Maeneo mapya ya kupigia siasa yanavyoibuka nchini

Wednesday May 15 2019

 

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Sasa hakuna ubishi kuwa zuio la Rais John Magufuli la mikutano ya hadhara na maandamano kwa vyama vya siasa imeibua maeneo mapya ya ufanyaji wa shughuli za siasa nchini.

Ni miaka mitatu sasa tangu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ilipozuiliwa na Rais Magufuli Juni 24, 2016 akiwa Ikulu, Dar es Salaam na kuruhusu tu mikutano ya madiwani na wabunge wakiwa majimboni na kata zao.

“Ni matumaini yangu Watanzania wanataka maendeleo. Wanataka kuona kero zao mbalimbali zinatatuliwa. Yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi kwa miaka mitano

“Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kuyatekeleza kama tumeyatekeleza au hatukuyatekeleza.

“Ushindani wa siasa sasa hivi ni kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi,” alisisitiza Rais Magufuli na kutaka wabunge wafanye siasa kwenye majimbo yao na madiwani kwenye kata zao.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa vyama vya siasa kupitia kipindi kigumu katika ufanyaji wa siasa nchini Tanzania. Ilifika hatua hata mikutano ya ndani ikawa inazuiliwa kwa sababu mbalimbali ambazo Jeshi la Polisi husema za kiintelijensia.

Hata hivyo, ukizuia mkondo wake maji lazima yatafute njia nyingine ya kupita. Hivyo ndivyo inavyotokea sasa, zimeibuka fursa nyingine za ufanyaji wa siasa katika maeneo manne yasiyo rasmi.

Misibani, makanisani

Kama ilivyokuwa Kenya enzi za Moi wakati wapinzani hawapati fursa rasmi za kisiasa, misiba na makanisa yalitumika kupenyeza ujumbe wa kisiasa.

Hata hapa hali hiyo imekwishaanza. Misiba na makanisa ni mahali wanasiasa wakipata fursa ya kuzungumza huyatumia kutema nyongo zao na kupenyeza ujumbe wa kisiasa.

Mfano mzuri ni katika msiba wa Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Mei 8, 2019 wakati wa kuaga mwili wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipopata fursa ya kuzungumza alimtupia ‘dongo’ Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kwa kile alichosema anajua kuwa Mengi alikuwa anamdai, hivyo alipe deni hilo.

Siku iliyofuata wakati wa ibada ya mazishi yake iliyofanyika Usharika wa Moshi mjini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambapo ibada hiyo ilitumika kutema nyongo za kisiasa.

Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alitumia fursa hiyo kukemea “kauli za ukabila zinazowagawa Watanzania”.

Kauli hiyo ya ubaguzi inadaiwa kutolewa na Makonda aliyemwelezea Mengi kama mchaga pekee aliyeweza kutoa fedha zake kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Tusianze kubaguana kwa itikadi, tusibaguane kwa imani wala tusibaguane kwa makabila yetu. Tupendane kama Watanzania. Kauli za kuambiana kuna makabila hayawezi kuwatetea walemavu si za kweli”.

Kauli hii ilimgusa Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akatumia salamu zake za rambirambi kumwombea msamaha Makonda, akisema upo umuhimu wa kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora.

“Kazi ya kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora hatujaifanya. Na kwa sababu hatujaifanya tunaanza kuvuna matunda ya kutowaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora watiifu, wa kweli, wanyenyekevu na wenye heshima,” alisema Dk Bashiru.

“Naomba nitumie fursa hii kumwombea msamaha kijana wangu Paul Makonda. Mimi namfahamu na hii ni mara ya pili nimemsema hadharani. Mara ya kwanza nilimsema Simiyu….,”aliongeza kusema.

Ufanyaji wa siasa makanisani na misibani, ni staili mpya inayotumiwa na wanasiasa, na mara nyingi hali hii inajitokeza pale ambapo aliyekufa ni mwanachama wa chama fulani cha siasa.

Mitandao ya kijamii

Eneo jingine ambalo linatumika kufanya siasa baada ya zuio hilo la mikutano ambalo linasimamiwa kikamilifu na Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama, ni mitandao ya kijamii.

Kumekuwa na mijadala mikali ya kisiasa katika mitandao ya kijamii hususan kwenye makundi ya Whatsapp na mitandao kama Jamii Forums, Twitter, Instagram na Facebook kila linapojitokeza tukio la kisiasa.

Si viongozi wa kisiasa pekee, wabunge, madiwani, wafuasi na wasio wafuasi wa vyama vya siasa wote wanatumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe na maoni yao hasa linapoibuka suala la kitaifa.

Mathalan, tukio la hivi karibuni kabisa la kutekwa Mdude Nyagali maarufu kwa jina la Mdude Chadema, kuliibuka mijadala mikali na yenye hisia kali juu ya tukio hilo la utekaji.

Hata baada ya Bunge kuzuiwa kuonekana moja kwa moja, baadhi ya wabunge wamekuwa wakirekodi michango yao na kuisambaza katika mitandao ya kijamii ambako hupata wasikilizaji au watazamaji wengi zaidi.

Wadau wazungumza

Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema alisema hakuna kitu kigumu kushindana nacho kama teknolojia ya habari na kueleza kuwa waliomshauri Rais kuzuia mikutano, hawakupima vizuri matokeo yake.

“Rais alipopiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa upinzani tulikuwa hatujajipanga vizuri. Lakini alipopiga marufuku mikutano ndio upinzani umejipanga kuliko 2015,”alisema Lema.

Lema alisema mbali na teknolojia, pia huwezi kushindana na uwezo wa kujenga hoja ambao kwa kiwango kikubwa uko upinzani.

Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS) tawi la Kilimanjaro, David Shillatu alisema pamoja na kuibuka njia nyingine, kuzuia mikutano ya kisiasa hakuleti afya na kusisitiza haki hiyo ipo kikatiba na kisheria.

Shillatu alisema kinachojitokeza hivi sasa, mijadala mikali zaidi iko kwenye mitandao ya kijamii kuliko hata ilivyokuwa kwenye mikutano ya hadhara na mingine imekuwa ni hasi dhidi ya Serikali.

Advertisement