nyingine muhimu iwapo binti akigoma kukeketwa. Jamii ya Wakurya wana jina maalumu kama ‘Ilikunena’, huyu ni mwanamke aliyeolewa kabla hajakeketwa na anaweza kufanyiwa hivyo wakati akijifungua kama atakuwa ametokea jamii nyingine.

Mmoja kati ya mabinti waliokeketwa ambaye alikataa kutajwa jina, amesema mabinti wengi wanashawishika na maneno kutoka kwa wazazi wao kwamba wasipofanya hivyo watalaaniwa.

Udhibiti wa ukeketaji

Aidha diwani wa kata ya Sirari wilayani Tarime, Nyangoko Paul, anasema uwepo wa jamii moja kati ya Kenya na Tanzania imekuwa ni kichocheo kikubwa cha kushindwa kudhibiti ukeketaji kwa mabinti.

“Hapa mpakani asilimia 98 ni jamii moja tu ya Wakurya na ndivyo ilivyo hata ukivuka upande wa pili, Kenya. Mara nyingi tukizuia hapa kuna wale wazazi vichwa vigumu na wasiojali afya za watoto wao, wanaamua kuwapeleka kwa ndugu zao Kenya wanakeketwa na wanarejea hapa wakiwa tayari walishapona,” amesema Nyangoko.

Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Tarime Glorrious Luhoya amesema licha ya kuibuka na changamoto mbalimbali bado wanaendelea na mikakati ya kuwakamata wahusika wote ambao wanawakeketa mabinti.

“Hakuna Serikali ambayo inaweza kuruhusu zoezi hilo, tunawakamata wahusika,” amesema Luhoya.

Kauli sawa na hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima ambaye amefafanua kwamba pamoja na wakeketaji kukamatwa, pia wanawabana viongozi wa mila na wa serikali za mitaa ambao si wadhilifu lakini pia wasioonyesha ushirikiano katika kulidhibiti hili.

“Mambo haya yamekuwa yanatokea kwa kuvizia tu lakini kila tukimkuta mhusika amefanya au ameruhusu kitendo hiki cha ukeketaji, tunamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” Malima.

Madhara ni makubwa

Dk Andrew Kilonzo, mtaalamu wa magonjwa ya watoto na wanawake jijini Mwanza, anasema madhara yatokanayo na ukeketaji ni makubwa licha ya watu kuyapuuza.

Anasema madhara hayo ni pamoja na kutokwa na damu nyingi. Uambukizo unatokea iwapo vifaa vilivyotumiwa havikuwa safi. Uambukizo unaweza kuenea mpaka katika viungo vya ndani vya uzazi na kusababisha ugumba na hata vifo.

Pia, kuna hatari ya kuambukizwa VVU au kuziba kwa mkojo na damu ya mwezi (hedhi) ndani ya mwili wa mwanamke na kusababisha uambukizo.

Mengine ni maumivu makali wakati wa kujamiiana na wakati wa kujifungua kutokana na kupungua ukubwa wa uke. Ukeketaji wa wanawake mara nyingi una madhara ya kisaikolojia ambapo wasichana hupoteza tumaini na imani kwa walezi au wazazi na wanaweza wakapata mateso ya kujisikia waoga, kufadhaika, kutojiweza na kutokuwa kamilifu kimwili.

Zaidi ya hayo, ukeketaji unampunguzia mwanamke hamu ya kujamiiana. Kufanikisha hamu ya ngono inategemea kwa kiasi kikubwa viungo vya uzazi vya nje. Ukeketaji hata hivyo unaharibu umbile na kazi za viungo vya uzazi vya nje vya mwanamke.

Aidha Dk Cecilia Protas kutoka Hospitali ya Rufaa, Bugando jijini Mwanza, amesema ukeketaji una madhara kimwili na kisaikolojia ambapo mara nyingi huleta matatizo ya mahusiano ya kimwili kati ya mwanaume na mwanamke.

“Sehemu ya ndani ya mashavu na ya juu kwa kiasi kikubwa vinahusika na kiwango cha raha ya na kufikia mshindo wakati wa kujamiiana.”

Endapo mwanamke amekatwa vibaya sana au uke umeshonwa, kuna uwezekano wa kupata maumivu na matatizo wakati wa kujamiiana na wa kujifungua.

Mratibu wa dawati la jinsia mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya, Claud Mtweve amefafanua kwamba ukeketaji umekuwa ukichangia visa vya kiuhalifu ikiwemo wizi wa mifugo kutokana na sherehe zinazofanyika.

“Ukiangalia watoto wadogo wanaokeketwa, wanabadilika hadi tabia maana wanakuwa wameaminishwa kwamba sasa wao si watoto tena na hivyo wanaanza kiburi na mambo mengine mabaya,” anasema Mtweve.

Sabasi Mwikwabe 81, ambaye pia ni mzee wa kimila kutoka jamii ya Wakurya kwenye mahojiano maalum na Mwananchi, amesema anashangaa ni kwa nini nguvu itumike kudhibiti ukeketaji huku mambo mengine yakiwa bado yapo.

“Zamani Wakurya walikuwa wanakata masikio kama sehemu ya kudumisha mila, mbona ilikuja ikaisha tu bila shinikizo au kwa kuwa masikio si sehemu ya siri?,” amehoji Mwikwabe.

Mwaka 2016, jumla ya mabinti 4,148 waliokolewa kutoka kwa ukeketaji huku 1,473 wakiathirika na kitendo hicho wilayani Serengeti mkoani Mara.

Advertisement