Kiza Mayeye: Tunaweza hata bila kuwezeshwa

Muktasari:

Wiki iliyopita mwandishi wetu Habel Chidawali alifanya mahojiano na Kiza Mayeye, mbunge wa Viti Maalumu (CUF) akizungumzia mambo mbalimbali huku akieleza imani yake kuwa “mwanamke anaweza hata bila ya kuwezeshwa.

Swali: Ni hivi majuzi umeteuliwa kuwa mbunge, tueleze historia yako na uzoefu katika siasa.

Jibu: Siasa nilianzia chuoni. Nilichagua chama cha CUF kwa sababu naamini katika haki na usawa, jambo ambalo linasimamiwa na chama hicho ingawa wakati huo hakikuwa na nguvu kubwa mkoani Kigoma nilikozaliwa ukilinganisha na vyama vingine.

Nilizaliwa Kijiji cha Mwandiga, Mkoa wa Kigoma na nimesomea mahusiano ya umma katika ngazi ya shahada nikihitimu mwaka 2010.

Swali: Ilikuwaje hadi ukapata ubunge?

Jibu: Nilipomaliza chuo kikuu nilianza harakati za siasa huku nikifanya kazi benki. Ilipofika mwaka 2014 niliacha kazi na kujikita katika siasa na ujasiriamali nikilima mazao ya biashara.

Mwaka 2015 niliomba kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini lakini sikuteuliwa baada ya muungano wa Ukawa. Chadema waliokuwa na nguvu walisimamisha mgombea, nikajikita kugombea viti maalumu.

Wakati huo kura za chama hazikutosha na hivyo jina langu halikufikiwa katika uteuzi, lakini likasogea na tume hadi ilipopatikana nafasi.

Swali: Nini kilikusukuma kwenda bungeni?

Jibu: Ni sauti za wanyonge, nilitamani siku moja niwe mtu wa kuwasemea wanyonge wa Tanzania bila kujali itikadi za vyama vyao na ndiyo kazi ninayofanya hadi sasa napambana kuona taifa linakuwa moja lenye upendo.

Swali: Umeifikia ndoto hiyo kwa kiasi gani?

Jibu: Mimeifikia japo kwa kiasi, nalalamika kila wakati kuhusu barabara, maji, afya na elimu kwa watoto wa kike ambako bado kuna shida hasa Mkoa wa Kigoma.

Kwa mfano, katika zahanati nyingi za mkoa wetu hakuna dawa, hakuna madaktari wa kutosha wala watumishi wa kada hiyo. Pia, mkoa unaozungukwa na Ziwa Tanganyika na Mto Malagalasi, maji ni tatizo kubwa kwetu.

Swali: Kwenye elimu hali ikoje?

Jibu: Ni shida, watoto wa kike ndiyo wahanga wakubwa katika kutafuta elimu. Bado nina kazi ya kutoa elimu kwa jamii kutambua umuhimu wa kusomesha watoto wa kike ili kuwajengea uwezo.

Swali: Kuna wanaosema hakuna ajira, hivyo watoto wa kike ni mtaji wakiolewa, wewe unasemaje?

Jibu: Hilo halikubariki, ukosefu wa ajira si tatizo kwa wanawake pekee, bali hata vijana wa kiume linawagusa. Mimi ninao vijana wengi ambao hawana ajira na kwa sasa nimeamua kuomba ardhi ili tujikite katika kilimo kuliko kuwaacha wakirandaranda.

Swali: Unawazungumziaje wanawake kwa ujumla?

Jibu: Ndiyo wapiga kura wangu. Niko nao karibu sana, zaidi wanahitaji kupewa elimu ili waweze kujiamini katika shughuli zao na wasitegemee kuwatanguliza wanaume katika mambo ya uchumi bali wapambane.

Swali: Baadhi ya wanasiasa wanawake huelezwa kuwa wanapata nafasi na upendeleo, wewe ulipataje nafasi hii.

Jibu: Sijawahi kuamini hilo, siamini na sitaamini ingawa nimekuwa nasikia mambo hayo.

Swali: Tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani uchaguzi mkuu, umejipangaje?

Jibu: Siwezi kukueleza najipangaje lakini nina deni la kufanya kwa wanawake wa CUF na wale wa Kigoma. Ngoja nipambane katika nafasi hii ya kuwatumikia wanawake kitaifa na wabunge wa CUF.

Swali: Kwani una nafasi gani kwa wanawake ndani ya CUF?

Jibu: Nimeteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa wanawake wa CUF Bara. Mwenyekiti wetu ameniona na vikao vimenikubali sasa nataka kuonyeshe kipaji changu na moyo wa kuwasaidia wanawake ili kuwaunganisha wawe kitu kimoja.