KAKAKUONA: Tunasubiri Rais afoke ndiyo mambo yaende?

Wednesday October 23 2019

 

By Daniel Mjema

Kila eneo na kila wilaya au mkoa alipofanya ziara, Rais John Magufuli amekutana na kero nyingi na wakati mwingine kulazimika kutumia lugha ya ukali, najiuliza hivi hayo maeneo hayana watendaji?

Kama kila jambo sasa limesimama hadi Rais au waziri mkuu atembelee maeneo yetu ndio lipate ufumbuzi, basi naona kuna shida kubwa ya kimfumo au kuna tatizo kubwa kwa watendaji wetu.

Ni kama watendaji wa Serikali kuanzia mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wamemwagiwa maji ya baridi, kiasi kwamba kila kitu kinamsubiri Rais.

Mathalani, Rais alipokuwa Nachingwea alilazimika kutumia lugha kali dhidi ya mkurugenzi wa halmashauri kutokana na ukarabati wa soko kuchukua muda mrefu licha ya kutumia Sh71 milioni.

Lakini akiwa Masasi, Mkoa wa Mtwara, Rais alimweleza Waziri wa Maji, Makame Mbarawa kwamba angemfukuza uwaziri baada ya upembuzi yakinifu wa mradi kuchukua miezi sita.

“Nitazungumza mara ngapi. Waziri sitaki hiki. Nakupa wiki mbili wamalize feasibility study (upembuzi yakinifu) na wakati mwingine si lazima wafanye huo upembuzi. Wanaweza kuchora na kujenga.”

Advertisement

Akiwa hukohuko, akaamuru kuondolewa kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa mmoja wa Kusini, kwa kushindwa kuwachukulia hatua wanaodaiwa kula fedha za wakulima.

Hii ni mifano ya karibuni kabisa lakini ipo mingine mingi ambapo Rais Magufuli au waziri mkuu, Kassim Majaliwa, waliwajia juu watendaji ama kwa ufisadi au kwa kutotatua kero za wananchi.

Ukitizama sana, ni kama watendaji wamekuwa waoga kufanya maamuzi, hawamuelewi Rais anataka nini na pengine ukali na kutotabirika anataka nini kunawatia hofu zaidi.

Wakati mwingine Rais unamuona kabisa anavyoumia kwa namna wateule wake wanavyoshindwa kwenda na kasi yake na yeye anatamani matokeo, si kujivutavuta kwa watendaji wake.

Mkoani Kilimanjaro, kuna mradi mkubwa wa maji wa Mwanga-Same-Korogwe unaogharimu zaidi ya Sh650 bilioni na umesimama tangu Januari 2019, hivi Mbarawa anamsubiri Rais aende Mwanga?

Katika eneo linalofanya vibaya ni miradi ya maji nchini, huko ndiko kuna upigaji wa kufa mtu, lakini vyombo vya dola ikiwamo Takukuru zipo maeneo hayo, hakuna watu wanaoshtakiwa.

Sawa, Takukuru wanaweza kujitetea kuwa wao wakishapeleleza wanapeleka jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) na huko ndipo mambo yanakwamia, kwanini sasa wasimweleze Rais?

Lakini pengine tunaweza kuwaona watendaji ndio tatizo, lakini upande wa pili inawezekana ukali huu wa Rais hauwasaidii watendaji kuwa na ujasiri wa kutenda kwa kuogopa kuumbuliwa hadharani.

Suluhisho pekee kama lilivyo lengo namba 16 la malengo endelevu ya dunia ni kuwa na taasisi imara zinazoongozwa kimfumo na kisheria na si kwa utashi wa mtu mmoja. Utawala bora ni muhimu sana.

Lakini pia ipo haja sasa ya kutafakari kama mfumo tunaoutumia kuwapata watendaji wa Serikali kama wakurugenzi, makatibu tawala wa wilaya na mikoa, unasaidia kupata watendaji bora wa Serikali.

Ukweli ni kwamba mfumo huu wa sasa hatujasaidia, ndio maana tangu aingie madarakani 2015, Rais anaonekana kama bado anaunda Serikali licha ya kubakiza mwaka mmoja.

Huko nyuma watendaji hawa walipikwa ndani ya utumishi wa umma na si kuteua kutoka miongoni mwa makada wa CCM, ambao hawajui mfumo wa utumishi wa umma.

Advertisement