Asia, mwanasiasa kijana asiyeamini katika viti maalumu

Wednesday May 29 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

“Ukifuatilia kwa undani migogoro iliyo ndani ya vyama kati ya wanawake ni vita ya viti maalumu kuanzia kwenye ubunge hadi udiwani. Jambo hili linaturudisha nyuma mno wanawake kwenye uwanja wa siasa.”

Hivyo ndivyo anavyoanza kueleza Asia Msangi, aliyekuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema, wakati wa uchaguzi wa marudio uliofanyika Septemba 16, 2018.

Katika uchaguzi huo Msangi ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Jimbo la Ukonga alishindwa na Mwita Waitara wa CCM.

Katika mahojiano na gazeti hili, Msangi anaeleza masuala kadhaa, likiwamo la viti maalumu analosema linawarudisha nyuma wanawake na kuwaacha wanaume wakitesa majimboni.

Anasema licha ya mwamko mkubwa wa wanawake kujitosa kwenye siasa, ni wachache wenye uthubutu wa kusimama na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi.

Jambo hilo linasababisha idadi ndogo ya wanawake kuchaguliwa ikilinganishwa na wale wanaopitia viti maalumu na wanaoteuliwa kwa vigezo mbalimbali.

Advertisement

“Naumizwa sana na hili suala, kwamba baadhi ya wanawake kwenye vyama wamejiandaa kuwa wa viti maalumu. Yaani mtu anawaza kuwa mbunge lakini mlango wa kuingilia ni viti maalumu, si kusimama katika jimbo kupambana.

“Mawazo haya yamekuwa yakichangia migogoro mingi ya wanawake katika vyama, na ukifuatilia kwa karibu chanzo ni udiwani au ubunge wa viti maalumu,” anasema.

Anasema kuelekea 2020 wanawake wanapaswa kuachana na mtazamao huo na kujipanga kugombea majimboni kwa kuwa wanao uwezo na wakakubalika kwa wananchi.

“Kitu pekee ninachoweza kuwaambia wanawake wenzangu kwamba tuachane na mawazo ya viti maalumu, tunaweza kusimama kama wagombea kwenye udiwani na ubunge na wananchi wakatuamini. Mbona Esther Matiko ameweza kusimama kule Tarime na amepewa nafasi, tena kule kunatajwa kuwa na mfumo dume.

“Kama unajiona unataka nafasi fulani anza kujiandaa, jifunze kwa waliotangulia, pitia mafunzo ya uongozi zipo taasisi mbalimbali ambazo zinawajengea uwezo wanawake wanasiasa, tutumie njia hiyo kujijenga na si kusubiri viti maalumu na tusikubali kukatishwa tamaa,” alisema.

Katika kufanikisha hilo mwanasiasa huyo aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwaunga mkono wanawake wanaojitokeza kugombea ama ubunge au udiwani.

“Akioneka mwanamke amesimama viongozi wanapaswa kumpima uwezo wake na wakijiridhisha, kama anafaa wampe nafasi na kuzidi kumjenga ili awe kiongozi bora.”

Anawashauri wanawake wanaopata nafasi za kugombea kusimama imara na kupambana kwa uaminifu huku wakijiwekea dhamira ya kushinda.

Msangi pia anaitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia sheria ya uchaguzi ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Anasema sheria ikifuatwa hakuwezi kutokea vurugu na hata wananchi watakubali matokeo bila manung’uniko.

“Taratibu zikizingatiwa, mawakala wakaapishwa mapema na kupewa viapo vyao, wakaachwa wawe huru kwenye vituo kutimiza wajibu wao, sidhani kama kutakuwa na fujo lakini hii hujuma wanayofanyiwa mawakala wa upinzani inaleta doa,” anasema.

Anasema uamuzi wa mahakama kuzuia wakurugenzi kutumika kama wasimamizi wa uchaguzi ni hatua nzuri kuelekea 2020 huku akionyesha kushangazwa na nia iliyoonyeshwa na serikali ya kukata rufaa.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Msangi anasema ina mabadiliko makubwa ambayo yanawatisha walio nje na yanawarudisha nyuma wanasiasa wachanga au vijana wanaotamani kujitosa kwenye ulingo wa siasa.

“Shughuli za kisiasa zimekuwa ngumu kufanyika, yaani ule uhuru haupo kama ilivyokuwa zamani. Sasa kijana akiona namna ambavyo viongozi kila kukicha wanakamatwa na kufunguliwa kesi inawaweza kuwatia hofu na wasitamani kuingia kwenye siasa,”

Pamoja na hali hiyo Msangi anasema hatoacha kufanya siasa kwani amelelewa katika misingi ya kuishi kulingana na mazingira yoyote.

“Ndani ya Chadema tunapewa mafunzo yanayotukomaza kisiasa na miongozo inayotupa fursa ya kufanya siasa katika mazingira yoyote,” anasema.

Advertisement