Zijue mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi

Saturday March 30 2019

Uwekkaji wa mbolea ya mboji kama

Uwekkaji wa mbolea ya mboji kama hivi,kunasaidia uhifadi wa unyevu kwa muda mrefu.Ni mbinu muhimu katika mazingira yasiyo na mvua nyingi. 

Sekta ya kilimo inatajwa kuwa nguzo muhimu ya uchumi wetu. Sekta hii inajumuisha uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi na inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania; na huchangia takribani asilimia 95 ya mahitaji ya chakula kwa Taifa na nusu ya pato la Taifa.

Hata hivyo, kilimo hiki hutegemea hali ya hewa hasa mvua, hivyo huathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi. Athari hizo zinaonekana kwa mifumo tofauti katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo

Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, makala haya yanatoa mwongozo wa kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, huku ikiainisha mbinu na teknolojia mbalimbali za kuwaongoza wakulima, maofisa ugani na watunga sera katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ukwatuaji mdogo wa ardhi au kutokwatua kabisa

Mbinu hii inafanyika ikiwa na lengo la kutovuruga udongo au kuvuruga kwa kiasi kidogo wakati wa kukwatua/kulima eneo la shamba. Faida ya mbinu hii ni kupunguza gharama za uzalishaji, kuruhusu maji kupenya katika udongo, kuhifadhi unyevu katika udongo, kuhifadhi hewa ya ukaa katika udongo na kuzuia ongezeko la gesi joto angani.

Mbinu hii ya kilimo hufaa zaidi katika maeneo yote yenye uhaba wa maji/mvua au sehemu ambazo uwezo wa udongo wa kuhifadhi maji ni mdogo.

Advertisement

Kilimo cha mazao ya kufunika udongo

Mbinu hii hutumia mimea inayotambaa kufunika udongo kwa lengo la kuongeza naitrojeni, kuhifadhi unyevu katika udongo na kuzuia magugu. Mazao yanayolimwa ni yale yenye uwezo wa kutambaa na kufunika ardhi mfano mimea jamii ya mikunde, ambayo hupandwa kwenye shamba la mazao ya msimu au mazao ya muda mrefu.

Mbinu hii husaidia kurutubisha udongo na pia kupunguza athari ya matone ya mvua katika udongo ambayo huweza kusababisha mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.

Kilimo cha mazao mzunguko

Mbinu hii hutumika kwa kubadilisha mazao ya aina mbalimbali kwenye shamba moja katika misimu ya kilimo. Mbinu hii hupunguza matumizi ya mbolea za viwandani, hudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu, huhifadhi udongo na hivyo kuongeza uzalishaji.

Mbinu hii hufanywa kwa kujumuisha mimea jamii ya mikunde (katika mzunguko) ambayo ina uwezo wa kubadilisha hewa ya naitrojeni kuwa kirutubisho kinachoweza kutumika na mimea mingine. Njia hii hutumika pia katika kuhifadhi unyevu wa udongo hivyo kusababisha ongezeko la uzalishaji kwa mkulima.

Kilimo cha kutumia matandazo kufunika udongo

Mbinu hii ya kilimo hutumia matandazo yatokanayo na nyasi au matandazo maalumu kuzunguka mimea kwa lengo la kuhifadhi unyevu ardhini na kuzuia uotaji wa magugu. Matandazo haya yanaweza kutokana na majani, nyasi, mabaki ya mimea mingine au matandazo maalum ya nailoni.

Mbinu hii pia husaidia kuhifadhi unyevu, kurutubisha udongo na kusaidia mimea kupata virutubisho kwa urahisi kutoka kwenye udongo. Hivyo, mbinu hii humsaidia mkulima kuongeza uzalishaji, kupata kipato na kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Mbinu hii inaweza kutumika katika maeneo tofauti ya nchi hasa sehemu zenye uhaba wa maji au ambazo upatikanaji wa matandazo ni rahisi.

Kilimo Msitu

Mbinu hii huchanganya mazao ya kilimo na miti katika eneo moja ili kuleta faida za kijamii, kiuchumi na kimazingira. Kilimo hiki pia husaidia upatikanaji wa chakula, kufyonza hewa ukaa, kuboresha mzunguko wa virutubisho na kuhifadhi unyevu kwenye udongo, kupunguza kasi ya upepo na kuongeza kipato kwa mkulima kutokana na mazao ya kilimo na misitu endapo mkulima atafuga nyuki katika eneo husika.

Matumizi ya mabaki ya mazao

Mbinu hii hutumia mabaki ya mazao ambayo huachwa shambani baada ya kuvuna kwa lengo la kurejesha virutubisho kwenye ardhi na kuhifadhi unyevu kwenye udongo kwa kipindi cha muda kabla ya msimu mwingine kuanza.

Matumizi ya mbolea za asili

Mbolea za asili kama vile samadi na mboji huongeza uhifadhi wa hewa ukaa na unyevu katika udongo kwa muda mrefu, huboresha muundo wa udongo na kuongeza rutuba. Matumizi sahihi ya mbolea za asili huchangia katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kipato cha mkulima na kuhifadhi mazingira.

Makala haya kwa hisani ya Wizara ya Kilimo

Advertisement