MTATIRO: CCM ni chama cha ajabu mno!

Kuna wakati unaweza kudhani CCM inaelekea shimoni, inakufa, imepoteza mwelekeo, haitakuwapo tena au imetetereka kweli kweli. Kumbe huo ndiyo wakati ambapo CCM inaibuka chama imara kisicho na mbadala nchini Tanzania.

Nilipokuwa upinzani na nikishiriki ajenda za kujenga upinzani nchini Tanzania, nyakati ambazo viongozi wa upinzani walikutana na kufurahia ni pale iliposikika kuwa CCM inamhoji mwanachama wake mashuhuri au kiongozi mstaafu fulani, au inamhoji kiongozi wa wadhifa fulani.

Hizo ni nyakati ambazo nazikumbuka vizuri, wakati huo nilikuwamo kwa hiyo tulibweteka kwelikweli, tuliamini CCM imefika mwisho. Ilipotokea mathalani, viongozi waandamizi na wakongwe wa CCM wakatoa kauli zenye utata za kukitahadharisha chama hicho, kauli hizo zilibebwa kwa uzito mkubwa na upinzani, na ziligeuka ajenda kubwa za kufurahia anguko la CCM.

Dua la kuku

Ugonjwa huu wa vyama vya upinzani kujifungia na kufurahia viashiria vya uwezekano wa CCM kuanguka, ni ugonjwa mbaya na unavimaliza vyama hivyo. Kila mara zinapotokea tetesi za migawanyiko au mivutano fulani ndani ya CCM, tetesi hizo huaminiwa sana na vyama vya upinzani.

Ni kama zile hadithi za fisi anayemfuatilia binadamu na kusubiri mkono udondoke ajiokotee vya bure. Kasumba na tabia hiyo inavipotezea vyama vya upinzani nchini Tanzania muda mwingi, kuna nyakati havifanyi kazi za kisiasa katika maeneo muhimu kwa kuamini maeneo hayo yana mgogoro mkubwa wa ndani ya CCM na upinzani utautumia wakati wa uchaguzi kushinda eneo hilo.

Imani za namna hiyo mara nyingi kwa uzoefu wangu hazikuzaa matunda, nyakati za uchaguzi zilipofika CCM huungana na kuwa kitu kimoja, na umoja huo huleta ushindi mkubwa wenye kutikisa nchi. Na huo ndiyo wakati ambapo upinzani huduwaa na kujiuliza nini kimetokea? Maana kiuhalisia upinzani uliamini kuwa CCM ingelikufa kwenye eneo hilo la uchaguzi.

Kuijua CCM hadi uingie ndani

Kama ukiishi tu siasa za upinzani huwezi kuijua CCM. Kama ukikaa mahali na kusikiliza hotuba za viongozi wako wa upinzani unaowaamini huwezi kuijua CCM halisi.

Tangu nijiunge CCM nikiri kuwa nimeendelea kukijua chama hiki kikongwe, nimekijua kama chama imara, chenye uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yake ya ndani na chenye visheni kubwa ya uongozi wa nchi kwa miaka mingi ijayo.

Ukiwa ndani ya CCM unagundua maamuzi ya chama kwenye ngazi mbalimbali yanatokea chini kwenye vikao vya mashina, matawi, kata, wilaya, mkoa hadi taifani.

Ajenda zake haziibuki bila mpango, tofauti na nilipokuwa upinzani, ambako ajenda nyingi hutokea kwa viongozi wakuu kwenda chini.

Kwa CCM ajenda, mijadala yake, utekelezaji wake na mengine mengi vinatokea ngazi ya chini vikienda juu. Hali hii inaifanya CCM iendelee kuwa chama cha wananchi walio wengi, kikiaminika kitaifa.

Nyakati za viashiria vya migogoro

Nyakati ambazo CCM huonyesha dalili za kuzongwa na migogoro ya ndani, ndizo nyakati ambazo CCM huibuka ikiwa imara kushinda kipindi cha nyuma. Mathalani, mwaka 2015 Mzee Edward Lowassa na wenzake kadhaa walipoondoka CCM na kujiunga upinzani, dhana iliyojengeka ni kubomoka kwa CCM na kuinuka kwa upinzani.

Mwaka mmoja baadaye tukashuhudia mabadiliko makubwa katika nchi yakiongozwa na mtu aliyeshinda urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, ushindi ambao aliupata katikati ya hali iliyodhaniwa kuwa ni kuharibika kwa hali ya hewa ndani ya CCM.

Miaka mitatu baadaye tumeshuhudia kinyume cha vicheko vya upinzani mwaka 2015. Vicheko hivyo ilikuwa ni raha ya upinzani kuvuna magwiji wakubwa wakubwa wa kisiasa, na CCM kupoteza CCM haikupiga kelele sana zaidi ya kuendelea kujipanga, upinzani ukiamini chama hicho kimemalizika.

Tafakari ni ya lazima

Miaka mitatu baadaye, CCM imevuna magwiji wengi wa kisiasa kutoka upinzani, imevuna viongozi wengi wa upinzani waliokuwa watiifu na walioshikilia nyadhifa kubwa ndani ya upinzani. Huu ni wakati ambako upinzani ulipaswa kukaa chini na kutafakari kwa nini miaka mitatu baada ya mavuno yake, mavuno yanaondoka, mimea inaondoka na mashamba yanaondoka?

Badala yake viongozi wa upinzani wanaendelea na mazoea yale yale ya kuamini kuwa haya yanayotokea ni njama tu. Jambo kubwa la kujifunza siku zote na hata kwa watu kama mimi waliowahi kupitia kwenye siasa za upinzani wanaweza kulishuhudia ni kwamba, CCM ni chama cha ajabu mno, kimejijenga kwa ndani, kina mifumo imara na kinaaminika sana kwa wananchi.

Kupambana na chama cha aina hii kunahitaji viongozi wa upinzani wakweli, wasio na mipango mingi binafsi ndani ya siasa kuzidi mipango ya vyama vyao, wenye visheni ya kutotegemea kuharibika kwa hali ya hewa ndani ya CCM kama faida ya kukua kwa upinzani na wenye ajenda ya thabiti ya kukuza upinzani bila kuweka maslahi binafsi mbele, maana kama nilivyosema kila unapoona CCM ina fukuto la ndani, hapo ndiyo inajijengea uimara mkubwa kupitia fukuto hilo.

CCM ni kubwa kuliko kila mtu

Walioko ndani ya CCM muda mrefu wameliishi jambo hili, nadhani tangu enzi za Mwalimu Nyerere. Ndani ya CCM, chama ni kikubwa kuliko kila mtu. Chama ni kikubwa kuliko mwenyekiti wa chama, katibu mkuu na kila kitu. Wanachama ni watiifu sana kwa chama, na wanachama wanajitolea kwa hali na mali kukijenga chama chao.

Uzoefu wangu ndani ya upinzani unaonyesha kuwa kwa vyovyote vile lazima kwenye upinzani baadhi ya viongozi wa chama wanakuwa na nguvu kubwa kushinda chama, na chama kinawatii viongozi hao. Yaani, wakiamua kuondoka na chama mfukoni wanaondoka nacho. Na mifano halisi iko mingi sana unaweza kukiangalia chama changu cha zamani cha CUF, tizama kuwa Maalim Seif tangu aondoke chama hicho kimejiporomoshea robo tatu ya nguvu zake. Lipumba naye atakapohitimisha safari yake ya siasa mwaka huu 2020 hasa baada ya uchaguzi mkuu, chama hicho kitakufa.

Unaweza kuitazama Chadema tangu Dk Slaa aondoke, chama hakijapata Katibu Mkuu mwenye uwezo wa kushika nafasi yake na huenda hatatokea baada ya miaka 30 ijayo.