Dk Bashiru huwa anapata nafasi ya kujisikiliza yeye mwenyewe?

Muktasari:

Dk Bashiru Ally ni mzaliwa wa Mkoa wa Kagera, Kaskazini magharibi mwa Tanzania.Alikuwa mhadhiri katika Idara ya Say-ansi ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.Dk Bashiru pia ni mkufunzi wa masuala yanayohusu utawala na sheria za ardhi .

Ni mtafiti na mwandishi wa makala mbalimbali zilizochapishwa kwenye matoleo ya machapisho mbalimbali. Amekuwa akijihusisha katika shu-ghuli zilizoratibiwa na taasisi kwa muda mrefu.Kiitikadi amejipambanua kama mja-maa na mfuasi wa sera za Mwalimu Julius Nyerere.

Hapo kabla hakujiweka wazi kama ni mwanachama wa CCM mpaka pale ali-poteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati maalumu iliyopewa jukumu la uhakiki wa mali za Chama cha Mapinduzi.Dk Bashiru alichukua nafasi ya Abdul-rahman Kinana aliyeamua kustaafu ukatibu mkuu wa CCM.


Alithibitishwa kushika wadhifa wa katibu mkuu kwenye mkutano wa Hal-mashauri Kuu ya CCM (Nec) iliyoketi jijini Dar es Salaam Mei 28-29, 2018

Uwasilishaji ni fasihi. Mambo makuu mawili katika fasihi hasa kwa fanani ni kumbukumbu na marejeo ya uwasilishaji wa nyuma. Vinginevyo mtu mmoja anaweza kutengeneza fanani wengi katika mada moja.

Mada ni kwa nini nchi haipigi hatua kimaendeleo? Leo fanani amesimama na kueleza kwa umahiri kuwa tatizo la nchi kutopiga hatua ni sera mbovu ya Serikali ambayo haiwezeshi msisimko wa kiuchumi kuanzia vijijini, ndio maana nguvu kazi kubwa inakimbilia mijini.

Fanani huyohuyo jana alisema sababu ya nchi kutoendelea ni wananchi kuwa wavivu na kutoitikia mipango na sera ya Serikali ya kujenga uchumi kuanzia vijijini. Jana aliwabebesha lawama wananchi, leo anaishutumu Serikali.

Juzi fanani alitia fora aliposema nchi haiwezi kuendelea kwa sababu mungu amekasirika. Kwamba jitihada nyingi za Serikali, kimipango, sera na utekelezaji pamoja na uitikio mzuri wa wananchi na kujituma kwao, si lolote kwani mungu amenuna.

Kwa uwasilishaji wa fanani juzi ni kuwa Serikali ina mipango, sera na utekelezaji mzuri, vilevile wananchi wanaitikia vema na wanajituma sana, lakini mungu amekasirika. Jana alilaumu uvivu wa wananchi, leo anashutumu sera ya Serikali.

Kwa mujibu wa fanani, juzi Serikali ilikuwa vizuri kisera, kimipango na utekelezaji. Juzi pia wananchi walikuwa safi kabisa. Wanajituma, sio wavivu. Jana wananchi waligeuka kuwa wavivu lakini Serikali haina tatizo. Leo Serikali ndio shida kuu na wananchi hawana lawama.

Fanani wa aina hiyo lazima tumkumbushe maneno yake ya juzi na jana, ajisikilize mwenyewe. Kisha tumuulize juzi alipokuwa anaitetea Serikali na wananchi alikuwa anatumia chumba kipi cha fahamu? Jana je? Leo vipi?

Inashauriwa kabla ya kuanza kuhutubia utulize kichwa na kukumbuka hotuba za nyuma ulisema nini katika jambo ambalo unaliendea. Ni muhimu sana, vinginevyo mtu mmoja anaweza kuzalisha fanani 10 katika mada moja.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, inabidi naye akumbushwe kujisikiliza katika hotuba zake za nyuma. Kwani amekuwa akitengeneza fanani wengi ndani ya mada kuhusu uchaguzi.

Dk Bashiru, hivi karibuni alitamba kuwa mwakani CCM itapata ushindi wa asilimia 99.9 kwa sababu kimeshawasha taa kupitia ushindi wa Serikali za Mitaa ambao CCM ilivuna asilimia 99.7. Akasema CCM kwa sasa masafa yake ni 99.7, mwakani yatakuwa 99.9.

Ukisikiliza hotuba ya Dk Bashiru humuoni akisikitikia kujitoa kwa wapinzani kwenye uchaguzi, wala kushitushwa na idadi ndogo ya wananchi waliojitokeza kupiga kura, anachojivunia ni ushindi wa asilimia 99.7. Na anatamba kuwa mwakani ushindi utakuwa mnono zaidi.

Kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dk Bashiru alikuwa mwanaharakati mzuri wa uchaguzi. Hotuba zake zipo kwenye rekodi na zinazunguka mitandaoni, akikiri kuwa watu hawajitokezi kupiga kura. CCM hushinda kwa wastani wa wapigakura asilimia 30 ambao hujitokeza.

Kwa mujibu wa Dk Bashiru, wananchi kwa wastani wa asilimia 70, hubaki nyumbani au kuendelea na shughuli nyingine badala ya kujitokeza kwenye vituo vya kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaowapenda.

Dk Bashiru alisema kuwa wananchi wengi huona uchaguzi ni kituko au mchezo wa kuigiza, ndio maana huamua kutojitokeza kupiga kura. Huyo ndiye Dk Bashiru wa jana. Aliyesikitikia uitikio mdogo wa wapigakura. Aliyeumia chama chake kuchaguliwa na watu asilimia 30, akisema hawakidhi uhalali wa kuongoza.

Dk Bashiru wa leo haumizwi CCM kuchaguliwa katika uchaguzi uliodorora. Wapinzani kujitoa na vituo vya kupigia kura kuwa vyeupe kwa sababu ya uitikio mdogo. Anashangilia ushindi wa asilimia 99.7.

Leo Dk Bashiru hasemi ushindi wa asilimia 99.7 CCM imeupata kutoka kwa wapigakura asilimia ngapi. Anachosisitiza ni kwamba mwakani watashinda zaidi. Ndio maana kuna haja ya kumuuliza Dk Bashiru kama hujisikiliza yeye mwenyewe.

Kipindi alipokuwa akisema nchi imekuwa na uchaguzi wa maigizo na kituko, wengi walimuona ni taa inayowaka vizuri. Na kwa vile yeye ni Katibu Mkuu wa chama kinachoongoza dola, alitarajiwa achochee mabadiliko ili wananchi wasione uchaguzi ni kituko.

Wananchi waliomsikiliza jana, leo bila shaka wanastaajabu. Kwani uchaguzi wa Serikali za Mitaa uligomewa na wananchi tangu kujiandikisha. Kelele za kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha zilikuwa nyingi. Yakatolewa matangazo na vitisho vya kufuata watu baa, mitaani na kubana watumishi wa umma ili kubaini ambao hawakuwa wamejiandikisha.

Hamasa ya kujiandikisha ilitolewa pia na viongozi wa vyama vya upinzani. Hivyo, kuna idadi ya wapigakura waliojiandikisha kwa sababu ya wito wa vyama vya upinzani. Kuelekea uchaguzi, vyama vyote vya upinzani vyenye uwakilishi bungeni na vingine kadhaa, vilijitoa kwenye uchaguzi.

Kwa mazingira hayo hutakosea ukisema kuwa katika idadi iliyojiandikisha kwa taabu, wengine wengi hawakujitokeza siku ya kupiga kura kwa sababu walijiandikisha kwa wito wa vyama vya upinzani ambavyo vilijitoa.

Wapo ambao si kwa sababu ya upinzani, bali walijionea kuwa mazingira ya uchaguzi yalishavurugika, sasa wajitokeze ili kufanya nini? Vituo vingi vikawa vyeupe, na ikumbukwe kwamba maeneo mengi wagombea wa CCM walipita bila kupingwa.

Kwa Dk Bashiru ambaye alikuwa akiumizwa na uchaguzi ambao wapigakura wanaojitokeza ni wachache, angetarajiwa kuumia zaidi kutokana na mazingira ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini imekuwa kinyume chake. Anashangilia ushindi na anaahidi ushindi mkubwa zaidi mwakani.

Nini kimembadilisha Dk Bashiru? Kwa nini jana aliumizwa CCM kushinda katika uchaguzi wenye wapigakura asilimia 30 kwamba ni kidogo na hawatimizi uhalali wa kuongoza, halafu leo anashangilia ushindi usio na washindani wala wapigakura?