USHAURI WA DAKTARI: Unywaji pombe kwa mjamzito si salama

Sunday September 29 2019

 

Unywaji pombe upo kwa wanaume na wanawake lakini kwa mjamzito huwa ni jambo hatari kiafya kwake na mimba aliyobeba.

Kwa kawaida pombe huingia mwilini kupitia mdomoni na kufika kwenye mfuko wa chakula na haraka ndani ya dakika chache huwa tayari imeisha nyonywa na kuzunguka katika mzunguko wa damu.

Mjamzito katika nyumba ya uzazi huwa amebeba mtoto ambaye anapitia hatua mbalimbali za ukuaji.

Baadhi ya wajawazito na wengine hawana ufahamu juu ya usalama wa mimba hiyo endapo mjamzito atakuwa anakunywa pombe.

Madaktari bingwa wa kina mama duniani hawakubaliani na kiasi chochote kile cha pombe kwa mjamzito kutumia, wanaamini kinywaji hicho hata kiwe kidogo kina madhara.

Yapo madhara ya wazi ambayo yameonekana kuwapata wajawazito wanaotumia pombe kupita kiasi, ingawa ni kweli wapo wanaoweza kutumia bila kupata madhara.

Advertisement

Madhara hayo yanaweza kujitokeza kwa mjamzito mwenyewe pamoja na mtoto aliye katika nyumba ya uzazi.

Madhara hayo ni pamoja na kutoka au kuharibika kwa mimba, mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, ulemavu wa mbavu, kidari, mgongo wazi au kupinda, vidole kuungana au kuzaliwa na kichwa kidogo kuliko kawaida.

Mengine ni pamoja na kuzaliwa na hitilafu za kimaumbile puani, taya, kupata tatizo la uoni hafifu, matatizo ya moyo kama vile moyo kuwa na tundu, matatizo ya figo, mtoto kuwa na ubongo mdogo na matatizo ya akili.

Tafiti iliyowahi kuchapishwa katika jarida la utafiti wa saratani la Marekani (JAACR) linaonyesha kuwa unywaji wa pombe wakati wa ujauzito unahusishwa na kutokea aina mojawapo ya saratani ya seli nyeupe ya damu kwa watoto.

Kwa kawaida madhara haya huwa si ya muda bali huwa ni ya kudumu ambayo yanaweza kusababisha kifo kwa mtoto baada ya kuzaliwa na vile vile yanaweza kusababisha kuwa mzito kiakili (uelewa).

Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito ni kweli kwamba si kila mtoto anaathiriwa na unywaji huo ingawa hatari ya kuathirika ni kubwa zaidi.

Sababu ya baadhi ya wajawazito kunywa pombe lakini hawapati madhara haya ni kutokana na miili yao kuwa na uwezo wa kujihami na kusahihisha athari zinazoletwa na pombe.

Madhara haya yanaweza kuletwa na aina zote za pombe ikiwamo bia, pombe kali na mvinyo.

Ni kweli si watoto wote wanaopata madhara haya, lakini ukweli wa kisayansi unadhihirisha kwamba pombe si salama kwa wajawazito.

Ni muhimu kwa mjamzito kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya usalama wake na ujauzito kwa kuepuka kunywa wakati akiwa katika hali hiyo ili kuepukana na athari zinazoweza kutokea.

Kwa yule atakayeshindwa kuacha basi anywe kwa kiasi angalau asizidishe chupa mbili kwa wiki.

Advertisement