Mkapa anasemaje juu ya wahamiaji haramu?

Sijafanikiwa kusoma kitabu cha Mzee Mkapa, rais wa tatu wa Tanzania. Nimeambiwa hakipatikani kwa sasa hadi vichapishwe vingine, ingawa wengine wanasema mitaani unakipata kwa bei juu ya iliyotangazwa. Hiindiyo Bongoland!

Waliofanikiwa kukisoma, wanampongeza Mkapa kwa kuandika wazi juu ya maisha yake, kwamba ametimiza msemo wake wa ‘uwazi na ukweli’.

Pale alipoteleza, amesema wazi na ni matumaini yetu kwamba kwa njia hii atawasaidia viongozi waliopo na wajao wasiteleze kama yeye.

Siku ya uzinduzi wa kitabu hicho, Profesa Mukandala alikuwa kwenye kipindi cha Kumekucha cha ITV akikielezea na kupokea maswali kwa simu. Nilijitahidi kupiga simu bila mafanikio. Hivyo swali langu kwake naliandika hapa: Je, Mzee Mkapa anaongea chochote juu ya msamiati wahamiaji haramu? Kwamba hawa ni raia lakini wengine si raia. Sote tunajua kwamba msamiati huu wa wahamiaji haramu ulianza awamu ya tatu.

Hapo tulishuhudia suala la uraia likiibuka kwa kasi ya kutisha. Tukasikia watu ambao tulifikiri ni Watanzania, wakavuliwa uraia! Na uraia ikawa silaha kubwa ya kuwanyamazisha watu wenye maoni tofauti.

Hadi leo hii bado tunashuhudia silaha hii ya kibaguzi inaendelea kutumika. Ningependa kujua ni kwa nini Serikali ya Mkapa ilianzisha msamiati huu.

Je, katika kitabu chake anaelezea tulivyomsaliti Mwalimu Nyerere na jitihada zake za kuwaruhusu Waafrika wote kuja na kuishi hapa Tanzania na zile za kupigania ukombozi kusini mwa Afrika. Mwalimu Nyerere hakuimba tu wimbo wa Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja, bali alitekeleza kwa matendo.

Ndo maana wakati wa uongozi wake, Tanzania, ilikuwa kimbilio la kila Mwanadamu. Wapigania uhuru walikaribishwa Tanzania na kuishi kama nyumbani kwao; walipotaka kutembelea nchi za nje kama Ulaya na kwingineko, walitumia pasi za Tanzania; walianzisha makambi ya mapambano hapa hapa Tanzania. Uganda, ilipopinduliwa na kutawaliwa na Iddi Amin, Mwalimu, alikataa kukaa kimya, alifanya uamuzi mgumu wa kuingilia kwenye mapambano ya vita vya Kagera. Hatukusikia lugha ya wahamiaji haramu wakati wa uongozi wa Mwalimu. Sasa hivi ni kinyume. Watanzania tumeanza kujenga utamaduni wa ubaguzi, tena ubaguzi mbaya kabisa. Hivi karibuni Tanzania, tumekuwa na zoezi la kuwafukuza wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi na Uganda. Ndugu zetu ambao tunaunganishwa na damu, na wengine tunaongea lugha moja na utamaduni unaofanana, lakini tunateganishwa na mipaka ya kikoloni.

Hata hivyo kwa nini tufukuzane, badala ya kushirikiana wakati tunaimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wimbo wa Umoja wa Afrika?

Tutaunganaje bila kuishi pamoja? Kwanini wahamiaji haramu, wasishawishiwe kuishi kwa vibali na kama wanafanya biashara au uwekezaji kwenye mifugo na viwanda, watozwe kodi na kuchangia Pato la Taifa?

Kama mtu anaweza kuwekeza kutoka Amerika, kwa nini Warundi, Wanyarwanda na Waganda wasiwekeze? Kwanini tusijenge daraja la kuunganisha Tanzania, Kenya, Burundi Rwanda na Uganda na daraja hili likaendelea kutuunganisha na nchi za kuzini, kaskazini na Magharibi mwa Afrika?

Ubaguzi huu ulianza kwenye utawala wa Mkapa. Ninatamani kukisoma kitabu chake ili nione anasema nini juu ya hili na analitafutia ufumbuzi gani? Tunawabagua wengine, lakini kama Mwalimu alivyosema, tukisha wabangua Warudi, Wanyarwanda nda Waganda, tutaanza kubaguana sisi kwa sisi. Na hili limeanza, suala la uraia imekuwa ni salaha ya kuwanyamazisha watu wenye maoni tofauti.

Kwa vile mtu ambaye msamiati huu ulianza wakati wake yupo, atueleze.

Je, na hapa alishauliwa vibaya kama kwenye suala la EPA? Je na hili ni kati ya mambo anayoyajutia na kuyaungama?