Lugha gongana za mapato ya Serikali zinatuyumbisha

Katika andiko la kifalsafa la Republic la mwanafalsafa Plato, husimulia namna galacha wa falsafa duniani, Socrates alivyopata wakati mgumu kujadili maana ya “Haki” na mwalimu wa Uturuki ya kale, Thrasymachus.

Swali lilikuwa “haki ni nini?” Thrasymachus kwanza akamkosoa Socrates kuwa hajui haki ni nini. Alisema haki ni upendeleo anaopata mwenye nguvu na udhalimu ni upendeleo na faida za mtu.

Tafsiri hiyo ikamfanya Socrates kutambua kuwa kuendeleza mjadala wa tafsiri ya haki na Thrasymachus ni kuumiza kichwa. Hawakuwa wakielewana, ingawa kila mmoja aliamini anazungumzia haki kwa usahihi wake.

Kuna msemo wa Kiingereza, “talking past each other”, wenye maana ya mgongano wa tafsiri. Watu wawili au zaidi wanaamini wanachozungumza ni kitu kimoja lakini uwasilishaji wao unawapambanua kuwa wanagongana. Mtaani wanaita lugha gongana.

Kama Socrates alivyovurugwa na tafsiri za Thrasymachus kuhusu haki, ndivyo wananchi hivi sasa wanavyochanganywa na matamko ya viongozi wa Serikali kuhusu shabaha ya ukusanyaji wa mapato.

Shabaha nini hasa? Ni kukusanya mapato bila majadiliano ya aina yoyote na ikibidi kufunga biashara za watu au kuzungumza na wafanyabiashara wanaopepesuka kibiashara na kuwavumilia wazalishe na kulipa madeni?

Kuna watendaji wanaodhani mapato, kudai madeni na kufungia biashara kuwa ndiyo njia ya kukusanya mapato mengi ya Serikali. Viongozi wanasema kufunga biashara za watu ni kuikosesha Serikali mapato mengi na kuua mzunguko wa uchumi.

Mpaka hapo unaona kuwa kuna mgongano wa shabaha ya mapato ya Serikali. Cha kukupa mshangao ni kwamba wanaogongana hivyo ni watu ndani ya Serikali moja. Je, sera ya Serikali ni nini? Kufunga biashara za watu au kuwalea wafanyabiashara wenye madeni ili walipe taratibu bila kuathiri uchumi?

Mwananchi leo anasikia kauli kwamba watu walipe kodi na ikibidi wafungiwe biashara ili Serikali ipate fedha. Kesho, kiongozi mwingine wa Serikali anaibuka na kauli kuwa kufunga biashara kunaikosesha mapato Serikali na uchumi wa nchi unadumaa.

Hapo amwelewe nani? Amwone yupi yupo sahihi, labda sasa tusubiri tuone maana limezungumzwa na katika Bajeti.

Waziri wa Ardhi, William Lukuvi amesema wasiolipa kodi za majengo ya Serikali mpaka Juni 20, mwaka huu, watafungiwa biashara, magari yao na mali nyingine zitakamatwa na kupigwa mnada.

Kauli ya Lukuvi inaenda sawa na hatua ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikizichukua. Kuwafungia biashara wadaiwa wa kodi za mapato, kukamata mali zao na hata kuzipiga mnada. Hatua hii imekuwa ikisababisha malalamiko mengi kwa wafanyabiashara na hata kugonganisha kauli viongozi serikalini.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Godfrey Mwambe kupitia video ambayo imekuwa ikisambaa mitandaoni, anaonya tabia ya kufungia watu biashara kwa sababu athari yake ni kubwa.

Mwambe anasema kumfungia mtu biashara kwanza kunaikosesha mapato Serikali katika maeneo mengi. Anasema, zipo biashara hutozwa kodi za uzalishaji (excise duty), hizo hazisubiri kuuza na kupata faida. Unapozifunga hizo nchi inakosa mapato ya wakati wa kuzalisha na baada ya kuuzwa.

Anaendelea kusema kuwa kufunga biashara kwa sababu ya madeni ya nyuma, unamfanya mfanyabishara ashindwe kutengeneza fedha. Hivyo, kwa vile hazalishi, maana yake hatalipa kodi mpya, na za nyuma anazodaiwa anashindwa pia kulipa, kwani fedha anakuwa hana.

Akiendelea kuchambua mnyororo wa athari za kufungia biashara, Mwambe anasema kuwa mfanyabishara anaposhindwa kuzalisha, anapunguza wafanyakazi. Hili pia lina athari pana kiuchumi. Mtu anapokosa ajira, maana yake halipi kodi mbalimbali zenye kustahili kulipwa na mwajiliwa pamoja na michango ya mwajiri wake. Kingine mtu asiye na ajira hupoteza uwezo wa kufanya manunuzi, hivyo kudumaza mzunguko wa kifedha.

Mwambe anagusia kuhusu mapato ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kwamba biashara zinapofungwa, umeme huzimwa na kusababisha Tanesco wakose mapato. Alisema tatizo ni kubwa lakini limekuwa likitazamwa kwa juujuu.

Katika video hiyo, Mwambe anatoa wito kwa mamlaka mbalimbali zenye kuhusika na ukusanyaji wa mapato kuwa watu wanaokutwa na changamoto za kimazingira waelezwe ili warekebishe kuliko kufungia biashara.

Anasema kuwa wapo waliofungiwa wakiwa tayari wameshanunua malighafi, matokeo yake zinakwisha muda wake kabla ya kutumika na kupata hasara kubwa. Anaeleza kwamba wengine wanakuwa wamechukua mikopo benki, wanashindwa kurejesha kwa kuwa biashara zao zimefungwa na benki nazo zimechukua fedha za watu zinatakiwa zirudishwe.

Ukimsoma Mwambe ni kuwa anaamini kufungia biashara ni hasara kwa Serikali na mzunguko wa kiuchumi kwa nchi. Ukimsikiliza Lukuvi, yeye anaamini kuna fedha nyingi zitapatikana kwa kufungia biashara watu kuliko kuzungumza na wadaiwa ili watengenezewe mazingira ya kulipa huku wakiendelea kufanya kazi.

Mwambe anasimamia anachokiamini kwamba ukimfungia mfanyabishara asifanye biashara kwa sababu anadaiwa, humfanyi alipe, bali unamsababishia apoteze uwezo wa kulipa kabisa, maana anakuwa haingizi. Lukuvi msimamo wake ni kuwa bila kuwapa msukosuko wadaiwa na kufungia biashara zao, hawatalipa.

Hapa ndipo palipo na mgongano wa lugha. Kwa nini Serikali inashindwa kuwa na msimamo mmoja? Iweje ndani ya Serikali moja, kuwepo na kauli za kupingana?