Njia nne za kutengeneza fedha kupitia zao la parachichi

Saturday April 27 2019

 

By Phinias Bashaya, Mwananchi

Haijalishi kama wewe ni mkulima ama la. Huhitaji kuwa mkulima ili ufanikiwe na kilimo cha zao la parachichi.

Katika mazingira ambayo zao hili sasa linachangamkiwa na watu wengi, mkulima na hata asiye mkulima anaweza kujitengenezea kipato kupitia zao hilo.

Makala haya yanaangazia njia kadhaa ambazo wewe usiyekuwa mkulima unaweza kutengeneza fedha kupitia zao la parachichi. Na kwa kuwa njia zote hizo ni fedha, ni dhahiri hata atakayelima, ana uhakika wa kujihakikishia soko la mazao yake.

Sharubati ya parachichi

Njia mojawapo ya kufurahia utumiaji wa parachichi ni kutengeneza sharubati au juisi. Utamu wa sharubati hii ndio unaolifanya tunda hili kuwa miongoni mwa matunda yanayopendwa na watu wengi nchini.

Sharubati hii unaweza kuinogesha au kuikoleza kwa kuongeza viungo vya aina mbalimbali kutokana na matakwa ya mtumiaji wa bidhaa hiyo.

Advertisement

Aidha, juisi ya parachichi inaweza kuchanganywa na maziwa ya soya au maziwa ya ng’ombe ili kuifanya kuwa nzito. Matunda na mbogamboga pia vinaweza kuongezwa kwenye juisi ili kuongeza ubora wa lishe kwa mtumiaji.

Ili kutengeneza juisi hii unaweza kukata vipande vya tunda hilo na kuchanganya na matunda mengine pamoja na sukari kisha kuyasaga kwenye blenda ili kutengeneza mchanganyiko utakaokupatia kinywaji kizuri.

Ukifanikiwa kuandaa juisi ya aina hii, kwa nini usijihakikishie soko kwa wateja wako hasa ikiwa mashari mengine kama vile ya ufungashaji bora na usafi na usalama wa bidhaa yako yatakuwa yamezingatiwa? Anza sasa kufikiria kufanya biashara ya kutengeneza sharubati ya parachichi.

Ni tunda zuri kuliuza

Hapa ndipo Watanzania wengi walipoangukia. Matumizi ya walio wengi ni kutumia parachichi kama tunda. Kwa sura hiyo, ukiamua kufanya biashara ya matunda, parachichi usiliweke kando.

Uzuri wake anaujua yule ambaye ambaye ameshalitumia.

Kama hujui waulize wataalamu wa afya wakupe utajiri wa virutubisho vilivyomo kwenye tunda hili.

Kwa kifupi, parachichi linaelezwa kuwa na Vitamini A, inayosaidia kuimarisha macho kuona vizuri. Lina Vitamini B (B1-B12) ambazo husaidiaa mfumo wa misuli ya mwili kuwa sawa na kuuepusha mwili na matatizo ya neva.

Lina Vitamini C, inayosaidia kuimarisha ngozi, kwa sababu liko na mafuta, lina zaidi ya mara nne ya virutubisho vya vitamini C vinavyopatikana katika machungwa. Lina vitamini D-ambayo husaidia sana kuimarisha mifupa ya mwili

Aidha, lina vitamini E-hii ambayo husaidia kuimarisha seli za uzazi, linasaidia sana kuongeza nguvu na utengenezwaji wa seli za uzazi

Ikiwa parachichi lina sifa zote hizi za kiafya, nini kinakufanya usianze leo biashara ya kuuza tunda hili?

Umefikiria kutengeneza mafuta?

Kwa wale wanaojiongeza kijasiriamali, tunda hili linaweza kutumika kutengenezea mafuta. Ni mafuta yenye mvuto na manufaa muhimu katika mwili wa binadamu.

Ili kutengeneza mafuta mazuri, parachichi halitakiwi kuwa limeiva sana na ni muhimu liwe na mizizi midogo na tunda lisiwe na kasoro zinazotokana na matatizo ya uvunaji au kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Utakachofanya ni kuondoa mbegu na ngozi na kusaga nyama yeka, kisha changanya kwa dakika 40-60 katika joto la nyuzi 45-50oC ambapo hii ni hatua ya kutenganisha mafuta na maji kutoka kwenye matunda.

Wataalamu wanasema mafuta ya parachichi yanaondoa lehemu na kemikali zote zenye madhara mwilini. Dk Twahir Said anasema amekuwa akinunua tani 1o za matunda na hayo na kuandaa mafuta yanayofika lita 500. Anasema kila lita moja huiuza kwa bei ya Sh 30,000.

Unga wa parachichi

Matunda ya avocado yaliyovunwa yanaweza kukatwa vipande vidogo vidogo na kukaushwa ili kupata bidhaa bora iliyokauka.Baada ya kukaushwa inaweza kutengenezwa unga ambao una faida nyingi na unahifadhiwa kwa urahisi. Unga wa parachichi ukiwa tayari unaweza kutumiwa katika kutengeneza supu, mchuzi wa mboga, ‘ice cream’

Jifunze kilimo cha parachichi

Parachichi ni zao linalostawi katika maeneo yanayopokea mvua kati ya milimita 1000-1200. Kiwango cha joto kinachohitaji kwa matunda hayo ni nyuzi 20 hadi 24. Ni zao linalofanya vizuri katika udongo wenye asidi (ph) ya 5-7.

Kwa Tanzania, mikoa ya baridi kama vile Njombe, Iringa, Mbeya, Arusha, Morogoro, ni maarufu sana kwa uzalishaji wa zao hili. Zao hili linaweza kukuzwa kupitia miche iliyoandaliwa kwenye viriba au kitalu au unaweza pia kupanda mbegu moja kwa moja.

Andaa mashimo kwa ajili ya kupandia mapema kabla ya mvua za mwanzo kuanza. Umbali wa mche na mche uwe ni mita sita na mita sita mstari hadi mstari.

Hii ni kwa sababu mche hupanuka, hivyo huhitaji nafasi ya kutosha. Kina cha shimo na upana kiwe futi mbili.

Katika shimo, changanya udongo na mbolea ya samadi kiasi cha debe moja hadi mbili. Anza kupanda miche shambani mapema mara tu baada ya mvua kuanza kunyesha.

Hakikisha unapalilia mara kwa mara, ili kuondoa magugu yasiweze kuua miche. Kama ni wakati wa kiangazi, hakikisha unamwagilia maji ya kutosha ili udongo uweze kuwa na unyevu wa kutosha wakati wote.

Upuliziaji wa dawa ni muhimu ili kukinga magonjwa ya ukungu na wadudu kama vile inzi weupe, kimamba wekundu na wengineo.

Mara nyingi miparachichi haishambuliwi na wadudu wala magonjwa hivyo upuliziaji unahitajika kufanyika pale panapokuwa na ulazima au kwa kiwango kidogo.

Advertisement