Busara iliyotumika kwa Masele iwaone wengine

Wednesday May 29 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi

Mataifa mengi hivi sasa hasa katika nchi zinazoendelea, yapo katika mgongano wa kifikra baina ya makundi ya vijana na wazee, mambo ambayo yamekuwa yakileta tafakari na mivutano.

Lakini kuna usemi kila zama zina kitabu chake na huenda sasa, labda ni zimefika zama za vijana kutaka mawazo yao kuheshimiwa na kufanyiwa kazi hata kama yana mapungufu.

Lakini pia kila jambo lina faida na hasara zake. Inawezekana faida za jambo hilo, zikawa si za mtu binafsi bali kwa maslahi ya watu walio wengi ama taifa, hivyohivyo inawezekana kwa hasara ikawa kwa binafsi au Taifa.

Migogoro ambayo imekuwa ikiibuka bungeni, baina ya baadhi ya wabunge hasa vijana na kiti cha spika na kamati yake ya maadili, inaweza kupatia ufumbuzi kwa njia moja tu ya maridhiano na msamaha.

Jambo hili limedhihirisha katika mgogoro wa hivi karibuni baina ya Spika wa Bunge, Job Ndugai na Mbunge wa Shinyanga mjini, Stephen Masele ambaye pia ni makamu wa rais katika Bunge la Afrika (PAP).

Spika alitangaza kumrejesha nchini Masele ambaye alikuwa anaongoza vikao vya PAP, vilivyokuwa vinashughulikia kashifa ya unyanyasaji watumishi kijinsia ya Rais wa Bunge hilo, Roger Dang.

Advertisement

Mgogoro huu wa Rais wa PAP unamng’arisha Masele na Tanzania kwa ujumla kutokana na msimamo wake katika kupinga matendo ya unyanyasaji wa kijinsia lakini huku kwetu ulimtia matatani.

Masele mbunge kijana, alirudi nyumbani kwa wito wa Spika na kuhojiwa na Kamati ya Bunge inayoshughulika na maadili kwa tuhuma za kugombanisha mihimili ya nchi wakati akijaribu kujitetea kuhusu wito wa kurudi nyumbani.

Masele baada alirudi nchini na hatimaye alihojiwa na akatiwa hatiani kwa makosa manne kwanza kudharau mamlaka ya Bunge, kudhalilisha bunge, kuchonganisha viongozi na kusafiri bila kibali cha spika wa Bunge.

Kamati hiyo pia ikapendekeza Masele asimamishwe kuhudhuria mikutano mitatu baada ya kumtia hatiani.

Hata hivyo, baada ya kupewa fursa ya kujitetea Masele alieleza kilichotokea katika Bunge la PAP na jinsi alivyoamini kuwa alikuwa sahihi na aliomba radhi bunge na kiti cha spika kwa kilichotokea.

Hata hivyo, licha ya Masele kuibua malumbano mapya na Spika, Spika kwa busara aliomba Bunge kupuuza hoja za Masele akimweleza kama amekuwa na tabia za ajabu za ‘fitina, uchonganishi, ujanjaunja’ jambo ambalo si zuri na akaamua asamehewe.

Watanzania walio wengi wameridhishwa na maamuzi ya Ndugai kumsamehe Masele ingawa bado suala hili lina wingu zito.

Licha ya msamaha huo, hadi sasa haijulikani dhahiri ni nini chanzo cha mgongano huu baina ya Ndugai na Masele.

Itoshe kuheshimu busara za wabunge wetu na kiti cha spika kuamua kulimaliza jambo hili kwa maridhiano ili mambo mengine ya msingi yaendelee.

Tofauti na matukio ya wabunge wengine waliowahi kutiwa hatiani na kamati hiyohiyo, Masele aliomba radhi mapema kabisa, ingawa aliamua pia kuweka mambo mezani akitaka kumbukumbu za kikao cha kamati ziwekwe wazi.

Hata hivyo, naamini katika kurejesha maridhiano, upendo na mshikamano katika Bunge ni vyema pia wabunge wengine waliotiwa hatiani kwa makosa mbalimbali wapatie na msamaha kama wa Masele.

Inawezekana ikawa ni jambo ambalo linapaswa kufuata taratibu kadhaa za kibunge, lakini kwa busara ambazo zilionyeshwa na wawakilishi wetu bungeni bila kujali itikadi zao, ni vizuri msamaha ukawagusa na wengine ili warejee kufanya kazi walizopewa na waliowachagua.

Nimalizie kwa kulishauri Bunge letu, zile huruma ambazo zimetukika kumsamehe Masele pia zitumike kuwasamehe Profesa Mussa Asaad, Godbless Lema (Arusha Mjini) na mbunge wa Kawe Halima Mdee.

Mungu wabariki viongozi wetu waendelee kuamini katika maridhiano na kusameheana.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoa Arusha 0754296503

Advertisement