Tumia mbinu hizi kuchagua zao la kulima

Uchaguzi wa zao la kulima ni jambo muhimu sana katika shughuli nzima ya kilimo. Kwa kuchagua zao sahihi kazi ya uzalishaji hupunguzwa kwa kiasi kikubwa na hii ina maana ya ongezeko la tija.

Kufanya kosa katika kuchagua husababisha zao husika kukosa soko na kuongezeka kwa kazi ili kuhakikisha zao linapata soko.

Pia ni chanzo cha ubora duni wa zao na wakati mwingine kushindwa kabisa kuvuna zao husika.

Mazao ya shambani na bustanini yapo mengi, baadhi yake ni kama vile malisho ya mifugo, mazao ya mafuta, nafaka, mikunde, matunda, mboga, karanga, madawa, kambakamba na mbao.

Iwapo unalima zao kwa mahitaji yako binafsi au ya biashara, mambo yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa wakati wa uchaguzi wa zao.

Moja, hakikisha umepata elimu au ufahamu wa kutosha ya kuzalisha zao unalohitaji.

Mbili, hakikisha unapata uhakika kwamba unaweza kuzalisha zao husika kwa gharama nafuu kuliko kama ungeweza kulinunua. Mara nyingi inawezekana kununua kitu kwa bei rahisi kuliko itakavyokugharimu kuzalisha zao hilo.

Iwapo lengo litakuwa kuzalisha kwa ajili ya soko, basi yafuatayo yapaswa kufuatwa:

Moja, fanya utafiti wa kutosha kuhusu mahitaji ya soko kwa mazao mbalimbali na chagua zao lenye kuhitajika sana. Pia zingatia namna gani zao hilo linafaa kwa kuzingatia udongo na hali ya hewa ya mahali shamba lilipo.

Mbili, fikiria gharama zote za kuboresha shamba kama mabanda ya kudhibiti hali ya hewa isiyotakiwa (nyumba kitalu) au kupanda miti ili kuzuia upepo, au kuboresha rutuba ya udongo ili kuzalisha zao kwa haraka na kwa mafanikio.

Tatu, ni muhimu pia kujua ni rasilimali zipi zilizopo, mathalani watu, mashine, eneo, fedha, na mazao yapi ambayo kwa kulingana na rasilimali iliyopo yanafaa kulimwa.

Nne, fikiria uwezo wa zao kubaki katika ubora unaotakiwa kwa muda mrefu. Mazao ambayo huharibika haraka kama vile nyanya au maembe yanatia wasiwasi kuliko yanayodumu kwa muda mrefu kama vile mpunga.