Diwani aliyedumu katika nafasi yake kwa miaka 55 huyu hapa

Fihiri Mvungi ni diwani wa Msangeni (CCM) wilayani Mwanga

Fihiri Mvungi anatimiza miaka 80 Desemba mwaka huu na kiwango hicho cha umri kina mengi ndani yake, kubwa likiwa ni kushikilia kw amuda mrefu nafasi yakuteuliwa.

Fihiri amekuwa diwani wa Msangeni (CCM) wilayani Mwanga kwa miaka 55, huku akishika nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri kwa miaka 40.

Lakini hiyo haijatosha; anataka zaidi na Oktoba ataomba ridhaa ya wananchi pamoja na kukaribia kutimiza karne.

“Bado nina nguvu. Endapo wananchi wataridhia kunituma tena, nipo tayari kuwatumikia kwa uaminifu,” alisema Mvungi katika mahojiano maalum na Mwananchi.

“Mimi kugombea au kutogombea inategemeana na wananchi. Wao ndio walinituma na bado nina nguvu. Wakiamua kunituma tena nitakwenda kuwatumikia lakini wakisema nipumzike sawa tu.

“Siwezi kuwakatalia watu, kuwakatalia ni jambo baya. Wakikuhitaji nao ukawakatalia, wakipata shida watasema kama si fulani tusingefikia hapa. Hivyo ni bora wao wanikatae.”

Mvungi, ambaye ni fundi nguo, kazi inayofahamika zaidi kama fundi charahani, alishinda nafasi ya udiwani kwa mara ya kwanza mwaka 1965 akiwa na umri wa miaka 25, wakati huo Wilaya ya Same na Mwanga zilikuwa hazijagawanywa.

Anasema kabla ya kuwa diwani, alishika wadhifa wa mwenyekiti wa Kijiji mwaka 1962 nafasi aliyodumu hadi alipochaguliwa kuwa diwani katika uchaguzi wa mwaka 1965.

Anasema mwaka 1979 Wilaya ya Pare iligawanywa na kupatikana Wilaya ya Mwanga na Same, mwaka 1980 akachaguliwa kuendelea na udiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.

Anasema mwaka 1980 baada ya kuchaguliwa kuwa Diwani wa Halmashauri ya Mwanga alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Halmashauri, nafasi aliyodumu nayo hadi sasa.

Wilaya ya Pare imefilisika

Anasema kabla ya mwaka 1965, ilitangazwa msikitini wanaotaka udiwani wajitokeza, wananchi wengi walimshawishi ajitokeze kugombea nafasi hiyo.

Fihiri anasema awali mwaka 1964 kulijitokeza jambo kubwa la kisiasa baada ya aliyeshinda udiwani kujiuzulu kutokana na aliyekuwa mkuu wa mkoa, Peter Kisumo kutangaza Wilaya ya Pare kuwa imefilisika.

“Baada ya tangazo hilo, aliyekuwa diwani alisema hawezi kukaa mahali ambapo pamefilisika, hivyo mwaka 1965 nafasi hiyo ilipotangazwa, nilijikuta nimejitokeza peke yangu,” anasema.

“Baada ya watu kuona uongozi utakuwa mgumu kwa kuwa wilaya imeshatangazwa imefilisika, huo ndio ukawa mwanya kwangu wa kupita katika nafasi hiyo. Nikakubali tena ombi la kuwa Diwani.

“Kukubali kuwa diwani wakati wilaya imefilisika kulinifanya niendelee kukubalika hadi sasa. Kila kunapotokea uchaguzi, akijitokeza mtu anayenizidi umri, nilikuwa namuuliza swali, kwa nini anagombea sasa. kwa nini hakujitokeza kuomba nafasi hiyo wakati ule wilaya imefilisika. Hili swali huwarudisha nyuma na kunifanya niendelee kushinda.”

Nini siri ya mafanikio

Kudumu katika nafasi ya kuchaguliwa kwa muda mrefu kuna siri yake, na Mvungi anaweka bayana kuwa ni “utumishi bora kwa wananchi na kujituma kuwatumikia”.

“Kazi hii ni mzigo ambao nimeubeba na ni lazima niubebe ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, lakini pia nimekuwa na ushirikiano nao mkubwa,” anasema.

“Wanachokiagiza ninakishughulikia na nikikwama wanajua kwa sababu nitarudi kwao kuwaambia. Ninawathamini wananchi wangu, na wao pia wananithamini. Mimi ni mwajiriwa wao.”

Anasema amekuwa akishirikiana na wananchi kuhakikisha anatatua changamoto zinazowakabili na kuwaletea maendeleo kama kuwezesha kuboreshwa kwa barabara, elimu na afya katika kipindi chake.

“Katika kata yangu, kuna vijiji vitano, vitongoji 19, lakini shule za msingi zipo saba, sekondari tatu na zahanati ziko nne,” alisema.

“Sasa hivi tupo katika mchakato wa kuiboresha zahanati ya Kikweni. Lengo ni kuifanya ipandishwe hadhi kuwa kituo cha Afya. Hii itatufanya tuwe na vifaa tiba na wataalamu wengi zaidi na mwisho wa siku ninachokitaka ni wananchi wapate huduma bora.”

Anasema wameweza kuboresha barabara na sasa zinapitika wakati wote, na kero kubwa iliyobaki ni upatikanaji wa maji, akisema baadhi ya wananchi hawapati maji kwa saa 24.

Shida ni kupinga kila kitu

Akizungumzia tofauti iliyopo katika mfumo wa vyama vingi na wakati wa chama kimoja, Mvungi anasema si vibaya kuwa na vyama vingi kwa kuwa vinaweka changamoto kwenye utendaji.

Bali anasema shida anayoina katika vyama vya upinzani nchini ni kwa wao kutaka kupinga kila kitu, hata pale yanapofanyika mambo mazuri ambayo yalihitaji kusifiwa.

“Si vibaya kukawepo na vyama vya upinzani, ni jambo nzuri. Lakini tatizo ni kwamba wanapinga kila kitu, hata yakifanyika mazuri, ingawa kwa hapa kwetu Mwanga hakuna shida hiyo,” alisema.

Hata hivyo alipozungumzia tofauti ya utendaji kwa awamu zote nne zilizopita, anasema kila kiongozi mkuu wa nchi anapoingia anakuja na utaratibu wake.

“Nimekuwapo awamu zote tano kama diwani, sijaona tofauti kubwa katika utendaji. Lakini kikubwa ni kwamba kila anapoingia kiongozi wa juu, anakuja na mipango na taratibu zake,” alisema.

Mvungi anaeleza kuwa ameitumikia nchi kupitia wananchi kwa zaidi ya miaka 50, hivyo angetamani kupongezwa na kutambulika kwa kupewa heshima ya kupewa hata cheti.

Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini apongezwe wakati nafasi hiyo amekuwa akiiomba mwenyewe, Mvungi alisema ni kweli amekuwa akiiomba mwenyewe, lakini ni vyema akapongezwa.

“Kupongezwa si lazima nipewe fedha, nipewe tu heshima na kutambulika kama miongoni mwa watu waliotumikia taifa kwa muda mrefu na kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.”