USHAURI WA DAKTARI: Zingatia haya kama unataka kuacha kuvuta sigara

Kama ni mvutaji wa sigara basi pia unapaswa kufahamu ni kwa kiasi gani uvutaji wa sigara ulivyo na madhara kwa afya yako. Nimejaribu kufanya tafiti ndogo sana ya kuongea na ‘wavutaji mahiri’ na asilimia 90 ya wavutaji wanakiri kwamba wasingethubutu kujiingiza katika tabia ya uvutaji wa sigara kama wangekuwa na uwezo wa kurudisha muda wao nyuma. Uvutaji wa sigara unachochea mazingira hatarishi ya magonjwa ya moyo, saratani ya mapafu, kifua kikuu, saratani ya damu na pia kupoteza nguvu za jinsia hususani kwa wanaume. Na cha kuhuzunisha zaidi magonjwa haya yote ni rafiki wa karibu wa wavutaji wa sigara na tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya nusu ya wavutaji wa sigara wanakufa mapema kutokana na kitendo hiki.

Kwa wewe ambaye umekuwa mtumwa wa kuvuta sigara, nakutia moyo kuwa bado hujachelewa sana kuchukua uamuzi wa kuacha kuvuta sigara na utapata manufaa makubwa sana kiafya kutokana na kuacha kuvuta sigara ndani ya mwaka wa kwanza kabisa. Na hata kama utakua tayari ni mwathirika wa magonjwa yatokanayo na uvutaji wa sigara, kuacha uvutaji wa sigara utaisaidia kuzuia hali ya afya yako kuwa mbaya zaidi.

Kwa kusoma makala hii ya jinsi ya kuacha kuvuta sigara ni hatua ya mwanzo na tayari umeshaanza kuichukua. Kinachofuata ni kutafuta mtu anayeweza kukusaidia katika kampeni hii binafsi ya kuacha kuvuta sigara ambaye atakusaidia zaidi kukushauri. Siku hizi kuna maelfu ya huduma za kusaidia kuacha uvutaji wa sigara. Wahudumu wa afya kwa ujumla, pia tupo mstari wa mbele katika hilo.

Tunakupatia tiba na ushauri pia. Tunaanza kufuatilia hali ya tabia yako ya uvutaji, ndipo tunajua tiba sahihi itakayokufaa lakini ni baada ya kukufanyia vipimo kujua ni kwa kiasi gani tatizo hili limekuathiri kimwili na kiakili pia.

Kwa nini unahitaji ushauri?

Uvutaji wa sigara ni vyema ikatambulika kuwa ni ulevi kama vilivyo vilevi vingine na wakati wote sio rahisi kuacha kutokana na uraibu. Hivyo ni vyema kwenda kwenye vituo vya ushauri na matibabu ya dawa za kulevya na hapo utakutana na washauri wa magonjwa ya akili na madawa ya kulevya ikiwemo hili la uvutaji wa sigara ambao wamepatiwa mafunzo ya kutosha kufuatilia mazingira yako yanayokushawishi uendelee kuvuta sigara.

Pia tutaangalia kwa namna gani ya kukusaidia kufanikisha azma ya kuacha kuvuta sigara.

Watakusaidia pia kukupa ushauri wa kisaikolojia namna ya kupambana na matamanio ya kukufanya uanze tena uvutaji wa sigara.