Mhitimu wa chuo kikuu aliyejiajiri katika kilimo cha matango

‘’Nilipomaliza shahada yangu ya ualimu Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) mwaka 2017, nilitafuta ajira kwa kupeleka maombi katika shule mbalimbali, lakini matokeo yake sikuitwa” anasimulia Raymond Jura.

Baada ya kusota kwa muda akitafuta ajira, aliamua kujitolea kufundisha baadhi ya shule kwa ujira mdogo, lakini nako alishindwa kuendelea na kazi hiyo ya ualimu na mwisho akaamua kujiingiza katika kilimo.

“Nilianza kilimo cha matango kwa majaribio kwa kununua mbegu ya Sh2,500 na kupanda, lakini baadaye niliongeza fedha na kuwa na mtaji wa kama Sh25,000 na kulima robo ekari,” anasema.

Safari yake ya kilimo cha matango ilianza miaka miwili iliyopita, lakini kwa sasa mtaji wake umeimarika kiasi kwamba ameweza kuongeza kilimo cha nyanya chungu kutokana na mtaji huo wa matango.

“Niseme kwamba kupitia kilimo hiki, nimeanza kuona mafanikio japokuwa bado nina safari ndefu ya kufikia ndoto zangu, lakini kuna vitu naendelea kujifunza katika kilimo,” anasema Jura.

Jura anasema kilimo alikianza miaka miwili iliyopota kwa kulima robo ekari katika kijiji cha Kiroka, wilaya ya Morogoro Vijiji.

Sababu ya kulima matango

Anasema sababu kubwa iliyomvutia kulima matango ni kutokana na zao hilo kutokuwa na changamoto, pia halichukui muda mrefu kuvunwa tangu linapopandwa na uvunaji wake hauna gharama kama mazao mengine.

“ Nilivutiwa na kilimo hiki cha matango kutokana na uvunaji wake, lakini pia hakina usumbufu tofauti na mazao mengine” anasema.

Anasema kabla ya kuanza kulima matango aliamua kwenda kupata mafunzo ya kilimo, ambayo anansema yamemsaidia.

“Nilipolima kwa mara ya kwanza sikufuata kanuni za kilimo bora, matokeo yake sikupata mavuno yanayotakiwa, lakini baada ya kupata elimu ya kilimo chenye tija, sasa nitavuna mazao mengi,” anasema Jura.

Anasema bei ya zao hilo inabadilika kulingana na msimu, kwa kuwa kuna wakati hupanda na kufikia Sh300 kwa tango moja na kuna kipindi inapungua hadi kufikia Sh 100 kwa tango moja.

Soko lake

Jura anabainisha kuwa hana wateja wa kudumu lakini soko lake kubwa ni katika mnada unaofanyika kila siku ya Jumanne na Alhamisi, katika eneo la Kiroka Soweto.

Mbali na kuuza katika mnada, wateja wengine ni watu wanaouza magengeni na katika masoko yaliyopo eneo hilo, ambao hununua kwa jumla.

Anasema changamoto aliyoipata mwanzo ni mtaji mdogo hali iliyosababisha ashindwe kupata mavuno mazuri.

“Nikipata mtu wa kunishika mkono, nina uwezo wa kufanya mambo makubwa tu. Niko tayari hata kufanya mkataba na atakayekuwa tayari tukalima na kuja kugawana faida,” anasema Jura.

Mikakati

Anasema mikakati yake ni kuboresha maisha yake, kulima kitaalamu, kulima mazao mengine na kuongeza mashamba kwa ajili ya kilimo.

“ Nataka kuwekeza katika kilimo na kuendelea kujifunza kila aina ya kilimo, lakini pia kuajiri vijana wenzangu kupitia kilimo” anabainisha.

Faida ya matango mwilini:

Tango ni moja kati ya matunda yenye maji mengi kama vile tikiti maji, ambalo husaidia kupambana na joto kali ndani na nje ya mwili, lakini huondoa taka sumu mwilini na husaidia kuongeza vitamin ndani ya mwiili.

Matango yana madini ya potassium, magnesium na silicon kwa wingi ndio maana yanafaa katika tiba.

Vile vile husaidia katika umeng’enyaji wa chakula na kupunguza uzito kwa sababu tango lina maji mengi, hivyo ni zuri kwa kupunguza uzito, pia kutokana na nyuzi nyuzi zilizopo hufanya mmeng’enyo wako ufanyekazi vizuri.

Lakini ulaji wa matango mara kwa mara husaidia kuondoa tatizo la kukosa choo na husaidia kusafisha macho.

Pia matango huondoa harufu mbaya kwenye fizi zilizodhoofika na magonjwa, hivyo mtu anashauriwa kuchukua kipande cha tango na ubonyezee kwenye ukuta wa mdomo wako kwa ulimi kwa muda wa dakika moja hadi mbili, pythochemicals ambazo zipo kwenye tango zitaua bacteria waliopo mdomoni ambao wanasababisha harufu mbaya.