USHAURI WA DAKTARI: Viashiria kuwa una tatizo la moyo

Una umri wa zaidi ya miaka 45 unapiga hatua chache tu unahisi kuchoka haraka na kupumua kwa shida isivyo kawaida.

Kiashiria kama hiki siyo chakupuuzia hata kidogo hasa kwa watu wenye miaka 45-60 kuendelea, wenye unene uliopitiliza, kisukari, kiwango kikubwa cha lehemu mbaya (cholestrol) na shinikizo la damu.

Sababu kubwa ni uwezekano wa viashiria hivyo kuwa ni vya magonjwa ya moyo, ingawa mara nyingi dalili zake huwa zinajificha. Mtu hujistukia ghafla amedondoka na kupoteza fahamu bila kuwa na dalili yoyote.

Magonjwa ya moyo yameshika kasi kwa sasa ni namba moja katika kusababisha vifo vya ghafla hivyo ni vizuri kujihami mapema angalau kwa kupata ufahamu wa viashiria vyake.

Moja ya kiashiria muhimu vya mtu yeyote kufahamu ni kuchoka kirahisi baada ya kupiga hatua chache, hali hii huambatana na kubanwa au kukatika kwa pumzi.

Mfano mzuri ni pale mtu anapopanda ngazi anaweza kuhisi kuchoka huku akitweta na kupumua kwa tabu.

Uwepo wa maumivu ya kifua ni kiashiria ambacho hakiepukiki kupuuzwa kwa watu wazima. Maumivu hayo yanaweza kuwa yakubana au kukamua. Unaweza kuhisi kama kuna uzito fulani kifuani mfano kama vile kuna mtu anakukanyaga kifuani.

Maumivu hayo ya kifua yanaweza kuongezeka wakati mwili unapojongea au kufanya zoezi na vilevile kunapokuwepo na badiliko la hisia za kimwili (emotional stress).

Maumivu hayo huwa zaidi upande wa kushoto wa kifua na unaweza kusambaa katika bega na kushuka chini ya mkono wa kushoto.

Maumivu hayo yanaweza kutulia kwa dakika kadhaa pale unapoacha kufanya kazi au zoezi.

Kwa baadhi ya watu hasa wanawake wanaweza kupata maumivu makali yanayosambaa katika shingo, taya, mgongo na mkono.

Mabadiliko ya mapigo ya moyo kama vile kudunda kwa kasi isivyo kawaida au kudunda ovyo ovyo ni kiashiria kinachoweza kujitokeza pale kunapokuwa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Maumivu makali ya kichwa yanayoambatana na kuona mawimbi au giza na kupoteza fahamu ghafla.

Kupata kichefu chefu, kuhisi kujaa tumbo na kupata kiungulia pasipo uwepo wa matatizo ya mfumo wa chakula. Kukoroma kusiko kwa kawaida wakati wa usingizini.

Kutokwa la jasho la baridi pasipo sababu maalum na kupata kikohozi kisichoisha na kujaa/kuvimba miguu ikiwamo katika vifundo vya miguu.

Ni vizuri kwa yeyote atakayekuwa na viashiria na dalili hizi kufika katika huduma za afya mapema kwa ajili ya uchunguzi, matibabu au ushauri.

Jenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa jumla wa kiafya angalau mara moja kwa miezi sita.