Marais wastaafu wafarakana vikali hadharani Botswana

Sunday June 16 2019

 

By Salva Rweyemamu

Rais mstaafu wa Botswana, Mzee Festus Mogae, mwanzoni mwa mwaka huu ajitenga waziwazi kutoka kwa mtu ambaye alimteua kutoka katika Jeshi la nchi hiyo, ili aweze kumrithi katika kiti cha urais wa nchi hiyo yenye utulivu mkubwa wa kiuchumi na demokrasia ya kujivunia katika Afrika.

Alimweleza mrithi wake huyo, Seretse Khama Ian Khama kama binadamu mchonganishi ambaye hasikilizi la mtu, isipokuwa lile analotaka yeye lifanyike, na kwa mara ya kwanza Mzee Mogae alikiri kuwa alikuwa na wakati mgumu kumthibiti makamu wake huyo wa Rais wakati wakiwa madarakani pamoja.

Katika mahojiano maalum na gazeti la The Voice, Februari, mwaka huu, Mzee Mogae alikiri waziwazi kuwa mrithi wake huyo alimkatisha tamaa, na kumwangusha, na kuongeza kuwa anasikitika kabisa kwamba hata alifanya uamuzi wa kumteua kuwa Makamu wa Rais, nafasi ambayo hatimaye ilimwezesha Ian Khama kupanda ngazi na kuwa Rais, baada ya kustaafu kwa Mzee Mogae.

Mogae alikiri kuwa hakupata kuwa na uhusiano wowote binafsi wa karibu na Ian Khama, hata kama alikuwa amefanya kazi kwa karibu sana na baba yake mzazi, hayati Seretse Khama, mwanzilishi wa taifa la Botswana ambalo lilipata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Wakati huo nchi hiyo ikijulikana kama Bechuanaland.

Mzee Mogae ambaye sasa ana umri wa miaka 80, aliamini kuwa tunda lisingedondoka kutoka mtini, lakini kwa mshangao mkubwa, tabia ya Ian Khama ilithibitika kuwa tofauti kabisa na ile ya baba yake hayati Tseretse Khama, Rais wa kwanza wa Botswana na Chifu Mkuu wa kabila la Bamangwato, kabila kubwa zaidi katika nchi hiyo.

“Nilidhani kijana huyo alikuwa sawa na baba yake, lakini kwa mshangao mkubwa nikagundua kuwa alikuwa na tabia tofauti kabisa. Baba yake alikuwa ishara ya umoja wa taifa la Botswana. Wakati Ian Khama alipokuwa makamu wangu alikuwa ni mtu mchonganishi, mwenye tabia ya kugawa watu badala ya kuwa ishara ya kuwaunganisha. Baba yake mzazi alikuwa mzee tofauti kabisa, alikuwa mjenga umoja wa watu,” alidai Mzee Mogae.

Advertisement

Mzee Festus Gontebanye Mogae, mchumi ambaye alipata kuwa mwajiriwa wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Gavana wa Benki Kuu ya Botswana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, kabla ya kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, anatoka eneo moja na kabila moja na akina Khama, sehemu ya Serowe, mashariki kati mwa Botswana.

Kwa kuangalia nyuma sasa, Mzee Mogae aliliambia Gazeti la The Voice, kuwa alikatishwa tamaa sana na tabia na desturi ya mrithi wake, akimwelezea kama kiongozi aliyeendekeza taifa kupambana lenyewe kwa lenyewe, na kujenga mipasuko.

Mwaka 1997, wakati wa kilele cha mapambano ya kuwania madaraka ndani ya chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) katika kipindi ambacho makundi mawili yenye nguvu – Kundi A na kundi la Barataphati – yalipokuwa yanapambana kuwania madaraka ya nani awe kinara wa madaraka katika Botswana, chama hicho tawala kilimwomba Lawrence Schlemmer, mtaalamu wa sayansi ya siasa kutoka Afrika Kusini, kusaidia kutuliza mawimbi makali ambayo yalikuwa yanatishia kukizamisha BDP, ambacho kilikuwa kimeshikilia madaraka ya kuongoza Botswana kwa miongo mitatu, bila madaraka yake kutishiwa na chama kingine.

Uchambuzi wa Schlemmer ilikuwa rahisi na wazi kabisa. Mapambano ya kuwania madaraka kati ya makundi hayo mawili yangekitosa chama hicho kupoteza madaraka katika uchaguzi mkuu uliokuwa unakuja wa mwaka 1998, kwa sababu hakuna kundi mojawapo lilikuwa tayari kuliachia jingine kukamata madaraka ya kuongoza dola.

Ili kumaliza mgawanyiko huo, Schlemmer, ambaye baadaye alikuja kuitwa “mchawi wa kisiasa”, alipendekeza na kushauri BDP kumteua Khama kuwa makamu wa rais kwa sababu alionekana kukubalika kama mtu ambaye hakulalia upande wowote na angekubalika kwa pande zote mbili.

Aidha Khama, alionekana kama angeweza kuyaunganisha makundi hayo mawili hasimu. Isitoshe, wakati huo Khama alikuwa Kamanda wa Jeshi la Botswana, aliyekuwa na ufuasi na ushawishi mkubwa, na zaidi ya yote, alikuwa mtoto wa rais mwanzilishi wa taifa la Botswana.

Baada ya kujiunga na siasa mwaka 1998, Khama kila mara alikuwa anakuwambusha wananchi wa Botswana kuwa yeye binafsi aliichukia siasa, na kuwa alikuwa amelazimishwa kuingia katika shughuli hiyo tu kwa nia ya kutumikia nchi yake.

Na baada tu ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais, wachunguzi wa masuala ya siasa katika Botswana walikuwa wanaviambia vyombo vya habari pembeni kuwa wakati Mogae alionekana kuwa Rais wa nchi, lakini mwenye madaraka hasa ya kuongoza Botswana alikuwa Khama.

Ishara ya kwanza ya tabia halisi ya Khama ilijitokeza wakati vyama vya upinzani vilipolalamikia tabia yake ya kuendelea kutumia na kuendesha mwenyewe ndege za kijeshi za Jeshi la nchi hiyo kwa shughuli zake na za kisiasa. Kwa mafunzo na utaalam, Khama alikuwa rubani wa ndege za kijeshi.

Wakati suala hili lilipofikishwa kwa Mdhibiti wa Tabia ya Viongozi wa nchi hiyo aliamua kuwa yalikuwa ni makosa kwa Khama kuendelea kutumia na kuendesha ndege za Jeshi la nchi hiyo la Botswana Defence Forces (BDF), ambako Khama alianzia kazi kama rubani za ndege za jeshi.

Hata hivyo, Rais Mogae aliingia kati suala hili na kutoa ruhusa kwa Khama kuendelea kutumia na kuendesha ndege hizo za jeshi kwa shughuli zake.

Mbele ya umma, kati ya miaka ya 1998 na 2008, marais hao wa zamani walionyesha uhusiano wa karibu wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa karibu. Wabotswana hawakuwa na habari kuwa nyuma ya pazia, alikuwa ni rais ambaye alikuwa amezidiwa nguvu kabisa na makamu wake.

Sasa baada ya wote wawili kutoka madarakani, Mzee Mogae amekuwa mkosoaji mkubwa na wa waziwazi wa mtu ambaye alimlazimisha kwa wananchi wa Botswana kuwa kiongozi wao: Rais Mogae alifikia hata mahali pa kutishia kuvunja Bunge la nchi hiyo, kama lingekataa kumpitisha mteule wake Ian Khama kuwa makamu wake wa rais.

“Nilimteua Ian kwa sababu alikuwa anakubalika na pande zote mbili zilizokuwa zinakinzana. Sasa nasikitika kutoka ndani ya moyo wangu kuwa nilifanya kosa la kumteua mtu huyu. Khama alifanya kinyume kabisa na lile nililotarajia atafanya wakati namteua,” Mzee Mogae aliliambia Gazeti la The Voice katika moja ya mahojiano ambako alikuwa muwazi kwa namna isiyokuwa ya kawaida.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Mogae kumsema Khama hadharani. Mwaka 2014, Mogae, mshindi wa Tuzo ya Mo Ibrahim Prize for Achievement in Leadership inayotolewa kwa viongozi wakuu wastaafu wa Afrika waliochangia kupanua demokrasia, alisema kuwa demokrasia katika Botswana, ilikuwa imerudi nyuma chini ya uongozi wa Khama.

Baadaye, Mogae alifuatishia kauli yake hiyo kwa kumshutumu vikali Khama, akisema kuwa alikuwa ni mtawala badala ya kuwa kiongozi na Rais wa nchi, na akaongeza kuwa Khama alikuwa mtu asiyekuwa na uwezo (incompetent). Hata hivyo, siku chache baadaye. Mogae alifuta kauli yake hiyo na kudai kuwa alikuwa amekaririwa vibaya na vyombo vya habari.

Wakati akiwa Rais, kwa mfano. Khama aliwasema na kuwapuuza hadharani watangulizi wake, Rais Sir Quett Katumile Masire na Rais Mogae mwenyewe, akiwakemea kukoma kabisa kumwingilia katika utawala wake na maamuzi yake, kwa kutoa ushauri ambao yeye alikuwa hajauomba kuhusu namna ya kuendesha nchi hiyo.

Hii ilikuwa baada ya marais hao wa zamani kujaribu kusuluhisha na kumaliza mgomo wa kitaifa wa wafanyakazi uliokuwa umeibuka mwaka 2011, baada ya Khama kushikilia msimamo mkali dhidi ya madai ya vyama vya wafanyakazi kuhusu maslahi ya wanachama wao. Wakati wa mgomo huo, Rais wa sasa wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, ambaye alimrithi Khama, alimuunga mkono rais na bosi wake.

Katika mabadiliko ya msimamo yasiyokuwa ya kushangaza kwa wanasiasa, Mogae sasa ameelekeza nguvu zake kumwunga mkono Masisi katika mvutano wake na mtangulizi wake, Khama. Mogae aliliambia Gazeti la The Voice kuwa Khama alikuwa anamfanyia Masisi ambacho yeye Khama alimfanyia yeye mwenyewe Mogae wakati alipokuwa Rais wa nchi hiyo.

“Kwa sababu nilikuwa namwamini na nilimwambia siri zangu nyingi za uongozi, nilijiweka katika hali ambako alianza kutoa madai na masharti mengi na yasiyokuwa ya busara, lakini nilijizuia kumfukuza kazi kwa sababu hatua hiyo ingechafua zaidi hali ya kisiasa nchini ambayo tulikuwa tunajaribu kuilea na kuibembeleza ili itulie,” Mogae alikiri kwa mara ya kwanza tokea atokea madarakani.

“Kwa mfano, muda siyo mrefu baada ya kuteuliwa kuwa makamu wa rais, alitaka kwenda likizo isiyokuwa na malipo, tena mara moja bila kukawia, jambo ambalo lilikuwa la kushangaza kabisa, lakini nilimkubalia. Baadaye, yeye mwenyewe alirudi na kusema kuwa alikuwa tayari kurejea kazini, jambo ambalo alilifanya mwenyewe. Sikumwomba wala kumtaka arejea kazini,” alisema Mogae kuthibitisha kile ambacho katika Botswana kimekuwa historia ya pekee kwa makamu wa rais wa nchi hiyo kudai kwenda likizo ya masomo, muda siyo mrefu baada ya kuwa ameteuliwa kushika nafasi hiyo kubwa ya uongozi.

Katika kukiri kuwa vyombo vya habari vilikuwa vinaandika ukweli wakati vilipokuwa vinasema kuwa akiwa makamu wa rais chini ya Mogae, Khama alifanya alivyotaka, Mzee Mogae katika mahojiano hayo alisema kuwa Khama alikuwa anafanya kila aina ya vituko na vitendo visivyokuwa vya kawaida dhidi ya urais na uongozi wake.

“Lakini nilikuwa nampuuza na kuelekeza nguvu zangu katika uongozi wa nchi. Anachomfanyika Masisi sasa ndicho kile kile ambacho alikuwa ananifanyia mimi, ambayo n tabia ya uchonganishi na kugawa watu,” alisema Mzee Mogae.

Katika kauli nyingine mpya na isiyokuwa ya kawaida, Mzee Mogae aliliambia Gazeti la The Voice kuwa wafuasi wa Khama walikuwa wamemwekea shinikizo, na hata kumwamuru Masisi wakati wa Mkutano Mkuu wa BDP mwaka 2017 akubali na kuahidi kumteua Tshekedi Khama kama makamu wake wa rais, baada ya yeye Masisi kuwa amekuwa rais mwaka 2018. Tshekedi Khama ni mdogo wake, toka nitoke, Ian Khama ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Serowe Mashariki na aliyekuwa waziri chini ya kaka yake na baadaye chini ya Masisi.

Kwa mujibu wa Mzee Mogae, wafuasi wa Khama walikuwa wamefikia hatua, isiyokuwa ya kawaida, ya kumwandikia hata hotuba Masisi ambayo angeitoa katika mkutano huo ambako angejifunga kwa kutangaza kuwa angemteua Khama mdogo, kuwa makamu wake baada ya yeye kupanda na kuwa Rais wa Botswana.Masisi alikataa shinikizo hilo la wafuasi wa Ian Khama.

Kauli hiyo ya Mogae inafanana na ile ambayo Masisi mwenyewe alipata kuitoa katika mahojiano yake na Gazeti la Sunday Standard mwaka jana, ambako alitoboa kuwa mvutano na msuguano kati yake na mtangulizi wake, Ian Khama, ulikuwa unatokana na kukataa kwake kukubali kumteua mdogo wake - Tshekedi Khama kuwa makamu wa rais.

Khama, kwa upande wake, anadai kuwa hakupata kamwe kumwomba wala kumshinikiza Masisi kumteua mdogo wake kuwa makamu wa rais. Badala yake, Khama anadai kuwa Masisi mwenyewe, kwa uamuzi na mapenzi yake, alikuwa amejitolea kumteua Khama mdogo kuwa makamu wake, kama ishara ya shukurani kwa hatua ya Tshekedi kutowania uenyekiti wa BDP dhidi ya Masisi, na pia kama shukurani kwa Ian Khama mwenyewe, kwa kupambana kufa na kupona, kuhakikisha kuwa Masisi anakuwa makamu wa rais, na baadaya Rais wa Botswana.

Zaidi ya ilivyokuwa kwa matukio ya mwaka 1997, sasa chama tawala cha BDP kimemeguka kufuatia hatua ya Ian Khama kujitoa katika chama hicho na hakuna mwenye hakika ya kujua kitatokea nini katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu nchini Botswana.

Lakini hata kabla ya Khama kujitoa katika BDP, tayari alikuwa anashutumiwa kwa kumhujumu Rais Masisi kwa namna nyingine ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na kundi la “New Jerusalem” linalopinga uongozi wa Masisi wa chama tawala cha BDP. Khama na wafuasi wake, walitaka kupiga kura ya kumzuia asiteuliwe kuwa mgombea rais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Hata hivyo, njama hiyo ya Ian Khama na wenzake ilishindikana baada ya Rais Masisi kushinda katika mchuano wa uteuzi mwei Aprili mwaka huu.

Katika njama zao hizo, Ian Khama alikuwa amefanikiwa kumshawishi rafiki yake wa karibu na wa miaka mingi, mwanamama Pelonomi Venson Moitoi, kusimama dhidi ya Masisi kuwania uteuzi wa nani awe mgombea wa BDP.

Mara baada ya kutangaza nia yake hiyo ya kutoa changamoto kwa bosi wake, Rais Masisi, katika kinyanganyiro hicho cha kuteua mgombea Urais, Rais Masisi alimfukuza kazi Venson-Moitoi kutoka nafasi ya uwaziri wa mambo ya nje ambayo alikuwa ameishikilia kwa muda mrefu chini ya Ian Khama.

Dhahiri mpasuko huo ni mkubwa zaidi kuliko ule wa mwaka 2009 wakati baadhi ya wanachama wake walipokihama chama hicho kwenda kuanzisha Chama cha Botswana Movement for Democracy baada ya Ian Khama kumsimamisha kazi Gomolemo Motswaledi, ambaye alikuwa amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tawala.Sasa imekuwa zamu ya Ian Khama mwenyewe kuondoka katika chama hicho.

Makala hii imetafsiriwa kutoka mahojiano kati ya Rais Mstaafu Festus Mogae na Gazeti la The Voice la Botswana ambalo lilichapisha mahojiano kamili na kiongozi huyo ambaye alikuwa Rais wa Tatu wa nchi hiyo.

Advertisement