Meja Risasi asimulia makundi yanavyoitafuna CCM Dodoma

Makundi na ukabila ni mambo yanayotajwa kuzifanya siasa za Wilaya ya Dodoma ndani ya CCM kuwa ngumu kwa kuwa zimeota mizizi tangu miaka ya nyuma.

Viongozi wengi wanaopata madaraka ndani ya CCM wilayani Dodoma hutumia turufu ya kumaliza makundi lakini waingiapo hujikuta wanamaliza muda wao huku yakiendelea kuwapo kama ilivyo awali.

Baadhi ya wakongwe wanataja kuwa mgawanyiko kwa wanaCCM ulianza mwaka 1975 wakati wanasiasa nguli kwa wakati huo walipokuwa wakigombea Jimbo la Dodoma, ingawa maneno hayo hayajawahi kuthibitishwa.

Hivi karibuni wanaCCM wa Dodoma walifanya uchaguzi na kumpata mwenyekiti mpya, Meja Mstaafu Johnick Risasi ambaye kama walivyokuwa watangulizi wake alieleza kwa mapana namna alivyojiandaa kumaliza makambi na makundi ya wanasiasa.

Mwenyekiti huyu alitoa kauli hiyo mbele ya wanaCCM wakati akiomba kura, lakini pia baada ya kuchaguliwa wakati akitoa shukurani kwa wapiga kura alirejea kauli hiyo ya kuvunja makundi kwa maelezo kuwa yanakibomoa chama.

Meja Risasi aliingia katika uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa wilaya hiyo, Robert Muwinje kuondolewa kwa madai ya kukiuka kanuni na taratibu za chama.

Katika mahojiano ya hivi karibu ofisini kwake, Meja Risasi alisema kauli ya kuvunja makundi haikuwa ya jukwaani bali ni uamuzi na utashi wake wa moja kwa moja kushughulikia jambo hilo ambalo kwake limekuwa dondandugu linalohitaji tiba sahihi ili CCM ipone.

Risasi ambaye ni diwani wa zamani wa Kikuyu Kaskazini, aliwashinda aliyekuwa mbunge Dk David Malole na Vanessa Frank katika uchaguzi uliojaa vibweka na mikwara mingi huku Malole akipinga matokeo kuwa aliyeshinda alikuwa akisaidiwa na viongozi wa CCM na mbunge wa jimbo.

Sehemu ya mahojiano ni kama ifuatavyo.

Swali : Je, unajua kuhusu makundi?

Jibu: Hayo nayajua, tena ni makubwa ambayo nikiangalia kwa kijicho pembe ila sitakitendea haki chama changu, naweza nisifikie malengo niliyojiwekea kwa wakati lakini nataka watu waamini kuwa nitapambana kuhakikisha yanakuwa historia kwa wilaya ya Dodoma.

Mbali na makundi, lakini rushwa imekithiri ndani ya CCM Dodoma nyakati za uchaguzi hali inayosababisha baadhi ya maeneo kuendelea kupata viongozi wabovu.

Umetaja makundi hapa kuna vitu vikubwa viwili kama umeona hilo lazima uone na suala la rushwa ambayo kila mahali inatajwa.

Ni kweli ukabila na rushwa vipo lakini sijui kwa nini vimeota mizizi Dodoma Mjini, nitakesha usiku na mchana ili nihakikishe chama changu kinajisafisha.

Kila jambo siwezi kulifanya pekee yangu bali ninalo jeshi kubwa likianzia na mabalozi wa nyumba kumi.

Siwezi kuangalia wakati viongozi wabovu wakiingia madarakani kwa kutumia fedha na kupitia makundi ambayo mwisho wa siku yataigawa CCM, hivyo nitakuwa mkali katika baadhi ya maeneo na mwenye kufanya uamuzi mgumu pale inapobidi. Naamini viongozi wakubwa ni mabalozi, wajumbe wa mashina, matawi, kata ndipo ifike katika ngazi ya wilaya. Naamini sasa timu ya kamati ya siasa iko vizuri na imesheheni watu wenye kujituma na wabunifu.

Swali: Kampeni zako zilitajwa kuwa na utatu, je ni upi

Jibu : Moja ilikuwa ni kuondosha rushwa na uonevu, nilitaka na bado ninataka kuona mtu anayegombea nafasi yoyote katika siasa asigeuzwe kuwa ‘ATM’ (mashine ya kutolea fedha benki) hiyo ndiyo sehemu ya kwanza.

Lakini pili, kuhakikisha nawapa nafasi walioko madarakani kama mbunge na madiwani waweze kutimiza ndoto zao za kuwatumia wapiga kura, sipendi kuona watu wanakatisha mitaani kutaka nafasi wakati wenzao bado wako madarakani.

Na mwisho katika utatu wangu, nalenga kuingiza wanachama wengi zaidi ambao utakuwa mtaji mkubwa kwa CCM katika eneo langu, lakini nitaanza kupokea maoni kwenye kata zao na wilaya wanadhani nani anafaa kuomba ili tumshawishi achukue fomu.

Swali: Nini kilikubeba hadi ukashinda

Jibu : Mambo matatu yaliyonibeba kwenye uchaguzi huo ni kujiamini, kujibu maswali kwa mujibu wa katiba ya chama na kanuni na uchaguzi kuwa huru na haki.

Mbele ya wapiga kura 952, nilikuwa na ujasiri na kulitumia jukwaa vizuri katika dakika zangu. Hata baada ya muda wangu kumalizika nilianza kupokea meseji zikisema nimewazidi wenzangu kujieleza.

“Sisi wanasiasa ulevi wetu ni watu, sasa kama watu wamejaa halafu ushindwe kucheza na jukwaa, ujue umekwama na kwa vyovyote unaweza kukosa kuchaguliwa halafu ukaanza kumlaumu mtu mwingine, pale nilicheza kama pele,” alijigamba.

Swali : Unamudu vipi siasa za uzawa?

Jibu: Katika kipindi cha uongozi wangu sitegemei kuona mambo hayo yakiendelezwa ingawa nakiri kweli kuwa yapo kwa siasa za mji huo.

Lakini kama wameweza kunichagua mimi mtu wa Kusini ina maana siasa uchwara za uzawa Dodoma zimeanza kutoweka.

Katika kata zote 41 zinazounda wilaya pamoja na jimbo la uchaguzi sitoruhusu siasa za uzawa zitawale badala yake nitafanya kila namna ili kuwasimamisha wagombea wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi.

Swali: Chama gani kinakunyima usingizi

Jibu: Viko vyama vingi hapa Dodoma, kuna mchanganyiko wa watu kweli lakini nikuambie kuwa CCM ndiyo baba lao, nitashinda kata zote 41 na jimbo tena kwa kishindo, sitaingia kwenye uchaguzi nikiwa na makundi hayo ndiyo yanaharibu mambo.

Hata hivyo, kauli zangu zitakuwa na maana kubwa kama kutakuwa na mshikamano na umoja baina ya wanaCCM wote na hasa kwa viongozi wakubwa ambao ni mabalozi na wengine wote.