MAKALA YA MALOTO: Miaka 58 ya uhuru, ujumbe wa Mbowe, msimamo wa Zitto

Rais John Magufuli alipompa nafasi mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe atoe salamu zake za maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru, kila alichokisema unaweza kukiweka ndani ya neno moja; utaifa.

Mbowe alitaka kuwepo kwa upendo, maridhiano na mshikamano. Hayo mambo matatu ndio hasa msingi imara wa taifa. Nchi isiyo na watu wenye kupendana, kuridhiana na kushikamana, hiyo haina utaifa.

Mbowe amemuomba Rais Magufuli ayatende hayo matatu kwa ajili ya nchi. Kuwafanya Watanzania wapendane, waridhiane na washikamane. Kwa sentensi fupi ni kuwa Mbowe amemuomba Rais Magufuli ajenge utaifa.

Miaka 58 ya uhuru, Tanzania haihitaji kuunganishwa kimakabila na jamii za vijiji. Bila shaka, Mbowe alipoomba Rais Magufuli aliunganishe taifa kwa upendo, maridhiano na mshikamano, analenga siasa.

Taifa halina mgawanyiko wa makabila, lakini kisiasa nchi haipo sawa. Ndio maana Mbowe amemwambia Magufuli ajenge utaifa, wakati huohuo kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aligoma kushiriki sherehe za uhuru kwa anachoeleza kwamba nchi haipo huru na hakuna demokrasia.

Mbowe na Zitto wana ujumbe wa aina moja, kwamba nchi ina mgawanyiko. Walichotofautiana ni namna ya kufikisha ujumbe. Ujumbe wa Zitto kautuma kwa kususa, Mbowe alikwenda CCM Kirumba kumwambia Rais Magufuli ashughulikie utaifa.

Ikiwa hatubishani kuhusu sauti za Mbowe na Zitto, tupate nafasi ya kujiuliza; ni kwa nini wanasiasa hasa wa upinzani wanalalamika kuwa hawatendewi haki?

Miaka 24 iliyopita, Watanzania walikuwa hawajaupokea vizuri mfumo wa vyama vingi vya siasa, maana uchaguzi ulifanyika miaka mitatu baada ya kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992.

Wakati huo Watanzania wakiwa hawajaupokea vizuri mfumo wa vyama vingi vya siasa, CCM hawakupata ushindi hata wa asilimia 75. Mwaka 2019, upinzani ukiwa umeenea zaidi, CCM inashinda asilimia 99.7 serikali za mitaa.

Miaka 24 baadaye, kipindi ambacho nchi ina wasomi wengi na teknolojia ni kubwa, wapinzani wanakosea kujaza fomu kwa zaidi ya asilimia 90.

Wapinzani wanaona wanaonewa. Hawaruhusiwi hata kufanya mikutano ya kisiasa. Ndio sababu Zitto anasusa kwenda CCM Kirumba mwenye sherehe za Uhuru, wakati huohuo Mbowe anakwenda na kumuomba Rais Magufuli aliunganishe taifa.

Kazi ya kwanza ya Mwalimu Nyerere ilikuwa kujenga daraja, ili jamii ya kabila moja ilifikie ilingine, wilaya kwa wilaya, mkoa hadi mkoa, kisha kuifanya Tanzania kuwa familia moja.

Miaka 58 ya Uhuru inaonesha kuna daraja limevunjwa. Wapo Watanzania wanaomba daraja lijengwe upya. Ukifika hapo lazima uhoji; Watu wanakumbuka, wanazingatia na kuthamini jasho la ujenzi wa daraja la utaifa ambalo lilimvuja jasho Mwalimu Nyerere kulijenga?

Kwa mtu mwenye kuthamini ndoto za Mwalimu Nyerere, atahakikisha kila siku anajenga daraja la maridhiano, upendo na mshikamano wa kitaifa. Maana hilo ndilo la awali kabisa alilifanya Baba wa Taifa ili kuifanya Tanganyika kisha Tanzania kuwa moja.

Mwalimu Nyerere alivunja vyama vingi vya siasa mwaka 1962. Miaka 30 baadaye alipigania mfumo wa vingi ukarejea ili kukuza demokrasia, Watanzania wawe na wigo mpana wa kuchagua viongozi wanaowataka.

Miaka 58 ya Uhuru; Mbowe na Zitto wana ujumbe mmoja ila wametofautiana uwasilishaji. Ujumbe huo umpendeze Rais Magufuli kukutana na wapinzani ili kujenga daraja la uhusiano wa kisiasa kati ya vyama na vyama. Mwalimu Nyerere alisababisha Wairaqi na Wahazabe kuelewana, inashindikana nini Chadema na CCM au ACT na CCM?

Kenya, Rais Uhuru Kenyatta na mpinzani wake, Raila Odinga, wanajenga daraja, Tanzania daraja lilikuwepo, je limevunjwa? Mbona wapinzani wananung’unika? Muhimu ni Katiba na sheria kuheshimiwa. Nchi ni ya vyama vingi, iachwe ifanane ki-vyama vingi.