Njia rahisi za kuzuia magonjwa ya kuku

Saturday April 27 2019

 

Watanzania wengi hivi sasa wamevutika kuwekeza katika ufugaji wa kuku. Ufugaji huo unalenga kuku wa kisasa au wa kienyeji.

Watu hawa wanajenga mabanda, kununua chakula, pamoja na kuku wakitarajia kupata faida kubwa kutokana na uwekezaji huo.

Hata hivyo, mradi unapoanza mambo huonekana kwenda sawa, mpaka mfugaji atakaposhtuliwa na mlipuko wa magonjwa ambayo hupunguza uzalishaji au kuua kuku wake kabisa.

Inapofikia hatua hii., mfugaji unaweza kufanya nini kupunguza hatari hii?

Uzoefu duniani kote unaonyesha kuwa kuweka banda katika hali ya usafi, kuwalisha kuku ipasavyo na kuwapatia maji safi, ndiyo mhimili wa kupambana na magonjwa kama mharo mwekundu, kipindupindu cha kuku na ndui.

Kuwa makini katika ufugaji wa kuku ni pamoja na kutoa chanjo kwa kuku, kuzuia magonjwa kama sotoka au ndigana na ndui.

Advertisement

Taratibu za kufuata ili kuzuia magonjwa

Moja, utunzaji wa nyumba ya kuku. Ni lazima nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote

Mbili, nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu

Tatu, hakikisha unaondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote

Nne, matandazo na taka zinaweza kuwa mbolea nzuri ya mboji kwa mimea yako.

Tano, fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.

Sita, weka sehemu za kutosha kwa ajili ya kuku kupumzikia. Pia viota vya kutosha na kuweka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.

Saba, hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku, kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa

Utunzaji wa kuku

Hapa napo unatakiwa kuhakikisha yafuatayo: Moja, toa chanjo muhimu kwa kuku ili kuzuia magonjwa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo. Chanjo huanza katika wiki ya kwanza (mfano chanjo ya kuzuia sotoka) na inaweza kurudiwa baadaye.

Mbili, epuka kuweka kuku wengi mahali pamoja. Ni rahisi magonjwa kuenea kwa haraka kuku wanaporundikana eneo moja.

Tatu, tenganisha vifaranga na kuku wakubwa (isipokuwa kutoka kwa mama), kwa sababu vifaranga ni rahisi na wepesi kushambuliwa na magonjwa.

Nne, weka mipaka na madaraja ya sehemu za kuku kuzunguka/kucheza.

Ulishaji

Moja, wapatie kuku chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini au maganda ya mayai.

Mbili, wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.

Tatu, safisha vyombo vya kulishia na kun-yweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.

Nne, nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi.

Tano, hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.

Sita, usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.

Kukabiliana na magonjwa

Moja, muone mtaalamu wa mifugo mara uonapo dalili zozote za kuumwa kwa mifugo yako.

Tenga na wapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.

Mbili, ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliyekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.

Tatu, endapo kuna mlipuko wa ugonjwa katika eneo lako, usiruhusu watu kutembelea banda lako.

Watu wanaweza kuleta maambukizi kwa miguu yao, katika viatu, nguo na mikono. Pia magari yanaweza kuleta madhara kwa mabanda yako kupitia matairi na upakuaji wa mizigo

Ukaguzi wa mara kwa mara

Moja, safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea pamoja na viota.

Mbili, ondoa kinyesi.

Tatu, waangalie kuku wako kwa umakini ili kujua afya na maendeleo yao.

Nne, ondoa matandazo machafu na kuweka mapya. Angalia uwepo wa wadudu na chawa, kisha utibu kama kuna ulazima.

Tano, ondoa uchafu wote unaoonekana bandani. Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa. Suuza na uache likauke. Puliza dawa ya kuua wadudu kisha weka matandazo mapya.

Makala haya kwa hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu.

Advertisement