Habari njema kwa wafugaji wa samaki

Saturday May 11 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Mtafiti mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amefanya utafiti na kugundua kwamba funza ni chakula kizuri kwa samaki wa kufugwa.

Mtafiti huyo, Dk Shadrack Ulomi amebaini pia kuwa mende na majani aina ya lusina na azolla, ni chakula muhimu kwa samaki kwa sababu vyakula hivyo vina protini nyingi ambayo inamsaidia samaki kukua haraka.

Mwananchi lilimtembelea Dk Ulomi katika maonyesho ya kazi za utafiti yaliyofanyika katika wiki ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuonyesha jinsi alivyofanya utafiti wa chakula cha samaki ambao utawasaidia wafugaji wengi wa samaki wasio na ujuzi huo.

Dk Ulomi anasema ufugaji wa samaki ni rahisi kama utakuwa na chakula cha kutosha chenye protini kwa wingi. Anasema ukuaji wa samaki unategemea zaidi protini inayopatikana kwenye vyakula husika.

Anabainisha kiwango cha protini kilichomo kwenye vyakula hivyo ni kama ifuatavyo: mende (asilimia 60 - 68), funza (asilimia 48), lusina (asilimia 25 - 29) na azolla (asilimia 19 - 30). Mbali na protini, anasema funza na mende wana madini mengine muhimu kama vile kalshiamu.

“Ukipata funza wako au mende unawakausha, unawasaga kisha unachanganya kwenye vyakula vingine vya kawaida kama vile pumba au mashudu. Nimejaribu chakula hicho nikagundua kwamba vifaranga vya samaki vikila vinakua haraka tofauti na vyakula vingine,” anasema.

Advertisement

Kuhusu upatikanaji wa vyakula hivyo, anasema ni rahisi tu kwa sababu majani yanapatikana, mende na funza pia wanapatikana kwa urahisi. Mtaalamu huyo anasema funza siyo uchafu bali ni hatua ya ukuaji wa nzi.

Uvunaji wa funza

Anasema mtu akitaka kuvuna funza, achukue chombo kama ndoo kisha aweke chakula kidogo au tunda na kuacha uwazi kwa ajili ya nzi kuingia. Baada ya siku tatu atakuta funza wengi kwenye chombo hicho.

“Funza siyo uchafu inategemea wako wapi. Nzi wanapenda kutaga mayai yao sehemu ambayo kuna chakula; kama chakula chake ni uchafu basi utawaona nao ni uchafu. Lakini kitaalamu funza na mende wana protini nyingi,” anafafanua Dk Ulomi.

Anasema chakula cha samaki ni pumba, mashudu, unga wa dagaa na mifupa lakini chakula hicho kinachanganywa na virutubisho vingine kama wanga, protini, mafuta, madini na vitamin ili kumpatia samaki virutubisho vyote muhimu.

Dk Ulomi anabainisha kwamba asilimia 65 ya gharama za ufugaji wa samaki ziko kwenye chakula, kwa sababu wanahitaji chakula chenye protini kwa wingi. Anasema kama samaki hapati protini ukuaji wake unadumaa.

“Utafiti wangu umejikita kwenye vyakula vya kawaida ambavyo vina protini nyingi lakini havina gharama zozote. Mende na funza wanapatikana kirahisi bila gharama zozote, majani ya lusina na azolla pia yanapatikana,” anasema.

Unaweza kufuga samaki

Mtafiti huyo anabainisha kwamba mtu akitaka kufuga samaki, lazima awe na ardhi kwa ajili ya kuchimba bwawa. Anasema ardhi ya bwawa hilo ni vyema ikawa ile ya udongo wa mfinyanzi.

Pia, anasema mfugaji anatakiwa kuchagua mbegu bora za samaki anaotaka kufuga na mbegu hiyo anaweza kuipata kwa urahisi kutoka ziwani au mtoni kisha kuhamishia kwenye bwawa lake la samaki.

“Samaki wanatofautiana katika ufugaji. Kwa mfano, perege unaweza kumfuga kwenye bwawa lolote, lakini kambale ukimfuga kwenye bwawa ambalo limejengewa hawazaani, ‘’ anasema.

Anaongeza: ‘’ Ukiweka wawili utawakuta wale wale siku zote. Wao wanapenda sana tope, kwa hiyo ukitaka kufuga usijengee bwawa lako, tafuta sehemu yenye udongo wa mfinyanzi,” anasimulia mtafiti huyo.

Anafafanua kwamba kina cha bwawa hakina budi kuwa mita moja na robo mpaka mita moja na nusu lakini upana wake ni uwiano wa vifaranga 8 – 10 wa samaki katika bwawa la mita moja ya eneo.

Anasema ikiwa bwawa lina upana wa mita za eneo 100, linaweza kuhifadhi samaki 800 mpaka 1000. Anasisitiza umuhimu wa kubadilisha maji kila inapohitajika kufanya hivyo.

Mahitaji mengine anasema ni chakula cha kutosha chenye virutubisho muhimu. Anasema perege wakilishwa chakula chenye protini kwa asilimia 35 au zaidi wanakua haraka na kuvunwa ndani ya miezi sita, lakini madume yanaweza kuvuliwa baada ya miezi minne.

Anashauri wafugaji wa samaki kufuga madume zaidi kwa sababu wanakua haraka ndani ya muda mfup tofauti na majike ambayo yanaweza yakaanza kutaga mayai wakati yana miezi mitatu wakati bado wadogo, hivyo kuathiri soko la mfugaji.

“Siku ya 3 – 21 tunaweza kubadilisha jinsia ya samaki kwa kuwalisha vyakula vyenye homoni ya kubadilisha jinsia. Ni vizuri wafugaji wa samaki wakafuga madume matupu, ni rahisi kupata mbegu nyingine,” anaeleza Dk Ulomi.

Kuhusu magonjwa ya samaki, anasema yapo hasa fangasi wanaosababishwa na kuozeana kwa chakula kwenye bwawa la samaki na kusababisha maambukizi ya fangasi. Pia, anasema fangasi wanaweza kuingia wakati wa kubadilisha maji, hivyo, amewataka wafugaji kuwa makini na maji wanayobadilisha ili kutosababisha maambukizi kwa samaki.

Advertisement