Chadema watwishwa zigo la ‘Ukawa’ uchaguzi 2020

Vyama vya upinzani nchini, viko njia panda kutekeleza mpango wa kushirikiana kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikitiwisshwa mzigo huo.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, vyama vinne vikiogozwa na Chadema vilishirikiana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Mbali na Chadema vyama vingine ni NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.

Ushirikiano huo ulijikita katika kusimamisha mgombea mmoja wa udiwani, ubunge na urais na ulitoa ushindani mkubwa kwa CCM hali iliyosababisha kupata madiwani na wabunge wengi na kuongezeka kwa kura za urais.

Idadi hiyo ya kura za rais na kuongezeka kwa wabunge na madiwani kulisababisha Ukawa kuongeza majiji mkuu kama ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha; Manispaa na Halmashauri zaidi ya 20.

Mgombea urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama shiriki vya Ukawa, Edward Lowassa alipata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39 huku Dk John Magufuli wa CCM akipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46.

Juzi akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally aliuponda Ukawa akisema ulianzishwa kwa ajili Katiba lakini akabadili mwelekeo kuwa ‘basi’ la kwenda Ikulu.

Dk. Bashiru alikuwa akizungumzia hoja ya madai ya tume huru ya uchaguzi, agenda iliyopata msukumo mpya kutoka vyama vya siasa, asasi za kiraia pamoja na wanaharakati.

Nafasi ya Chadema

Wakizungumzia uwezekano wa kuunda umoja huo kwa sasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanakitaja Chadema kama chama kinachopaswa kuongoza mchakato wasasa.

Kwa upande wake Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini kinasema kinathamini ushirikiano na tayari kimeunda kamati ndogo ya kamati kuu ambayo itakuwa na jukumu la kufanya mazungumzo na vyama vitakavyokuwa tayari kushirikiana kwenye uchaguzi huo.

“Suala la ushirikiano Chadema hata sisi tunalithamini sana na ndiyo maana mwenyekiti (Freeman Mbowe) alipoandika barua kwenda kwa rais (John Magufuli), nakala aliituma kwa vyama vyote na sasa vyama vionyeshe ushirikiano kwanza kudai tume huru ya uchaguzi,” alisema John Mrema ambaye ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema

“Hatua ya sasa, tushirikiane kudai tume huru ili tukipata tume huru ya uchaguzi tutajua hata tunapoingia kwenye uchaguzi tuna uhakika tutashinda,” alisema Mrema ambaye ni katibu wa kamati hiyo ndogo ya ushirikiano ndani ya Chadema.

Hoja ya Chadema inaungwa mko no na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe ambaye anasema kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24 mwaka jana kinawapa shaka kama kutakuwa na uchaguzi mkuu au la.

“Ushirikiano upo lakini uchaguzi wenyewe haueleweki kama utakuwa sawa au vipi maana miezi nayo inakwenda,” anasema Rungwe na kwamba anasubiri kile walichoomba Chadema kufanyika kwa maridhiano na majibu ya barua iliyotumwa Ikulu.

Rungwe aliongeza, “bila ushirikiano hakutakuwa na lolote na hatuwezi kushiriki katika uchaguzi, lakini hili ni baada ya kujua kama utakuwapo au utakuwa kama wa serikali za mitaa.”

Naye Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema wako tayari kushirikiana na vyama vingine makini vya upinzani na kwamba chama hicho kilipitisha uamuzi huo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tunawaunga mkono Chadema kudai tume huru ya uchaguzi na tuko nao pamoja kwani wao ni chama kikuu cha upinzani, lazima tukubali wana nafasi kubwa. Chadema wakiita vyama vingine kushirikiana hakuna atakayekataa. Kila chama kinaonyesha nia, lakini lazima awepo wa kuanzisha,” alisema Shaibu.

Umuhimu na fursa ya kushirikiana

Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda anasema hakuna chama cha upinzani kinachoweza kusimama peke yake na kudhani kinaweza kuishinda CCM.

“Somo kubwa la ushirikiano wa kisiasa tunalipata Kenya. Kipindi cha utawala wa Rais Moi (mstaafu Daniel Arap) alikuwa anapata ushindi chini ya asilimia 50. lakini alikuwa anashinda uchaguzi kwa sababu vyama vya upinzani vilikuwa vinagawana kura vyenyewe kwa vyenyewe.”

“Kama wanataka kuitikisa kweli CCM waungane na nadhani walijifunza kupitia Ukawa mwaka 2015, licha ya Ukawa wenyewe kujihujumu, walijipunguzia kura,” anasema Mbunda.

Kuhusu muda uliobaki kama unatosha, msomi huyo anasema “muda nauona unatosha kabisa, kwani huo ushirikiano upo kisheria. Kama mnataka kuungana kwa ajili ya uchaguzi mkuu mnapaswa kupeleka makubaliano yenu kabla ya miezi mitatu, kwa hiyo muda unatosha,”anasema.

Hata hivyo Mbunda anasema ushirikiano huo hauwezi kuwa wa vyama vyote vya upinzani bali vile vyenye wafuasi wengi.

“Saikolojia ya mpiga kura, wanataka kuona umakini, hawataki wapige kura ipotee bali washinde. Kwa hiyo licha ya sasa upepo kuonekana uko CCM, lakini wakishirikiana na kuonyesha kuna umakini, wananchi wanaweza kuwapigia kura,”anasema Mbunda.

Njiapanda ya ushirikiano

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alitaja mambo matano ambayo ni kiini cha mkwamo wa kuungana. “Kumekuwa na vurugu tangu 2015, hakuna utulivu wa fikra kwenye vyama na hiyo yote inasababisha kukosekana utulivu wa kisiasa na mambo mengi yanaharibika,” anasema Mbatia.

“Kama conflicts (migogoro) ziko ndani ya vyama, Chadema wenyewe hawaaminiani viongozi wao wanahama hama, atapata wapi muda wa kuzungumzia kuungana na mwingine?” alihoji Mbatia.

“CUF wenyewe kwa wenyewe hawaaminiani. ACT- Wazalendo tunaosema ni chama mbadala lakini wapo kwenye uchaguzi wa ndani halafu ndiyo wajipange tena kwa uchaguzi mkuu,” alisema.

“Tuko njia panda. Kuungana kwa upinzani kuwa na nguvu ya pamoja uchaguzi mkuu 2020 kwa uchambuzi nilioufanya kwa kweli niwe mkweli, tuko njia panda,” alisisitiza.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman alisema, “mpaka sasa hakuna chama kilichokuja kutaka kushirikiana na sisi, tunaendelea na maandalizi ya kuingia kwenye uchaguzi sisi wenyewe.”

Alipoulizwa kwamba haoni kuunganisha nguvu kuna tija kama ilivyokuwa 2015, Suleiman alisema “hakuna faida”.

“Mwaka 1995 na 2015 tumeshirikiana na tumepata viti vingi lakini umeona yaliyotokea. lazima tujue lengo halisi la kushirikiana na lipi,”anasema.

Lawama za vyama vidogo

Baadhi ya vyama visivyo na wabunge vimevitupia lawama vyama vikubwa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na ACT- Wazalendo kuwa viongozi wake hawaonyeshi dhamira ya kutaka muungano.

Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alisema: “katika mwaka ambao upinzani umechemsha ni mwaka huu. Nimebembeleza sana hii hoja ya kuungana nimekwama. Huu ni msiba kabisa”

Dovutwa alisema kwa wanayoendelea ndani ya vyama vya upinzani kushindwa kuungana ni kama vyama hivyo vinafanya mipango ya kukipa ushindi wa chee CCM.

Katibu mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alisema amejaribu kuwasiliana na viongozi wa vyama vikubwa na vyenye ushawishi vya upinzani ili wakutane lakini hapati ushirikiano.

“Mimi niseme ukweli na nisiwe mnafiki kwenye upande wetu wa vyama vya upinzani kuna tatizo la arrogance (kiburi) hasa kwa viongozi wakubwa kama Mbowe, Zitto na Mbatia,” alisema.

“Hivi ndio vyama tunavyoviegemea kwa sababu vina fursa ya kuwa na ushawishi. Vina wabunge na vina watu maarufu. Sasa kila mtu anajisikia. Hakuna chochote kinafanyika,” alisisitiza Muabhi.

“Kwa muda uliobaki kwenda 2020 tungekuwa tumeshafikia hata nusu ya maazimio. Lakini vyama vinaonekana ni wabinafsi. Vina uchu kwamba vyenyewe ndio vina nguvu,” alilalamika.

Kaimu Katibu Mwenezi wa UDP, Andrea Bomani, alisema baada ya azimio la Zanzibar la 2018 lililoongozwa na Zitto, aliamini mambo yangekuwa ni moto moto lakini imekuwa tofauti.

“Kwenye lile azimio walionyesha wangekuja na mipango dhabiti ya kuungana. Ninavyoona hakuna mwelekeo wa jambo hili zito. Mimi nimeshauri kwa maandishi lakini kuna kusitasita,” alisema.

“Ni kama vile upinzani umechanganyikiwa hawajui washike lipi na siku zimeshaisha labda ni kwa sababu ya hii hamahama ya viongozi. Pengine imewaondoa kwenye msitari,”alisema Bomani.

Azimio la Zanzibar

Desemba 2018, vyama sita vya upinzani, CUF, NCCR-Mageuzi, NLD, Chauma, Chadema na ACT-Wazalendo, vilikutana visiwani Zanzibar na kutangaza azimio la kushirikiana.

Katika azimio hilo, viongozi wa vyama hivyo walitangaza kuunda kamati ya kuratibu ushrikiano huo.

Azimio hilo lilitiwa saini Maalim Seif wakati huo akiwa Katibu Mkuu CUF, Mbatia, Oscar Makaidi wa NLD, Salum Mwalim (Chadema Zanzibar) na Hashim Rushwe wa Chauma.

Azimio hilo liliweka mkakati wa kuyaunganisha makundi yote na wanasiasa wa upinzani na kuwa na mkakati wa pamoja wa kupigania haki. “Tunautangaza mwaka 2019 kuwa ni mwaka wa kudai demokrasia ambao tutapambana kuzidai haki zetu zote tunazonyimwa kinyume na sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.

“Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na vyenye utaratibu uliowekwa rasmi kisheria na kikatiba, tutatangaza rasmi namna na utaratibu wa kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona.”