HOJA ZA KARUGENDO: Kuhama chama cha siasa si kosa isipokuwa...

Kwa mara ya kwanza katika historia ya vyama vingi vya siasa nchini, tumeshuhudia wimbi kubwa la wabunge na madiwani wakihama vyama vyao na kujiunga na chama tawala.

Vyovyote vile, kuhama chama cha siasa na kujiunga na kingine si kosa, isipokuwa kama mtu anahama kwa lengo la kukaa kwenye meza ya chakula.

Kama lengo la kuhama ni kutafuta cheo, maslahi binafsi, kushibisha tumbo na kuishibisha familia, ukoo, kabila na kujitengenezea jina, hii ni dhambi ya mauti.

Kama mtu anahama chama ili kuleta ufanisi katika kulijenga taifa ni jambo jema. Tanzania ni yetu sote, cha muhimu si vyama vya siasa bali Utanzania wetu. Hivyo, anayehama chama kimoja na kujiunga na kingine kwa lengo la kuujenga Utanzania wetu, hana tatizo na wala asiitwe msaliti au kupokelewa kama shujaa kule anakotimkia.

Tunahitaji elimu ya kutusaidia kutofautisha vyama vya siasa na Utanzania wetu. Elimu ya kutupatia mwanga wa kutambua kwamba vyama vya siasa vitakuja na kupita, lakini Utanzania wetu ni wa kudumu. Elimu hii ambayo inaweza kumsaidia mtu kuutambua ukweli, kuwa na maadili mema, kuipenda haki na kuishi katika mwanga ndiyo tunayohitaji kwa sasa.

Tunahitaji elimu tafakari na elimu bunifu. Elimu inayoweza kutusaidia kutofautisha kati ya Mtanzania na Utanzania, tofauti kati ya mambo yanayopita na yale yanayodumu. Elimu ya kutusaidia kuangalia maslahi ya Taifa, kabla ya kuangalia maslahi ya mtu binafsi. Elimu ya kutusaidia kuijenga Tanzania si ya leo tu, bali Tanzania ya vizazi vijavyo inayodumu milele.

Jambo muhimu ni kuujenga utanzania zaidi ya vyama vya siasa. Hili likiwa wazi, huwezi kusikia majigambo na mipasho ya kisiasa, huwezi kusikia tena misemo ya “Uchovu” kukomboa majimbo kana kwamba yalikuwa mikononi mwa Warundi au Wanyarwanda, huwezi kusikia tena ushindi wa kishindo au kushinda asilimia 100, huwezi kusikia “Wataweza” kana kwamba tunashindana na Wakenya au Waganda.

Utasikia nyimbo za umoja, mshikamano na za kujenga nchi. Tutatofautiana njia za kupitia, lakini tunaelekea sehemu moja, tutatofautiana kwa sera, lakini tunalijenga taifa moja. Haya ndiyo mambo ya msingi ambayo kwa bahati mbaya, tunayaweka pembeni na kutaka kutukuza vyama vya siasa kuliko taifa.

Kawaida ni kwamba vyama vyote vinalenga kutoa huduma kwa raia. Chama chochote kinachofanikiwa kushinda, kinaunda serikali iliyowekwa madarakani na raia na serikali hii inawajibika kwa wananchi.

Serikali ni mtumishi wa wananchi. Uhusiano kati ya wananchi na serikali ni wa mkataba, yaani kuna mkataba kati ya wananchi na viongozi wao.

Katika jambo hili, viongozi na wawakilishi wengine wanafanya uamuzi kwa niaba ya mwananchi ambaye ni raia. Serikali inalazimika kufuata masharti ya mkataba kati ya wananchi na viongozi na wawakilishi wengine.

Tanzania inatumia mfumo wa uchaguzi ambao mgombea anayepata kura nyingi ndiye mshindi. Pia, Tanzania inatumia uwakilishi wa nusu uwiano katika uchaguzi wa wawakilishi wa wanawake katika Bunge. Haya yakiwa wazi kwa wapiga kura, haiwezekani kutokea vurugu au kuhama chama kimoja kwenda kingine.

Bado hatujajipanga vya kutosha kulijenga taifa letu. Bado tunaangalia vyama na ustawi wa vyama vya siasa badala ya kuangalia ujenzi wa Taifa letu.

Bila mfumo unaoeleweka, bila mfumo imara wa kujenga utaifa na uzalendo, kuhama utakuwa ni utamaduni wetu.

Bado watu wanataka kuyashibisha matumbo yao, kuzishibisha familia zao na labda watu wa makabila yao.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha mtu anajongea kwenye meza ya chakula. Hapo tunaweza kusema mtu huyo amekosea na kwa namna moja ama nyingine ni dhambi ya mauti kulitelekeza taifa kwa lengo la kujishibisha wewe binafsi na familia yako.

Ni bahati mbaya tumezalisha utamaduni wa watu kutamani kukimbilia kwenye meza ya chakula badala ya kuiandaa meza ya chakula kwa wote.

Bila kulisahihisha hili kwa haraka, tutaendelea kushuhudia kuhama kutoka upinzani kwenda chama tawala na hatujui ya kesho, yaweza ikawa ni kuihama CCM kuelekea popote pale.