Kisutu imetengeneza jukwaa la siasa za mahakama kuelekea Oktoba 2020

Ghafla, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imegeuka ‘jukwaa la maonyesho ya kisiasa’ kati ya CCM na Chadema kwa kuungwa mkono waziwazi na ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi.

Viongozi wa juu wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uchochezi, kufanya mkusanyiko usio halali na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Wengine katika kesi hiyo walikuwa John Mnyika, Dk Vincent Mashinji (aliyekuwa katibu mkuu Chadema), Salum Mwalimu (naibu katibu mkuu Zanzibar), Halima Mdee (mwenyekiti Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko (mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti na mbunge wa Tarime Mjini).

Peter Msigwa (mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa na mbunge wa Iringa Mjini), Ester Bulaya (mbunge Bunda Mjini na mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni) na John Heche ambaye ni bunge wa Tarime Vijijiji na mjumbe wa Kamati Kuu.

Wote kwa pamoja walikutwa na hatia katika makosa 12 kati ya 13 waliyoshtakiwa, hivyo kuhukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano kila mmoja.

Sasa, Chadema walianza kuchangisha michango ya kuwalipia faini viongozi wao.

Ndani ya saa nane walifikisha Sh108 milioni. Zilipotimu saa 16 tangu kuanza michango hiyo, taarifa za Chadema zilitaja makusanyo kufikia Sh234 milioni.

Kasi ya uchangishaji ikawa kubwa na muitikio ukawa wa hali ya juu.

Baada ya hukumu, asubuhi iliyofuata katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliongoza ujumbe wake kwenda mahakamani hapo kumlipia faini Mashinji.

Japo alishtakiwa akiwa Chadema, alipohukumiwa tayari alikuwa mwanachama wa CCM.

Hivyo, CCM waliwahi kumtoa mwanachama wao.

Tafsiri ni kuwa CCM walionyesha msuli wao wa kiuchumi kwa kuwa wa kwanza kumtoa jela Mashinji ambaye peke yake alikuwa akidaiwa Sh30 milioni ili awe huru.

Chadema msuli wao waliuelekeza kwa umma.

Ndururu si chururu, lakini akaunti za fedha kwenye mitandao ya simu na benki zilifoka fedha kwa kasi kubwa.

Turudi siku ya hukumu. Mshauri wa ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad, mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, walikuwepo mahakamani kuungana na viongozi wa Chadema.

Tena, taarifa ya ACT-Wazalendo, iliyotolewa na ngome yao ya vijana ilihamasisha wanachama wao kuungana na Chadema mahakamani.

Kwa kuweka kwenye kapu moja, mambo yote yaliyojiri na yanayoendelea kujiri baada ya hukumu dhidi ya viongozi wa Chadema, unaweza kupata mambo mawili; mosi ni nukuu ya mwandishi mashuhuri wa Uingereza, William Shakespeare. Pili, ni siasa za mahakama.

Tuanze na Shakespeare. Aliandika “a friend in the court is better than a penny in purse”.

Alimaanisha kuwa rafiki anayeambatana nawe mahakamani ni bora kuliko fedha kwenye pochi.

Kutafsiri mshikamano wa wapinzani kutokana na kesi za viongozi wa Chadema maana yake bila shaka kuna jambo zito ndani ya nyoyo zao ambalo limejitengeneza au wamelitengeneza.

Ni ule urafiki unaozidi thamani ya fedha ndani ya pochi. Kasi kubwa ya ukusanyaji michango kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wa Chadema imeonyesha ni kiasi gani chama hicho kina wigo mpana wa wafuasi na ulio hai. Pia jinsi hukumu dhidi yao ilivyogusa watu wengi.

Imedhihirika kuwa viongozi wa Chadema wapo upande wa kushoto wa vifua vya wengi, kwa sababu marafiki wa mahakamani ni bora kuliko fedha ndani ya pochi.

Kuhusu siasa za mahakama (court politics), ni kwamba siasa za nchi zinapakwa rangi kutokea chumba cha mahakama, Kisutu.

Mazingira ya siku ya hukumu na mpaka hukumu yenyewe ilipotoka, si tu yamevifanya vyama vya upinzani kuwa na mshikamano wa imani kubwa, bali pia umewapa fursa wapizani wenyewe kujipima na kuona msuli wao na nafasi yao kwa umma.

Zitto Kabwe, kiongozi wa ACT-Wazalendo, hakuwepo mahakamani, lakini baada ya hukumu alikuwa mstari wa mbele kuhamasisha michango.

kama haitoshi, Zitto aliongoza ujumbe wa ACT kwenda makao makuu ya Chadema Kinondoni, Dar es Salaam, kuwasilisha mchango wa chama chao.

Ndivyo siasa zinavyopata sura mpya kutokea mahakamani, hukumu iliyotolewa imechukuliwa kama jukwaa la siasa.

Kutoka CCM na hatua za haraka kumtoa Mashinji jela, hadi vyama vingine vya upinzani vinavyotumia fursa hiyohiyo kusikitika pamoja na Chadema.

Kutoka Chadema na michango yenye kasi, hadi Chadema hiyohiyo na uamuzi au ujanja ambao umekibeba chama mbele ya wanawake. Kilichotokea mahakamani kimetengeneza jukwaa pana kwa kila chama kujaribu kulitumia kwa namna chanya.

Taarifa ya Chadema kuwa baada ya kukusanya michango ya awali, wangeanza kuwalipia faini wanawake-- Mdee, Matiko na Bulaya-- iwe waliamua kwa kujali au mkakati kisiasa, bila shaka uamuzi huo unaingia ndani kabisa kwenye nyoyo za wanawake wengi na kuonyesha kuwa chama hicho kinamjali na kumthamini mwanamke.

Pengine uamuzi huo wa kutangulia kuwatoa jela wanawake ulifikiwa baada ya mabishano, au labda yalishakuwepo mawazo ya kuanza kumtoa jela mwenyekiti.

Vyovyote vile, mtoa wazo na waliolipitisha walicheza mpira mtamu wa kisiasa kwa wanawake na hata mbele ya wanaume wenye huruma kwa wanawake.

Linaweza kuwepo swali, nini kingetokea kama hukumu isingekuwa kama ilivyo? Ama wangeachiwa huru au kusingekuwa na fursa ya kulipa faini. Jibu ni moja; siasa zingeendelea kama zilivyoanza.

Hukumu ingekuwa kuachiwa huru, tambo za ushindi zingesikika. Viongozi wa Chadema wangesema kesi ilifunguliwa kisiasa na wangemsifu hakimu kwa kutenda haki.

Zingatia siasa zilishaanza kabla ya siku ya hukumu. Wiki moja kabla, Mbowe aliwaaga wapigakura wake jimboni Hai kuwa wajiandae kwa lolote ambalo lingetokea.

Kwamba hata angefungwa jela wasivunjike moyo.

Kisha tena, siku ya hukumu aliandika ujumbe kupitia akaunti yake ya Instagram akiwataka wananchi wawe watulivu, wasivunjike moyo kwa hukumu ambayo ingewakuta. Hiyo inaonyesha kuwa alishaanza kutumia mapema kesi yao kujenga hamasa na huruma ya kisiasa.

Na kama hukumu ingekuwa kifungo bila faini, kelele kuwa wamefungwa kisiasa zingekuwa nyingi kwa kipindi chote ambacho wangekuwa jela.

Kwa kifupi, huwezi kuzuia mahakama kutumika kisiasa katika mazingira ambayo wanaoshitakiwa, kushitakiana au kuhukumiwa ni wanasiasa.

Ila sasa kilichopo ni namna siasa za mahakama zinavyoendelea, zinaweza kujenga tafsiri kwa kiasi fulani kuhusu kiwango cha wapinzani kukubalika.

Kwa sasa hakuna tafiti za maoni yenye kuibua matokeo ya nafasi za vyama kwa sababu shughuli za kisiasa zimekuwa na vizingiti vingi, hivyo mwitikio wa michango kwa Chadena unaweza kutoa picha ya nguvu za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2020.

CCM bila shaka watajifunza kwa matokeo ya michango ya watu kuona nguvu ya wapinzani kuelekea Oktoba, Chadema nao wanaweza kuwa na imani kubwa kwamba wanapendwa na watu wengi kwa moyo, hali na mali.

Hata hivyo, wasisahau kuwa kuna wachangiaji wengi wameongozwa na huruma.

Inawezekana wapo pia wasio na vyama, lakini walivutwa na huruma.