Dk Bashiru anapolalamika, wengine wamlilie nani?

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.

Muktasari:

Katika kitabu hicho, Covey ameweka duara lenye safu tatu ambalo linaitwa Circle of Influence. Safu ya juu ni uhusika (circle of concern). Je, unaguswa vipi na jambo? Ukiguswa maana yake utaangalia nafasi yako ya ushawishi wa jambo lenyewe, hapo ndiyo unaingia safu ya pili ya duara, yaani circle of influence.

Maneno yenye kujenga fikra yanaweza kutoka kwa yeyote ilimradi awe ametumia vizuri kiwango chake cha kufikiri. Si mpaka yatoke kwa wanafalsafa wakubwa wenye kutambulika.

Mwanamitindo wa Uswisi ambaye shughuli zake huzifanyia Brooklyn, New York, Marekani, Tina Eisenberg katika andiko lake la kanuni za Maisha, moja ya hizo kanuni anasema “Usiwe mlalamikaji. Yafanye mambo kuwa bora.”

Anafafanua kwamba kama mtu hana uwezo wa kufanya jambo ili kubadili hali iliyopo, vema akaacha kulalamika, maana malalamiko hayasaidii.

Mwandishi maarufu India, Tanmay Vora ana andiko lake kuhusu duara la ushawishi. Anasema kila binadamu ana duara lake la ushawishi. Anashauri kuwa kabla mtu hajalalamika, vema ajitazame yeye amefanya nini kushawishi pale anapofikia.

Tanmay anasema kabla ya kulalamika, mtu anapaswa kujiuliza maswali haya; Naweza kutatua mwenyewe? Utatuzi upo ndani ya uwezo wangu? Kama siyo, je, naweza kumshawishi mtu ambaye anaweza kutatua?

Kwa kuweka sawa, Circle of Influence imefafanuliwa vizuri kwenye kitabu cha “The 7 Habits of Highly Effective People”, yaani Tabia Saba za Watu Wenye Ufanisi wa Juu. Kitabu kimeandikwa na aliyekuwa mwelimishaji na mfanyabiashara wa Marekani, Stephen Covey.

Katika kitabu hicho, Covey ameweka duara lenye safu tatu ambalo linaitwa Circle of Influence. Safu ya juu ni uhusika (circle of concern). Je, unaguswa vipi na jambo? Ukiguswa maana yake utaangalia nafasi yako ya ushawishi wa jambo lenyewe, hapo ndiyo unaingia safu ya pili ya duara, yaani circle of influence.

Safu ya tatu ya duara ni mamlaka ya jambo husika (circle of control). Je, ipo ndani ya uwezo wako? Kama jibu ni ndiyo basi unajishawishi mwenyewe kushughulikia. Ikiwa ni nje ya uwezo wako, basi mshawishi mwenye mamlaka.

Circle of influence inaelekeza watu kutokuwa walalamikaji, kwa maana wanaotegea wengine wafanye ili wao watoe maoni (reactive). Inafundisha watu kuwa watatuzi na waanzisha mwendo (proactive).

Nafasi ya Dk Bashiru

Dk Bashiru Ally ni katibu mkuu wa CCM. Ndiye mtendaji mkuu na mwenyekiti wa sekretariet ya chama hicho. Kwa asili ya muundo wa chama hicho, uhai wa CCM kwa kipindi hiki upo mikononi mwake. Zaidi, CCM ni chama kinachoongoza Dola.

Kitabia, CCM wamejiwekea utaratibu kwamba wanapoongoza dola, Rais ndiye anakuwa mwenyekiti wa chama. Kutokana na hali hiyo, mzigo wote wa uhai wa chama upo kwa katibu mkuu. Ni kwa sababu hiyo mwenyekiti si mjumbe wa timu ya utendaji wa kila siku wa chama, yaani sekretarieti.

Kwa maana hiyo, Dk Bashiru kwa sasa ndiye oksijeni ya CCM. Wajibu wake mkubwa ni kuhakikisha chama kinapumua hewa safi. Ukirejea falsafa ya duara la ushawishi (Circle of Influence), ndani ya CCM Dk Bashiru anao uhusika kamili, ana ushawishi na anayo mamlaka.

Kama kuna mtu ambaye hatakiwi kulalamika kabisa kuhusu CCM na jumuiya zake, huyo ni Dk Bashiru. Maana anahusika moja kwa moja, nguvu yake ya ushawishi ni kubwa na mamlaka aliyonayo ni ya kiwango cha juu. Akilalamika yeye wengine wawe na hali gani?

Mara kadhaa Dk Bashiru amekuwa akisikika akilalamika kuhusu viongozi vijana, kwamba wanafanya makosa mengi kwa sababu ni matunda ya vijana kutopikwa kiuongozi. Alianza kuwasema Nape Nnauye, mbunge wa Mtama CCM na Hussein Bashe, mbunge wa Nzega Mjini CCM.

Na karibu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipotoa kauli zenye viashiria vya ubaguzi wakati wa msiba wa mfanyabiashara Reginald Mengi, Bashiru alimuombea msamaha na kusisitiza kuwa ni matunda ya kutowaandaa vijana kuwa viongozi.

Bashiru analalamika kuwa vijana hawajaandaliwa kuwa viongozi. Anakiri kuwa kazi ilifanyika huko nyuma lakini ikaachwa. Ndani ya CCM kuna Umoja wa Vijana (UVCCM). Wajibu wa msingi wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwapika vijana kuwa viongozi wazuri na wazalendo kwa nchi yao.

Hivyo, badala ya Bashiru kulalamika kuwa vijana hawajaandaliwa, anatakiwa kuonesha nini ambacho ameanza kukishughulikia ili kuirejesha UVCCM kwenye misingi yake ya kuwapika vijana kuwa viongozi wazuri. Anapolalamika anakuwa anajiweka kama mtoa maoni baada ya matokeo, badala ya kuanzisha mchakato wa kuleta matokeo (proactive).

Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa alisema mfumo wa kuwaandaa vijana kiuongozi CCM ulikufa baada ya kuanzishwa vyama vingi. Alisema wakati wa chama kimoja fedha za kuwapika vijana vyuoni kuwa viongozi bora zilitoka serikalini.

Katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alisema kuwa wajibu wa kuandaa vijana kiuongozi linaanzia ndani ya familia. Kwamba wazazi lazima watimize majukumu yao ya malezi kwa watoto wao.

Msekwa amesema tatizo ni fedha. Makamba ametaja wajibu wa wazazi. Yote ni sawa. Bashiru anatakiwa achukue yote. Kuhusu fedha, CCM kweli inashindwa kuandaa vijana kuwa viongozi kwa sababu ya fedha? CCM inakosa mbinu za kufikia wazazi ili kushawishi malezi bora kwa viongozi wa kesho?

Mwisho, je, UVCCM imekuwa jumuiya ya mapambo? Malengo ya kupika vijana kiuongozi yamepotea. Nape, Bashe na Makonda wote ni zao la UVCCM. Kama Bashiru kwa nafasi aliyonayo analalamika badala ya kushawishi na kutumia mamlaka yake, wananchi wa kawaida wamlilie nani?