MAKALA YA MALOTO: Kigwangalla, Mkenda bado wapo? Hakika Rais Magufuli ana huruma

Friday January 17 2020

 

By Luqman Maloto

Siku Rais John Magufuli alipotishia kuwafukuza kazi Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, hazikupita saa nyingi ufumbuzi ulipatikana.

Rais Magufuli alisema, Kigwangalla na Mkenda walikuwa hawaelewani kiasi cha kutozungumza. Eti walikuwa wanapitana kwenye korido bila hata kusalimiana na kila siku wanagombana.

Rejea maneno “kila siku wanagombana”, tafsiri yake ni kuwa ugomvi wao sio wa kitu kimoja, bali ni kawaida yao. Tena Rais Magufuli amesema kwamba kutokana na ugomvi, mambo mengi wizarani hayaendi.

Ni sahihi kusema kuwa Kigwangalla na Mkenda, kwa sababu ya ugomvi wao, mambo mengi wizarani yalikwama. Ni sawa na kusema kwamba Kigwangalla na Mkenda wamezorotesha maendeleo ya wizara.

Tuje kwenye matokeo baada ya kauli ya Rais Magufuli. Jua halikutua, Kigwangalla alitoa taarifa mtandaoni kuhusu kumaliza tofauti zake na Mkenda.

Kigwangalla na Mkenda ni watu wazima, wasomi, kila mmoja alipoteuliwa na kula kiapo, alipewa utaratibu wake wa kazi. Kwa maana hiyo, kila mmoja anaitambua mipaka yake.

Advertisement

Kwa mtazamo huo, unaweza kuwatafsiri vipi viongozi wawili wanaoshindwa kuheshimu mipaka yao ya kazi na matokeo yake wanagombana mara kwa mara?

Na kwa sababu baada ya kitisho cha kufukuzwa kazi walikutana haraka kumaliza tofauti zao, je, wameelewana kwa dhati au wamelazimishwa na shinikizo la kupoteza kazi? Kama jibu ni ndiyo, maana yake wametengeneza maelewano ya maigizo lakini si ya moyoni, hivyo hawatafika popote.

Tunaweza kukubaliana kuwa kweli wameelewana kutoka moyoni. Je, wakiwa watu wazima walikuwa wanasubiri mpaka Rais aseme ndipo waelewane? Na endapo Rais asingesema chochote, mpaka leo wangeendeleza ugomvi wao?

Nikiielewa vizuri kauli ya Rais Magufuli ni kwamba Kigwangalla na Mkenda ni wagomvi wa muda mrefu. Kwa mantiki hiyo, ni watu ambao ilishindikana kufanya kazi pamoja, mpaka alipoamua kuingilia kati na kuwatishia.

Sasa basi, kama tatizo ni la mmoja, huyo hajui wajibu wake. Ikiwa kila mtu ana mchango kwenye matatizo yaliyozaa ugomvi, dhahiri wote hawafai. Kitapita kipindi kifupi kisha watarejea kulekule. Waungwana hunena kwamba tabia ni kama ngozi.

Ukifika hapo ndipo unaona huruma ya Rais Magufuli. Kwamba watu ambao kwa muda mrefu aligundua wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya Serikali, lakini aliamua kuwaonya na kuwataka wamalize tofauti zao.

Yupo mtu anaweza kuuliza; je, ni kazi ya Rais kuwaambia watendaji wa wizara kuacha ugomvi au wahusika wenyewe walipaswa kutambua kwamba ugomvi haufai na ni adui wa utendaji?

Je, kwa watu wazima na wasomi kama hao, kweli hawakujua kuwa chachu namba moja ya ufanisi kwenye kazi zao hususan wizara waliyopewa kuiongoza ni uhusiano mwema? Sifa ya uongozi ni uwezo wa kujisimamia, wao hawakuweza mpaka Rais alipoingilia kati.

Ikiwa wenyewe kama wakuu wa wizara walikuwa mfano mbaya kwa watumishi wengine, unaweza kujiuliza walikuwa na lipi la kufanya ili kusaidia kujenga uhusiano mwema kwa watumishi wengine ndani ya wizara?

Wakati fulani Rais Magufuli alisema kuwa kazi ya kuteua na kutengua ni ngumu sana. Kwamba kuna wakati huumia kichwa kufanya uamuzi, mpaka hulazimika kulala na kuamka.

Pengine mpaka Rais Magufuli alipoamua kuzungumza na kuwataka Mkenda na Kigwangalla kumaliza tofauti zao ni kwa sababu ya ugumu ambao Rais huupitia katika kutengua na kuteua. Kwamba wakati mwingine huona bora kusahihisha waliopo.

Kwa muktadha huohuo ni dhahiri wasaidizi wa Rais huongeza ugumu kwake. Mtu umepewa kazi, ni mtu mzima, iweje utake tena Rais akukumbushe hata kusalimiana na bosi wako au msaidizi wako ofisini?

Ingekuwa Rais hafuatilii mambo yenye kuhusu uhusiano wa wasaidizi wake ili kuwa na uhakika na kazi zilivyofanyika, maana yake nchi inaweza kukwama.

Liwe somo kwa watendaji wengine kutambua kuwa kudumisha uhusiano na maelewano kazini ni jukumu la mhusika, tena ni la lazima. Si kusubiri sauti ya mamlaka ya juu ndio mtu aogope.

Advertisement