MAKALA YA MALOTO: ATCL iangalie isimwangushe Magufuli kama ilivyofanya kwa Nyerere

Tanzania imenunua ndege saba ndani ya miaka mitatu. Hivi karibuni ilipokea Boeing 787-800 Dreamliner ya pili baada ya ile iliyotua Julai 8 2018. Kuna Airbus A220-300 mbili na Bombardier Q400 tatu.

Ni uhakika kuwa tangu Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, nchi haijawahi kufanya uwekezaji mkubwa kwenye usafiri wa anga kama sasa chini ya Rais John Magufuli.

Kipindi cha Mwinyi, Benjamin Mkapa mpaka Jakaya Kikwete, hakikuwa cha uthubutu mkubwa. Shirika la Ndege Tanzania (ATC kabla ya ATCL) lilifanya biashara kwa kusikilizia.

Kulikuwa na mahangaiko ya ndege za kukodi yaliyolifanya shirika hilo kusuasua miaka mingi, Mwaka 1994, ATC iliingia kwenye ushirika na Uganda Airlines na South African Airways, likaundwa Shirika la Alliance Air. Hasara ikawa juu ya hasara.

Zikawepo nyakati nyingine za kukodi ndege kisha kuingia ushirika na South African Airways, hasara ikaendelea. Mwaka 2002 ATC ilibinafsishwa kuwa ATCL, Serikali ilibaki na hisa asilimia 51, nyingine 49 ziliuzwa kwa South African Airways.

Biashara hiyo ikatajwa kugubikwa na hasara. Serikali ikavunja mkataba huo na ikapitia machungu ya kukodi ndege kwa mikataba iliyoinyonya nchi.

Mfano ni mkataba wa kukodi ndege ya Airbus A320 kutoka Kampuni ya Wallis Trading ya Lebanon.

Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh mwaka 2012 alipendekeza mameneja wa ATCL wachukuliwe hatua za kisheria kwa kutowajibika ipasavyo.

ATCL ilianzishwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nilipata kufanya mazungumzo na Samuel Sitta, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, kipindi cha kuvunjika kwa jumuiya.

Kwa mujibu wa Sitta, sasa marehemu, kama ambavyo maelezo yake niliyaandika kwenye kitabu changu cha “The Special One 2015; Nani Ajaye?”, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjwa Tanzania ilifanikiwa kuokoa ndege nne.

Na Tanzania haikuwa imejiandaa kuvunjika kwa jumuiya. Iliposhtuka, Mwalimu Julius Nyerere aliwaagiza wao, Sitta na aliyekuwa bosi wake, Ali Ameir (Waziri wa Uchukuzi) kushirikiana na jeshi kuhakikisha kila ndege ya Afrika Mashariki iliyokuwapo Tanzania haiondoki.

Maagizo mengine ni kuwa ndege yoyote ya Afrika Mashariki iliyokuwa kwenye anga ya Tanzania, ilazimishwe kutua kwenye uwanja wowote wa Tanzania. Jitihada hizo zilifanikisha kuokoa ndege nne.

Sitta alisema kuwa wazo lililofuata likawa kuanzisha ATC. Hata jina, Air Tanzania, lilitoka kwa Nyerere, aliyetaka popote ndege hizo zingekwenda, jina la Tanzania libaki na Tanzania ifahamike duniani.

Kwa mujibu wa Sitta, Nyerere aliona ndege nne zisingetosha kuendesha shirika, akataka ndege tatu zinunuliwe ziwe saba.

Sitta ndiye alitumwa na Mwalimu Nyerere kuongoza ujumbe wa wataalamu wa Wizara ya Uchukuzi, kwenda Canada kununua ndege hizo kwenye kampuni ya De Havilland Aircraft.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Canada, Pierre Trudeau, alipoona Tanzania inanunua ndege nchini kwake na kwa heshima ya Mwalimu Nyerere aliiongezea ndege mbili, zikawa tano.

Ndege hizo zilipowasili nchini, kwa kujumlisha zilizokuwapo, zilifanya Air Tanzania iwe na jumla ya ndege tisa. Haitoshi, Wizara ya Uchukuzi ilisomesha marubani wa kwanza wazalendo waliorusha ndege za ATCL.

Mwalimu Nyerere alianzisha ATCL ikiwa na ndege tisa. Zilikwenda wapi? Jawabu ni usimamizi. Walioaminiwa kuiongoza, ama kwa kutokuwa na maarifa au kukosa uzalendo, shirika lilianza kuchechemea hadi kufa.

Rais Magufuli ameikuta ATCL ikiwa na ndege moja, Bombardier Q300 iliyokuwa ikifanya safari zake kwa kusuasua. Aliingia na gia kubwa ya kununua ndege mpya mfululizo. Sasa zipo saba.

Kwa kurejea jinsi Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Air Tanzania kwa gia kubwa ya ndege tisa, unagundua kuwa mtihani uliopo sasa ni usimamizi.

Je, menejimenti ya sasa ya ATCL, itamtenda Magufuli kama wenzao walivyomwangusha Nyerere shirika? Muda ndio utaongea.