Manispaa ionyeshe mfano Mwezi wa Ramadhani

Kuanzia wiki iliyopita Waislamu walianza kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, moja ya nguzo tano za dini yao.

Wakati wa saumu hutakiwa kujiepusha na mengi. Hii ni pamoja na kula, kunywa chochote kile, kuvuta sigara na kusema uongo ili funga yao katika mwezi huu itimie.

Saumu kwa Waislamu wa Tanzania huchukua si zaidi ya saa 14 kwa vile huanza karibu saa mbili kabla ya jua kuchomoza na kufungua jua linapotua.

Lakini wapo wenzao katika nchi nyingine ambapo usiku ni mkubwa hufunga kwa saa 20 au zaidi kidogo.

Katika mwezi huu Zanzibar huwa na sheria na taratibu ambazo Waislamu na wasiokuwa Waislamu, wawe wenyeji au wageni hutakiwa kuzifuata na wanaozikiuka hupata adhabu ya kifungo.

Kwa mfano, mtu mzimu na mwenye akili timamu (bila ya kujali umri wake) akila, kunywa au kuvuta sigara mchana hupewa kifungo cha mwaka mmoja.

Kama umekamatwa ukila siku ya tatu ya Ramadhani utakwenda jela hadi siku ya tatu ya Ramadhani ya mwakani kwa vile umeonyesha jeuri na kuchezea hisia za Waislamu.

Mara chache huwepo adhabu ya faini kwakosa hili. Bei za vyakula katika mwezi huu mtukufu zamani zilikuwa poa, tafauti na hali ilivyo katika miaka ya karibuni.

Hii ilitokana na serikali na taasisi zake kufuta au kupunguza kodi na ada wanazotozwa wafanyabiashara, hasa katika masoko wakati wa mwezi huu. Kwa mfano, mtu alikuwa hahitaji leseni ya biashara na hatozwi ada zozote akifika sokoni.

Watu walijifanyia biashara za vyakula hata nje ya baraza za nyumba zao na hawakubughudhiwa kwa kutozwa ada hii au ile wala mchango wa usafi wa mazingira.

Lakini ukimalizika tu mwezi wa Ramadhani mambo hurudi kama kawaida.

Hata nauli za usafiri za kwenda na kurudi mashambani zilikuwa chini kutokana na bei ya mafuta kupunguzwa katika mwezi huu wa

neema na rehema.

Lakini hali leo ni tofauti. Wafanyabiashara wanakamuliwa kila pembe na wanatozwa malipo katika masoko kama kawaida na mara nyingine kuongezewa viwango.

Mbali ya leseni ya biashara upo msururu wa malipo, kama usafi wa mazingira. Hii inatokana na manispaa kutegemea ushuru na leseni kuwa kipato chake kikubwa.

Kwa mfano siku moja tu kabla ya mwezi wa Ramadhani kupiga hodi jana bei ya petroli na dizeli Zanzibar ilipanda kama vile ulikuwa unangojewa mwezi huu ufike wenye magari wachapwe kiboko.

Bila ya shaka unapopandisha bei ya petroli au dizeli malipo ya kupakia vyakula kutoka vijijini yatapanda kufidia ongezeko la gharama.

Manispaa imeona huu ndio mwezi wa kuchuma. Kabla ya jua kutoka, wafanyakazi wake ambao zamani walianza kutoza ada za kuegesha magari saa mbili asubuhi sasa wanaanza mara tu jua lilipotoka.

Ada za kuegesha ni kubwa kuliko maeneo mengi na zinatozwa hata katika vichochoro.

Sasa vipi mtu anaweza unakuwa na ujabari wa kumtaka mfanya biashara atoe unafuu kwa wateja wakati wewe unayesema hivyo unapandishagharama za kuendesha biashara.

Sijawahi kusikia mtu mwenye akili timamu kuuza bidhaa kwa bei ya chini ya gharama alizolipia. Akifanya hivyo huwa anatoa sadaka na si kufanya biashara.

Naelewa hali ya siku hizi ni tofauti na zamani si kisiasa tu bali hata kiuchumi si kwa Zanzibar tu bali hata nchi nyengine. Lakini msururu wa kodi Zanzibar ni kiboko.

Ni vizuri kwa serikali kujipiga moyo konde kwa kutoa unafuu wa za ada za leseni kwa wafanya biashara katika mwezi huu ili hiyo nafuu ya bei tunayoizungumzia ipatikane.

Hata mtindo wa kupandisha bei ya petroli kila mara kwa kiwango kikubwa na kupunguza baadaye kwa kiwango kidogo ungesubiri imalizike Ramadhani.

Vilevile iregeze mkanda kwa msururu wa malipo katika viwanja vya kusherehekea Idd el Fitr pale funga ya Ramadhani inapomalizika Huu ni mwezi wa rehma na watu hutarajiwa kusaidiana. Tuonyeshe mfano kwa vitendo na sio maneno.