TUONGEE KIUME: Wafahamu Mabaharia wa kike wa nchi kavu

Tumeshaitwa ma baharia sana mjini na tumeshajiita mabaharia vya kutosha. Sasa ni muda wa kujipa mapumziko na kuanza kuwazungumzia mabaharia halisi; mabaharia wa kike wa nchi kavu.

Baharia wa kike wa nchi kavu ni yupi? Ni yule ambaye unakutana naye asubuhi kwenye mgahawa, unajifanya mwanaume wa shoka, unamlipia alichokuwa anakula kisha unaomba namba ya simu unapewa.

Baadaye kidogo unamtumia meseji ya kumtongoza unapita bila kupingwa na hapo hapo anaanza kukuita majina mazito mazito ya mahaba mume wangu, baby na mengine yote ambayo hujawahi kuyasikia.

Mapenzi yanapamba moto ndani ya masaa machache tu tangu yaanze mpaka unashindwa kuelewa huyu baharia alikuwa anakupenda pia au kuna kitu anatafuta?

Mnapiga stori kwa meseji kisha ghafla anakutumia ujumbe; ‘mume wangu naomba ninunulie vocha au nipigie nina shida ya kuzungumza na wewe unaamua kumtumia vocha. Akiipokea anakujibu kwa meseji ‘Umenitumia 2,000? Nilijua utanitumia 5,000 nijiunge cha mwezi.’

Kisha usiku wa siku hiyo hiyo anakupigia simu kwa ile vocha yako ya 2,000 uliyomtumia unajiroga unaipokea, na cha kwanza kukwambia baada ya salamu ni ‘Baby nikuombe kitu?’ ukijibu ‘ndio’ tu umeisha.

‘Leo mama mwenye nyumba alikuja, kodi yangu imeisha. Halafu mimi nilikuwa nasubiria hela yangu ya vikoba tunavunja wiki ijayo ndo nimlipe sema ni Mswahili sana, atakuja kunidhalilisha, kwa hiyo naomba mume wangu unisaidie kulipa.’

Kama mwanaume unaona hili mbona ni tatizo la kawaida, ngoja nimlipie tu. Unakubali ukifanya hivyo unakuwa umejiroga kwa mara ya pili kwa sababu ndiyo utagundua kuwa hajamaliza.

‘Halafu baby hivi unanisikia vizuri kweli kwenye hii simu? Manake mchana nilienda kwa dada yangu ana mtoto mdogo, basi mtoto akaiangusha kutoka juu ya friji mpaka chini, sasa imeanza kusumbua mtandao, tachi haibonyezeki. Naomba kama una pesa kidogo, nisaidie kupata simu nyingine mume wangu.’

Hajamaliza

‘Halafu baby, hivi we unapenda mke wako nivae vipi?’ Anakuuliza. Unamjibu unachopenda na anageuza jibu lako kuwa fursa.

‘Ha ha haaa… jamani, mume wangu kweli tunaendana, manake hata mimi napenda hivyo hivyo. Halafu mchana nilipita Sinza, nikaona magauni marefu kama hayo unayoyapenda, ni mazuri mume wangu. Nikivaa nitapendeza… Sasa nilikuwa nasema kama una hela kidogo naomba nikanunue japo matatu.’

Bado anaendelea

‘Halafu baby hivi unajua ugonjwa wenye gharama kutibu kuliko wote ni pumu? Manake mimi mama yangu anaumwa pumu, inamsumbua balaa. Kesho yenyewe natakiwa nimpeleke hospitali, halafu sasa nikushangaze, nauli yangu imepungua. Basi kama una nauli niongezee nimpeleke mkweo hospitali. Manake bila mama usingejiua baby, au sio?’

Kamaliza.

Hawa sasa ndio mabaharia wa ukweli, sisi wanaume tunajiita mabaharia kwa kulazimisha tu.