Maendeleo na uwajibikaji, ushirikishaji na uwezeshaji

Ni wazi kwamba nchi za Afrika haziwezi kupata maendeleo ya kweli bila huduma inayoaminika ya kusambaza maji safi na salama. Karibia wabunge wote wa Tanzania wanapigia kelele tatizo la maji kwenye majimbo yao.

Yapo majimbo ambayo ili ufanikiwe kuchaguliwa ubunge au udumu kwenye kiti hicho ni lazima ufanikishe kwa kiasi kikubwa usambazaji wa maji. Utafiti juu ya usambazaji wa maji vijijini uliofanyika hivi karibuni kwenye nchi 13 zinazoendelea, umeonyesha kwamba tatizo hilo ni kubwa na matatizo yanayokwamisha miradi ya maji kati nchi hizi yanafanana.

Serikali za nchi kushindwa kupeleka madaraka kwa wananchi, miradi ya maji hupangwa kutoka juu na kwenda chini, badala ya kuanzia chini kwenda juu; majukumu ya wadau kwenye miradi hii kutowekwa wazi, serikali za mitaa kutokuwa na uwezo wa kuendesha miradi ya maji na kukosekana kwa sera nzuri za maji.

Vilevile kuna kukosekana kwa utekelezaji, miradi mingi hutegemea kwa kiasi kikubwa misaada kutoka nje na wananchi hawana uwezo wa kuendesha miradi hiyo kwa ufanisi.

Wakati Tanzania ilikuwa ikikazania kwamba asilimia 57 ya Watanzania wa vijijini wanapata maji safi na salama, utafiti huo unaonyesha kwamba wanaopata maji safi na salama hawazidi asilimia 40.

Malengo ya milenia yalikuwa ni kwamba kufikia 2015, asilimia 65 ya watu wa vijijini wawe wamepata maji safi na salama na asilimia 90 mijini wawe nao wamepata maji safi na salama, lengo hili halikufikiwa.

Rwanda, kwa upande wake imefanikiwa kutunga sheria ya kuvuna maji ya mvua, na hii imewasaidia kupiga hatua kubwa katika zoezi zima la kusambaza maji safi na salama.

Huu ni mfano mzuri uwajibikaji, ushirikishwaji na uwezeshwaji. Kila mtu anawajibika kuyavuna maji, serikali imewashirikisha wananchi kwa kuitunga sheria ya kuvuna maji ya mvua na inawawezesha katika njia za kuyavuna.

Kwa kifupi changamoto kubwa inayoikumba miradi ya maji hapa Tanzania ni masuala haya matatu – uwajibikaji, ushirikishaji na uwezeshaji. Hata hivyo, shuhuda zilizopo ni kwamba miradi mingi ya maji vijijini imekufa au imekwama kabisa. Miundombinu yake imechakaa na hakuna mpango wa kuikarabati, vyanzo vya maji vimekauka kwa sababu watu hawatunzi mazingira, sehemu ambapo maji yanasukumwa na mashine zinazotumia mafuta, kuna tatizo la kupata mafuta hayo na kama ni umeme kuna tatizo la kulipa bili ya umeme.

Na wakati mwingine wataalamu wa maji kutoka wilayani hawana magari au mafuta ya kufikisha kwenye vyanzo vya maji ili kutoa huduma.

Kinachojitokeza wazi ni kwamba bila ushirikiano wa serikali, mashirika ya misaada, wadau wote wa maji na wananchi itakuwa vigumu kutengeneza miradi endelevu ya maji.

Endapo uwajibikaji, ushirikishaji na uwezeshaji ukifanya kazi kwa pamoja na kuweka wazi, umilikaji wa miradi hii ya maji itakuwa endelevu, kinyume na hapo ni kutwangia maji kwenye kinu.

Kama serikali ingewajibika ipasavyo na kutambua kwamba wajibu wake si sera na kuisimamia miradi ya maji, bali ni kuhakikisha inawashirikisha na kuwawezesha wananchi na kuwajengea uwezo kuiendesha na kuisimamia miradi ya maji, matokeo yangekuwa mazuri.