Hizi ndiyo sababu za watu kususia uchaguzi duniani

Tanzania itafanya uchaguzi wake wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijijini Jumapili Novemba 24,2019, huku vyama vya upinzani saba vikitangaza kutoshiriki uchaguzi huo.

Lakini ni vyema tukatafuta sababu zinazosababisha vyama kujitoa, ukiacha zile zilizotolewa na vyama vyenyewe kikiwamo Chadema ambacho kinaonekana ndicho chama kikuu cha upinzani.

Vyama hivyo vimejitoa kutokana na kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ambapo wagombea wao karibu asilimia 90 nchi nzima walienguliwa kwa madai ya kukosa sifa.

Sifa hizi ni pamoja na kutokujua kusoma na kuandika, kukosea tarehe ya kuzaliwa, kukosea jina la chama na katika maeneo mengine hata wasimamizi wasaidizi hawakueleza sababu za kuwaengua.

Suala hili la wagombea wa upinzani pekee kukosa sifa linafikirisha sana, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya walioenguliwa wamemaliza sekondari wengine ni wasomi wa vyuo vya elimu ya juu.

Pamoja na sababu hizo, wanazuoni mbalimbali wanataja sababu kubwa nne zinazofanya wapiga kura kususia uchaguzi na moja ni pale wanapohisi kutakuwa na udanganyifu katika uchaguzi husika.

Sababu nyingine ni pale wanapoona mfumo mzima wa uchaguzi unapendelea wagombea fulani na tatu ni chombo kinauchoandaa kukosa uhalali.

Ipo sababu nyingine ya nne ambayo ni pale kama wagombea hawana umaarufu au hawajulikani, lakini sababu hii haiingii katika hatua tuliyokuwa tumefikia katika mchakato wa uchaguzi tulionao.

Dalili za watu kususia uchaguzi huu zilionekana zoezi la uandikishaji wapiga kura, ambapo Serikali ililazimika kutumia nguvu kubwa kuhamasisha watu kujiandikisha wakiwamo watumishi wa umma.

Hii haikuwa dalili njema, kwa sababu Serikali ililazimika kuongeza siku za watu kujiandikisha, kisha ikaja na takwimu kuwa watu milioni 19.6 walikuwa wamejiandikisha.

Lakini kujiandikisha ni jambo moja, na kujitokeza kupiga kura ni jambo jinmgine, hasa katika mazingira tuliyonayo ambapo karibu asilimia 90 ya wagombea wa upinzani wameenguliwa.

Wala tusidanganyane, yale yaliyotokea hadi wagombea hao kuenguliwa ni dhahiri yametuletea mpasuko na chuki kama taifa na wala CCM hakipaswi kuchekelea hadi jino la mwisho kuonekana.

Tumeona wakati wa uandikishaji namna watumishi wa umma katika baadhi ya maeneo wakilazimishwa kujiandikisha, lakini swali ni je, watalazimishwa tena kwenda kupiga kura?

Wanazuoni wanasema pale ambapo watu wanalazimishwa kwenda kupiga kura, ususiaji unaweza kwenda mbali na kuleta vitendo vya raia kutoheshimu sheria au kupiga kura za giza au maruhani.

Hali hii ambayo kumekuwa na kilio kikubwa cha kukiukwa kwa taratibu na kanuni za uchaguzi, iliwahi kuzikumba nchi mbalimbali duniani ambapo sehemu kubwa ya wapiga kura walisusa.

Mathalan, katika uchaguzi mkuu wa Jamaica mwaka 1983, ni asilimia 2.7 tu ya wapiga kura walijitokeza kupiga kura na Bangladesh mwaka 1996 asilimia 21 tu walijitokeza kupiga kura.

Pia Venezuela mwaka 2005 katika uchaguzi wa wabunge ilishuhudiwa asilimia 25.3 tu ya wapiga kura wakijitokeza na Ghana hali ikawa hivyo 1992 ambapo waliojitokeza ni asilimia 28.1

Dalili mbaya za wapiga kura kutojitokeza tumezishuhudia katika chaguzi ndogo za ubunge na madiwani ambapo waliojitokeza walikuwa kati ya asilimia 30 na 40.

Sitaki kutabiri siku ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 24 utakuwaje, ni vema tukasubiri na kuona.

Njia pekee ya kunusuru hilo na pengine mengine yanayoweza kulikumba taifa letu, ni kwa Serikali na chama cha mapinduzi kukaa meza moja ya maridhiano na vyama vya siasa vya upinzani.