Katu huwezi kustaafu kisha ukabakia kazini

Moja ya mambo makubwa ambayo wanasaikolojia wa nchi za Kiafrika wanapaswa kuyashughulikia kwa nguvu ni dhana ya kustaafu inayoambatana na misingi ya kukubali, kujiandaa na kukubali matokeo yake.

Ni wazi kuwa, dhana ya kustaafu bado haijafahamika vizuri miongoni mwa Waafrika wengi na inawaathiri viongozi wa juu serikalini, watumishi wa kada mbalaimbali.

Kutojiandaa kustaafu

Viongozi na watumishi wengi wa umma katika nchi za Kiafrika huwa hawajiandai kustaafu. Matokeo yake hujikuta wakikatalia madarakani au kupata woga mkubwa tarehe zinapokaribia.

Kutojiandaa kustaafu ni kosa kubwa kiutumishi linaloweza kuharibu maisha yaliyobaki ya mtu anayestaafu. Ni tatizo ambalo hupelekea viongozi na watumishi wengi kuishi maisha mafupi zaidi baada ya utumishi kwa sababu hawakujiandaa.

Kwa kawaida, na ni kanuni ya asili kuwa mwanadamu huzaliwa, baadaye kijana na kuingia kazini, baadaye huwa mtu mzima na hatimaye akifikisha miaka 60 au 65 hustaafu na kuacha kazi za umma akielekea uzeeni.

Kutojiandaa kustaafu ni kitendo cha mtumishi wa umma au sekta binafsi kufikisha miaka 60 au 65 akiwa bado anataka kuendelea na majukumu ya ofisi yake ya ajira, na inapotokea ameagwa rasmi na kutokuwa sehemu ya taasisi hiyo, hubaki na kinyongo rohoni mwake kwa sababu hakujiandaa kustaafu.

Maandalizi ya kustaafu

Maandalizi ya kustaafu si makubwa sana. Kwa kawaida huanza kwa mhusika kujua anastaafu mwaka gani, kisha humpasa kufanya hesabu za idadi ya miaka iliyobakia hadi kufikia tarehe hiyo na kuigawa miaka hiyo katika malengo.

Malengo ya mtu anayejua atastaafu baada ya muongo mmoja, miwili, mitatu au minne yanapaswa kuwa ni pamoja na kutenda na kufanya maamuzi ambayo alitamani yafanywe kwa ajili ya jamii yake, ili anapoondoka asiwe anaumia kuwa aliyotamani hayakaufanyika.

Kama ni kiongozi na unatamani watoto wasome bure kwenye kijiji chako, kata, wilaya, mkoa au ngazi zingine, tumia nafasi ya uongozi uliyonayo hivi sasa kushawishi na kutenda kwa mujibu wa matamanio yako kwa ajili ya ustawi wa wananchi wako ungali na madaraka au utumishini.

Ukishastaafu si rahisi kupata nafasi ya kutatua matatizo ya wananchi ambayo hukuweza kuyatatua ukiwa na madaraka au na sifa ya utumishi.

Baada ya kustaafu

Hili ni eneo muhimu kwa mtu yeyote ambaye amekuwa na madaraka yoyote ya kiutumishi au kiuongozi.

Mambo ambayo ungelipenda kuyafanya wakati unapostaafu yanapaswa kuanzishwa wakati ukiwa kazini. Mathalani, ikiwa unadhani kuwa ukishastaafu utakuwa mwekezaji wa kilimo cha matunda na mbogamboga, ni muhimu kuanza kilimo hicho wakati ukiwa kazini, ukiwa kiongozi au mtumishi na kuhakikisha unakuwa mfano bora kwa wengine lakini ukitumia mwanya huo kufanya mazoezi ya yale ambayo yataenda kuwa maisha yako baada ya kustaafu.

Wastaafu wengi hupata shida kubwa ya kuanza kufanyia kazi mawazo na matamanio yao ya hali ya ustaafu kwa sababu hulazimisha kuanza mambo ambayo hawajawahi kuyafanya.

Kama mstaafu alikuwa na mipango ya kuanza kufuga kuku kibiashara baada ya kustaafu, ni muhimu walau miaka 5 au 10 kabla ya kustaafu akaanza kazi ya ufugaji kuku kibiashara na akazoea shughuli hiyo.

Ukifanya hivyo, utakapostaafu hutaanza kujifunza kufuga kuku, utatumia fedha zako za kiinua mgongo kuwekeza zaidi kwenye biashara ya ufugaji kuku kibiashara.

Huwezi kula keki, ukabakia nayo

Ukishastaafu muda wako unakuwa umepita. Wewe mwenyewe unakuwa umeshapitwa na wakati, huwezi kuleta mabadiliko katika jamii yako baada ya kustaafu kwa sababu muda huo unakuwa hauna nguvu ya maamuzi. Unakuwa umebakia na nguvu ya kutoa mawazo na kushauri peke yake.

Hata kama utalia na kujigaragaza, ukishastaafu unakuwa umestaafu. Haya ambayo unaweza kujigaragaza na kulia nayo kwa nguvu, ni mambo ambayo ulipaswa kuyatekeleza ulipokuwa na dhamana na nguvu.

Kwa nchi zetu za Afrika, wastaafu wengi hubaki kulalama na kulalamika kuwa mambo hayaendi vizuri hapa au pale. Hulalamikia mambo ambayo walipaswa kuyawekea utaratibu wao wenyewe walipokuwa madarakani.

Mathalani, utamkuta mwalimu mkuu mstaafu analalamika kwamba watoto wa shule aliyowahi kufundisha hawana nidhamu na wanatoroka sana. Kumbe mwalimu huyu alipaswa kuwaunganisha wazazi wakati akiwa mwalimu mkuu ili wajenge uzio wa kisasa kuzunguka shule na kuwe na milango rasmi ya kuingia na kutoka shuleni ili kuzuia watoto wasitoroke.

Kama mwalimu huyu angetimiza wajibu wake wakati alipokuwa na mamlaka na maamuzi, leo hii asingeliwalalamikia aliowaachia shule kwamba wameshindwa kudhibiti utoro.

Wastaafu husema kimyakimya

Moja ya kanuni muhimu za kustaafu ni kujifunza kukaa kimya na kuwa mshauri wa kimyakimya. Ni muhimu kujifunza kukaa kimya na kuwaacha uliowaachia ofisi watende na kufanya kazi bila bugudha.

Kama kuna jambo unaona haliko sawa, ni muhimu kuwafuata wahusika, kujifungia nao chumbani na kuliteta na kuwashauri. Ukihamia barabarani na kupiga kelele utatafsiriwa kama mvurugaji, na hiyo ndiyo maana sahihi itakayokufaa.

Nadhani kwa bara la Afrika, kila watumishi na viongozi wa ngazi mbalimbali, wanahitaji somo la maisha baada ya utumishi au uongozi, maisha ya kustaafu.

Watu wengi wanaostaafu huanza maisha mapya ambayo hawajawahi kuyaonja, ni muhimu watu hawa wakaandaliwa tangu wakiwa kazini, wakafunzwa mbinu za kujiandaa kustaafu ili wanapostaafu wakapumzike, wawe washauri, wasiwe watu wa lawama na wapiga kelele, maana huwezi kustaafu halafu ukabakia kazini.

Julius Mtatiro ni mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Simu; +25578753675. Barua Pepe; [email protected]