Usichokijua kuhusu mafuta ya nazi

Mikoa mingi hapa nchini kuna mvua, bila shaka kuna hali ya baridi pia ukiachilia Dar es Salaam, ambako mvua inaweza kuwapo na kusiwe na baridi au hali hiyo isidumu sana.

Kunapokuwa na mabadiliko ya hali ya hewa, kwa maana ya baridi, joto kiangazi, mapambo pia hubadilika kulingana na nyakati hizo.

Katika makala haya tutaangalia namna ya kutumia bidhaa za asili kuifanya ngozi iendelee kuwa laini wakati wa baridi.

Achana na mafuta ya viwandani. Mafuta ya nazi yana wingi wa fatty acids ambazo husaidia kuipa ngozi unyevu nyevu muda wote.

Unachotakiwa kufanya ni kupasha mafuta ya nazi yawe ya uvuguvugu kiasi kisha paka kwenye ngozi.

Ukishayapaka licha ya kusambaa usijali yanavyofanya kazi, lala nayo usiku mzima yaani usiende kuyaondoa, ndiyo maana unashauriwa kuyapaka ukiwa umeshaoga.

Kwa matokeo mazuri, unaweza kuyapaka hata mchana na ukashinda nayo kutwa nzima.

Mafuta ya nazi yapo mengi ambayo hayana harufu, ukitengeneza nyumbani weka vitu kama karafuu, maua ya zeituni ili kuyakata harufu.

Usisahau kupaka mwili mzima hadi nyayoni, kwani pia hulainisha nyayo.