ONGEA KILIMO : Serikali isaidie soko la mazao

Saturday May 4 2019

 

By Elias Msuya

Kitu pekee ambacho hakiwezi kuachwa au kumalizwa kujadiliwa ni changamoto katika sekta ya kilimo.
Changamoto hizi zinaanzia kwenye upatikanaji ardhi, pembejeo, mbinu za upandaji kwa maana ya mbegu bora, mbolea na dawa za kuua wadudu na baadaye soko.
Lakini kwa namna mtiririko huu ulivyokaa, changamoto niliyoitaja mwisho ndiyo iliyobeba dhana nzima ya kilimo; mkulima analima ili aondokane na umasikini. Hivyo lazima awe na soko la uhakika kwa mazao yake.
Mchango wa sekta ya kilimo umeendelea kuwa muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 ya Watanzania na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwa miaka yenye mvua za kutosha.
 Mathalani, takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka 2015 sekta ya kilimo ilichangia asilimia 29.0 ya pato la taifa ikilinganishwa na asilimia 28.8 mwaka 2014.
Mchango mkubwa katika pato la Taifa ulitokana na sekta ya kilimo, ikifuatiwa na sekta nyingine za kiuchumi.
Kwa kuwa asilimia kubwa ya  Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, mchango huo  unachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza umaskini.
 Nimejaribu kueleza yote haya ili kuonyesha namna kilimo kilivyo na umuhimu, hata hivyo Serikali inapasa kuweka juhudi katika upatikanaji wa soko la uhakika.
Takwimu za kwenye karatasi haziwasaidii wakulima, malalamiko kila siku yapo kwenye masoko tu siyo kwingine.
Ni hatari kuona nyanya zinaharibika kwa sababu mavuno yamekua mengi, au mahindi yanaozeana kwenye ghala kwa kuwa msimu huo watu wamevuna kwa wingi. Kwa nini kusiwe na utaratibu mzuri wa kuikabiliana na mavuno mengi?
 Jibu pekee ni kuongeza viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na mifugo, tazama katika mwaka 2015/2016, uzalishaji wa maziwa ulikuwa ni lita bilioni 2.14, lakini ni lita 167,620 tu ndizo zilizosindikwa.
Maana yake maziwa yaliyobaki yaliharibika au yaliuzwa rejareja kwa faida ndogo. Serikali iwasaidie wakulima kupata masoko, kwa kuwa ndani ya mchakato huo, Serikali itakusanya mapato  yake yatokanayo na kodi mbalimbali.

Advertisement