Breaking News

Wakulima sasa kucheka kupatikana kwa tiba ya muhogo mnyauko

Saturday July 13 2019

 

By Rosemary Mirondo, Mwanancho [email protected]

Rajabu Ali ni mkulima anayepambana kutimiza ndoto za familia yake kupitia zao la muhogo.

Ni zao lilikokumbwa na changamoto ya kupoteza mwelekeo kwa muda wa miaka miwili sasa, baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa muhogo mnyauko hivyo kuathiri uzalishaji.

Ndoto ya Ali anayeishi Bagamoyo mkoani Pwani ya kulitumia zao hilo kuendesha familia yake inaweza kuyeyuka; hali katika shamba lake ni ya kusikitisha. Anasema uzalishaji ulishuka kwa zaidi ya robo tatu, sababu ikiwa ni ugonjwa huo. Kwa kila hekta anasema aliambulia tani tatu pekee.

Ugonjwa wa muhogo mnyauko husababisha vidonda kwenye shina na kuathiri mizizi ambayo hugeuka rangi na kuwa ya njano wakati mwingine ya kahawia kwenye tishu zinazozalisha wanga na hivyo kuathiri muonekano wake.

Apata ahueni

Hata hivyo, baada ya changamoto nyingi Ali alifanikiwa kukutana na wataalam wa zao ambao walimshauri njia za kibioteknolojia zinazohusisha matumizi ya mbegu bora.

Advertisement

Baada ya kutumia njia hizo anasema uzalishaji uliongezeka kwa asilimia 100 na kufanikiwa kuvuna kati ya tani 40 na 45 kutoka kwenye hekta moja tu.

Zao la muhogo ni zao muhimu kwa ajili ya chakula huku majani yake nayo yakitumika kama mboga.

Zao hilo ni muhimu kwa binadamu kwa sababu lina uwezo wa kuhakikisha usalama wa chakula na kupunguza umasikini.

Changamoto ya Ali pia imemkumba Amina Ali anayeelezea namna ugonjwa huo ulivyoathiri mazao yake na kupunguza usalama wa chakula hasa nyakati za ukame wakati ni tegemeo lake.

“Ilifika hatua nilikuwa navuna nusu tani kutoka kwenye hekta moja jambo ambalo lilininyima usingizi na kunifanya nianze kutafuta ufumbuzi,” anasema.

Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Rasilimali za Kilimo, Mpango wa Ulinzi wa Mazao (CPP) na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), ugonjwa huu ni tishio kubwa kwa usalama wa chakula.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa tatizo la muhogo mnyauko lilionekana kwa mara ya kwanza ukanda wa Magharibi ya Tanzania na badaye kuripotiwa kuonekana ukanda wa Afrika Mashariki na Malawi

Muhogo mnyauko ni nini?

Muhogo mnyauko ni kirusi kinachosambazwa na mdudu anayejulikana kama “White Fly” ambaye amesababisha uharibifu mkubwa kwenye mazao ya mihogo.

Muhogo mnyauko husababisha maafa ya zao la muhogo katika Ukanda wa Afrika Mashariki hasa kwa kusababisha vidonda kwenye shina. Ugonjwa huo pia huathiri mizizi na kuwa na rangi ya njano, kahawia kwenye tishu zinazozalisha wanga na wakati mwingine kuathiri muonekano wake.

Ripoti zinaonyesha kuwa muhogo mnyauko sio tu hupunguza mavuno kwa jumla, pia hufanya mzizi usifae kwa matumizi ya binadamu.

Maeneo ambayo mihogo upanda nchini

Ripoti zinaonyesha kuwa asilimia 23.7 ya mihogo huzalishwa kwenye ukanda wa Ziwa na asilimia 13.7 kutoka maeneo ya Ziwa Nyasa ambako hutumika kama moja ya chakula kikuu.

Pia hulimwa katika ukanda wa Kusini kama chakula cha biashara na cha usalama wa chakula hasa wakati wa ukame na katika wilaya za Nachingwea, Ruagwa na Tunduru ni chakula cha pili baada ya mahindi.

Bioteknolojia kama suluhu

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania, kituo cha Selian, Dk Joseph Ndunguru anasema kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani milioni saba kila mwaka za muhogo, lakini baada ya ugonjwa huo uzalishaji umepungua hadi tani milioni tano na nusu.

Anasema takribani watu milioni 800 wanategemea mihogo kama chakula kikuu katika ukanda wa Jangwa la Sahara ikiwa ni pamoja na Asia wakati Afrika pekee angalau watu milioni 300 wanategemea kama chakula na wakati huo huo kama zao la kuzalisha mapato.

“Ikiwa mbegu bora zitatumika pamoja na taratibu nzuri za kilimo, inawezekana kuzalisha tani 40 hadi 45 katika hekta moja tu, lakini utafiti unaonyesha kuwa katika maeneo yaliyoathirika sana yanaweza kuzalisha tani tano tu,” anasema.

Anasema kwa sasa nchi inatumia njia za bioteknolojia ikiwa ni pamoja na kutumia njia ya tissue culture ambayo husafisha mbegu na badae ikithibitika kuwa ni safi hutumika kuzalisha.

Suluhisho jingine la bioteknolojia ni kupitia teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa kwa ajili ya ugonjwa unaosambaa haraka na hufanyika moja kwa moja shambani.

Aliongeza kuwa pia wapo kwenye hatua za kimaabara za kutafuta suluhu ya kiuhandisi jeni.

”Kwa kupitia bioteknolojia tumefanikiwa kuwafikia wakulima na mbegu bora kwa ukubwa wa hekta 80, huku baadhi ya wakulima wakiwa kwenye makundi na wengine mmoja mmoja katika maeneo ya Handeni, Kisarawe, Tanga, Mpinga Rorya.” anasema.

Advertisement