Inaonekana Nyerere alikufa akiumia kwa Dk Salim kutokuwa Rais

Katika kitabu cha “My Life My Purpose” ambacho Rais wa tatu, Benjamin Mkapa ameandika kuhusu mapito ya maisha yake, amesimulia alivyopata wazo la kugombea urais mwaka 1995, kuwa alijiona ana uwezo kuliko waliotajwa na waliojitangaza.

Mkapa anasema alikwenda kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, bila shaka kuomba baraka zake, akamweleza nia yake ya kuingia kwenye kinyang’anyiro. Mwalimu alimjibu: “Kachukue fomu, kuna mtu nilikuwa namfikiria lakini bado anasitasita.”

Septemba 20, mwaka jana, Rais wa nne, Jakaya Kikwete, alipokuwa kwenye kongamano la mapitio ya kitabu chake kinachoitwa “The Story of My Life; From Barefoot Schoolboy to President”, naye alisimulia safari yake ya kugombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995 kuwa hakuwa na wazo kabisa.

Kikwete alisema aliitwa na Mwalimu Nyerere wakafanya kikao. Mwalimu Nyerere alimuomba Kikwete waunde timu ya kumshawishi “mtu” awe mgombea urais. Kikwete alikutana na huyo mtu Nairobi, Kenya.

Majibu kutoka Kenya hayakuwa mazuri kwa Mwalimu Nyerere, kwamba aliyefuatwa kushawishiwa na Kikwete, alisita kuacha kazi aliyokuwa anaifanya ili ajitose kuwania urais.

Ndipo ushawishi wa kumtaka Kikwete achukue fomu ya kugombea urais ulipoanza.

Ni Salim Ahmed Salim

Mwalimu Nyerere alimtaka Salim Ahmed Salim awe Rais wa Tanzania tangu mwaka 1985. Wakati huo, kwa mujibu wa wazee wa CCM, kilichosababisha vikao vya chama viamue mgombea awe Ali Hassan Mwinyi, rais wa pili, badala ya Salim, ni itifaki.

Ni kwamba majina matatu yaliingizwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais ambaye angemrithi Mwalimu Nyerere aliyekuwa anang’atuka – Mwinyi, Salim na Rashid Kawawa.

Mwinyi alikuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Salim kwa wakati huo alikuwa Waziri Mkuu, Kawawa alikuwa Katibu Mkuu CCM, lakini alishakuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais.

Mchuano ulikuwa kati ya Mwinyi na Salim. Vikao vikaona kiitifaki Mwinyi alikuwa na cheo kikubwa kuliko Salim. Na kwa sababu hiyo, ingekuwa si heshima kumpitisha Waziri Mkuu na kumwacha Makamu wa Rais.

Hivyo, kiu ya Mwalimu Nyerere kumfanya Salim awe mrithi wake mwaka 1985, ilidhibitiwa na hekima ya kiitifaki iliyoibuliwa ndani ya vikao vya CCM.

Kisha tena, mwaka 1995, bila shaka Mwalimu Nyerere aliona hoja ya kiitifaki isingekuwa na nguvu, akamuita Kikwete akamtuma kwa lugha ya kuunda timu ya ushawishi, akamwambie Salim arejee chini aingie kwenye kinyang’anyiro.

Salim wakati huo alikuwa katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU ambayo sasa ni AU, ofisi yake ilikuwa Ethiopia. Kikwete baada ya kuwasiliana na Salim, walikutana Nairobi.

Inaelezwa kuwa Salim hakukataa wito wa Mwalimu, ila alitaka apewe uhakika. Kwamba si aache kazi OAU, halafu arejee nchini kisha yatokee kama ya mwaka 1985. Huku ndiko “kusita” ambako Mwalimu alimwambia Mkapa.

Kikwete anasimulia kuwa aliitwa na Mwinyi (akiwa Rais), akamwambia wamemjadili na Mwalimu Nyerere na walikubaliana wamwambie achukue fomu.

Maana yake ni kuwa Mwalimu Nyerere alimpa baraka Mkapa achukue fomu baada ya Salim kusita, pia alimtaka Kikwete kuingia kwenye mchuano, sababu alipomtuma kumshawishi Salim, hakupata majibu mazuri.

Kutaka uhakika wa nafasi, lilikuwa shambulio la demokrasia. Wanaochagua ni wajumbe wa vikao. Nguvu ya Mwalimu ni ushawishi na si uamuzi. Ndio sababu mwaka 1985, wajumbe waliamua awe Mwinyi na si Salim ambaye Mwalimu alimtaka.

Ndoto ya Mwalimu

Kumbe sasa, Salim alikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere. Alitamani kumuona akiongoza nchi kabla ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Hatumsemi Rais John Magufuli, kwani wakati Mwalimu anafariki dunia Oktoba 1999, hakuwa amechipuka vema kisiasa.

Turejee kwa Mwinyi na Mkapa ambao Mwalimu Nyerere aliwafanyia kampeni, au Kikwete ambaye Mwalimu alikufa hajawa Rais, lakini alimwambia achukue fomu, bila shaka wote hao, walikuwa chaguo lenye kufuata baada ya Salim.

Unaweza kupatia ukisema Mwalimu Nyerere alikufa akiumia, akishangaa au akijiuliza kwa nini Salim hajawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Inawezekana Mwalimu Nyerere alimpenda Salim kwa sababu alikulia kwenye uongozi. Tangu akiwa na umri wa miaka 19, Salim alikuwa balozi. Pengine umahiri wake, kwamba kila kazi aliyompa aliifanya vema.

Mwaka 1970 hadi 1980, Salim alikuwa mjumbe wa kudumu wa Tanzania wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1981 mpaka 1984 alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na mwaka 1984-1985, alikuwa Waziri Mkuu. Katika nafasi hizo zote aliwajibika chini ya Mwalimu Nyerere.

Inawezekana Mwalimu Nyerere alimuona Salim anafaa kwa sababu tayari alikuwa mzoefu na alifahamika kimataifa. Miaka ya 1970 alipata kuwa rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vilevile rais mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Salim alikaribia kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1981, alishinda kwa kura dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu, Kurt Waldheim, raia wa Austria. Marekani ilimkataa Salim kwa kura ya veto.

Hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995, Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi Salim alivyokaribia kuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine mwaka 1996 dhidi ya aliyeshikilia nafasi hiyo, Boutros Boutros-Ghali, raia wa Misri, lakini Ufaransa ikaahidi kumpigia kura ya veto.

Ni kipimo kuwa Salim mbele ya macho ya Mwalimu Nyerere, ama alikuwa kiongozi mzuri kihulka na uzoefu, au anayefahamika na kukubalika kimataifa, hivyo ilimpendeza mno angekuwa Rais, lakini Mwalimu alikufa ndoto yake haijatimia.

Ni darasa kubwa

Kama swali litakuwa kwa nini Salim hajawa Rais wa Tanzania? Majibu ni mawili; Mosi, si kila alichokitaka Mwalimu Nyerere kilitimia. Tanzania ni ya Watanzania wote, kuna alichotamani yeye lakini kikazidiwa nguvu. Kiu yake ya Salim kuwa Rais ilizidiwa nguvu.

Pili, sifa nyingi za kiuongozi kuliko wengine si kigezo pekee cha kupata nafasi. Salim alikuwa na sifa nyingi kimataifa kuliko Mwinyi, Mkapa hadi Kikwete, lakini wenzake walifanikiwa kuongoza nchi, yeye alipojitokeza mwaka 2005, alichokipata aliapa kutorudia tena kugombea urais.

Salim ni ndoto ya Mwalimu Nyerere ambayo haikutimia. Pamoja na hivyo, haiondoi ukweli kuwa Salim ni hazina kwa nchi. Ana maarifa na uzoefu mkubwa. Ni wajibu wa viongozi wenye mamlaka kumtumia, tunu iliyopo kichwani kwake isikae bila kulifaa Taifa.