MAKALA YA MALOTO: Kwa hili la Idris Sultan, Makonda amemkosea zaidi Rais Magufuli

Ni kweli, Wamarekani wamewekwa huru sana hadi kuonekana wanatumia uhuru wao vibaya. Na kwa huo ubaya, huwakosea mpaka viongozi wao.

Ni jambo la kawaida kuona raia wa Marekani, hasa watu maarufu kuonekana wakilumbana na Rais Donald Trump ama kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.

Ni kawaida wasanii kutumia sanaa yao kumjadili na kumsokoa Rais Trump. Wanamuziki wa Hip Hop, Snoop Dogg na Eminem, ni mfano wa karibu wa waliorekodi nyimbo hasi dhidi ya Trump.

Machi 12, 2017, Rapa wa Marekani, Snoop Dogg alitoa wimbo unaoitwa Lavender (Nightfall Remix) ambao maudhui yake ni kutetea jamii ya Wamarekani weusi dhidi ya Serikali ya Marekani.

Snoop Dogg anaimba akirap kuwa polisi wa Marekani na Serikali yote ni adui wa Wamarekani weusi, wenye kuwakandamiza. Anasema usiku ukifika ndiyo itakuwa tamati yao kwa sababu wanastahili pigo la bunduki.

Katika video ya wimbo huo, kipande cha mwishoni kinaonyesha usiku umefika ili hukumu ya bunduki itimie, yupo mtu amevalishwa wajihi na sura ya Trump.

Ndani ya video hiyo, huyo mtu aliyetengenezwa kufanana na Trump, anatambulishwa kama “Ronald Klump” badala ya Donald Trump kisha anashikiwa bastola na Snoop, kuonyesha kuwa tayari muda wake umefika.

Trump alijibu hiyo video kupitia Twitter, akaandika: “Unaweza kufikiri mayowe yangekuwaje kama Snoop Dogg aliyeshindwa kisanii na kila kitu, angedhamiria kumlenga na bunduki Rais Obama? Muda wa jela umefika.”

Maneno hayo ya Trump kwenye Twitter dhidi ya Snoop, ndiyo yaliamsha hisia kali kutoka kwa wanamuziki wa Rap Marekani, waliomshambulia Rais wao kuwa anatakiwa kumwacha mkongwe huyo wa Rap.

Oktoba 2017, Eminem alitoa wimbo “The Storm” ambao haukuwa na ala (freestyle), pia akimshambulia Trump. Ni wimbo maarufu na uliotazamwa na watu wengi YouTube.

Hata Tanzania, Rapa Ney Wamitego alitoa wimbo, “Wapo” ambao kwa tafsiri ya wengi ni kuwa alimshambulia Rais John Magufuli. Siku mbili baada ya wimbo kutoka alikamatwa na polisi Morogoro kisha kusafirishwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Nay aliachiwa huru baada ya Rais Magufuli kusema aliupenda wimbo huo. Tafsiri ni kuwa Rais Magufuli anapenda na kuthamini sanaa.

Idris na Makonda

Oktoba 30, mwaka huu, msanii wa vichekesho nchini, Idris Sultan anadaiwa kutengeza picha yake na ya Rais Magufuli. Picha yake akaiwekea kichwa cha Magufuli, halafu ya Rais akaiwekea kichwa chake.

Idris akaandika: “Kwa siku moja tukabadilishana kazi ili afurahie siku ya kuzaliwa kwa amani.” Akaambatanisha emoji za kicheko. Ni sanaa aliyotumia katika siku ya kuzaliwa ya Rais Magufuli.

Baada ya kuisambaza mtandaoni, Makonda alimtaka Idris ajipeleke polisi akisema amevuka mipaka ya kazi yake. Siku hiyohiyo Marekani, mchekeshaji Jimmy Kimmel aliandika rekodi ya kuweka video Twitter iliyotazamwa na watu wengi zaidi, wakifikia milioni tisa chini ya saa 24.

Kimmel aliweka pamoja vipande vya video za Trump na mtangulizi wake, Barack Obama. Trump akizungumzia kuuawa kwa kiongozi wa Islmic State, Abu Bakr al-Baghdadi, Syria, hivi karibuni na Obama akielezea kifo cha Osama bin Laden, Pakistan, mwaka 2011.

Mwanzo wa video, Kimmel anasema, Obama alitumia dakika 9 na nusu kuzungumzia shambulio la Osama na kuuawa kwake, lakini Trump alitumia dakika 48.

Alitaka kufikisha ujumbe kuwa Obama hakuweka mbwembwe Marekani ilipomuua Osama ambaye alikuwa mtu hatari zaidi, lakini Trump alinogesha mikogo kwa al-Baghdadi mpaka hotuba yake kubeba muda mrefu bila sababu yoyote.

Jinsi Kimmel alivyoikata video ya Trump na kuunganisha na ile ya Obama, ingekuwa Dar ni jimbo la Marekani na Kimmel ni mkazi wa Dar, halafu Makonda akawa ndo Gavana, bila shaka angeagiza akaripoti polisi.

Na kwa jinsi Wamarekani wanavyoishi kwa uhuru ‘uliopitiliza’, Makonda angehelemewa. Asingeweza. Wamarekani ni vichwa ngumu.

Makonda aache wasanii wafanye sanaa na Rais wao, hasa kama hawamvunjii heshima au kumdhalilisha. Alichokifanya Idris hakimvunjii heshima Rais.

Kwa hili la kumkamata Idris, Makonda amemkosea zaidi Rais Magufuli. Anataka kumweka mbali na wasanii wa nchi yake na kufanya ionekane wasanii na wananchi hawapo huru na Rais wao.

Kingine Makonda atambue kuwa thamani ya kiongozi si kutumia nguvu alizonazo, bali kujizuia kutozitumia. Kama kwa tafsiri yake, picha za Idris na Magufuli zilimkwaza, kabla ya kuagiza msanii huyo kwenda polisi, angetafuta wataalamu wa sanaa wamfafanulie.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ina kila aina ya wataalamu katika ngazi ya mkoa. Wanasheria mpaka wasomi wa sanaa na utamaduni. Wangemwambia kuwa kilichofanyika si dhambi. Tena inawezekana Rais alicheka alipoona picha hizo.

Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wake, Edward Lowassa waliwahi kutengenezewa picha ya wanamuziki wa bendi, Kikwete akipiga drum, Lowassa akipiga gitaa. Picha ilitoka ukurasa wa mbele wa gazeti na hakuna aliyeambiwa aripoti polisi au onyo lolote.

Rais Magufuli ni Rais wa Watanzania wote. Bila shaka Idris anamheshimu. Hakusema wabadilishane kwa sababu yeye anaweza kuongoza nchi vizuri, bali alisema siku moja (kwa utani) ili asherehekee kwa amani siku yake ya kuzaliwa.