Msamaha wa wahujumu unakumbusha EPA

Saturday October 12 2019

 

By Luqman Maloto

Aprili 23, 1963, mwanaharakati na shujaa wa wakati wote wa mapambano ya uhuru kamili wa mtu mweusi nchini Marekani, Martin Luther King (jr) alitoa moja ya hotuba inayokumbukwa wakati wote, “I Have A Dream”, yaani nina ndoto.

Katika sehemu ya hotuba hiyo, alisema katika benki ya haki Marekani, watu weusi walikuwa wakipewa hundi chafu ambayo ilionyesha hakukuwa na salio la kutosha. Akasema kuwa dhamira yao kuendelea kupigania haki ilitokana na imani yao kwamba benki ya haki kwenye nchi yao haikuwa mufilisi.

Kitendo cha Rais John Magufuli kuonyesha huruma kwa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi na kutoa msamaha kwamba warejeshe fedha wanazotuhumiwa kukwapua, kukwepa kodi au kuisababishia hasara Serikali, kisha waachiwe huru, kwa sehemu fulani ni ishara kuwa benki ya haki Tanzania haijafilisika.

Mashtaka ya uhujumu uchumi ni mazito mno. Hayana dhamana. Watu wanasota rumande, miezi na miaka. Wanaambiwa upelelezi haujakamilika. Angalau Rais Magufuli ameona kuwa ipo haja kwa walio tayari kulipa wasamehewe.

Japo Katiba Ibara ya 59B, inasema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hatakiwi kuingiliwa na yeyote, mtu au mamlaka, pindi anapotekeleza wajibu wake, Rais Magufuli ameona kuna haja ya kupunguza mlundikano wa watuhumiwa mahabusu, wapo mahabusu miaka, kesi haziendelei maana upelelezi haujakamilika.

Msamaha wa Rais Magufuli unatoa hati mbaya kwa DPP, kwamba yeye hakuona kama si sawa watu kukaa mahabusu muda mrefu wakati kesi haziendelei. DPP ambaye kazi yake ni kutengeneza mashtaka, kushtaki na kusimamia mashtaka, anapeleka mahakamani watu ambao upelelezi haujakamilika.

Advertisement

Kama upelelezi haukamiliki miaka nenda rudi, maana yake mashtaka yanakuwa hayajatosheleza. Yaani mtu anakuwa anahisiwa kutenda makosa lakini hajawa mtuhumiwa.

Mahakamani wanapaswa kupelekwa watuhumiwa waliopelelezwa. Sio wenye kuhisiwa kuwa watuhumiwa. DPP anashtaki kisha upelelezi unaanza, badala ya kumshtaki mtu baada ya upelelezi.

Kabla ya kuanzishwa kwa Ofisi ya DPP, maofisa wa polisi na Takukuru ndio walikuwa wanaendesha mashtaka. Ilionekana kuna kasoro. Wakamate wao, wapeleleze wenyewe, halafu waandae mashtaka na kuyaendesha. Kungekuwa na mgongano wa masilahi.

Ofisi ya DPP ikaanzishwa, angalau kuchuja pumba na mchele. Polisi au Takukuru wakikamata, wanapeleka mashauri yao kwa DPP ambaye anapitia, anayoona hayana msingi anayapuuza, yenye mashiko anayapeleka mahakamani.

Ajabu DPP anaruhusu kwenda mahakamani kesi nyingi ambazo tuhuma zake hazijakamilika, matokeo yake Rais Magufuli anaona bora kutoa msamaha, hata kama DPP naonekana ameingiliwa.

Pamoja na msamaha bado kuna kasoro kadhaa. Ya kwanza ni kuhusu matokeo ya msamaha. Wenye fedha na walio na utayari watatoka.

Ambao hawana, hata kama hawakutenda makosa, wataendelea kusota.

Tunazingatia tamko la Katiba kwamba mshtakiwa hana hatia mpaka athibitishwe na mahakama. Litazamwe vizuri hili kuthibitisha kuwa benki ya haki Tanzania si mufilisi.

Pili ni faida ya msamaha. Je, Rais Magufuli amehurumia watu kukaa mahabusu muda mrefu? Kama ndiyo, wale ambao ni maskini lakini wametuhumiwa kimakosa, huruma yao ni ipi? Na waliotenda makosa kweli, kwa vile wana fedha ndiyo wasamehewe?

Miaka 13 iliyopita iliibuka kashfa ya uchotaji fedha Benki Kuu kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Shilingi bilioni 133 zilikwapuliwa. Rais Jakaya Kikwete, alitoa msamaha warudishe fedha walizoiba, ambao hawakurudisha walishtakiwa na kufungwa. Kwamba wezi wenye fedha walisamehewa.

Kwa mantiki hiyo, hata msamaha wa Rais Magufuli, unaweza kuwapa msamaha wezi wenye fedha, wakarejea mitaani.

Watu ambao kwa hakika wametenda uhujumu uchumi hawapaswi kusamehewa kienyeji, pamoja na hivyo hawatakiwi kuwekwa mahabusu miaka kama hakuna ushahidi. Si vitendo vizuri katika mfumo wa utoaji haki.

Kuna hoja kuwa msamaha wa Rais unaingiliana na sheria ya makubaliano kati ya mshtaki na mshtakiwa (plea bargain). Kama ndivyo, hii haipaswi kutolewa kwa amri ya Rais, bali mtuhumiwa mwenyewe kwa ridhaa yake angepaswa kuomba, kisha upande wa mashtaka ukiona ombi lina tija, wanakubaliana kupunguza adhabu kisha makubaliano yanapewa kibali na mahakama.

Plea bargain huwa ina upande pia wa mtuhumiwa kuomba kutoendelea na mashtaka, kwa hiyo analipa fidia ya makosa yake lakini anatambulika hana hatia.

Upande wa mashtaka ukiona ombi hilo halina tija kwa sababu upo ushahidi wa kutosha kumtia hatiani, unakataa na kwenda mahakamani.

Marekani hutumia sheria hii katika kupata ufumbuzi wa uhalifu wa mipango na mauaji. Mfano, watuhumiwa wakubwa wa dawa za kulevya, wakikamatwa, hupewa ofa ya kutaja siri zao ili kupunguziwa adhabu.

Aliyekuwa bilionea wa cocaine, Rick Ross Freeway, alinusurika kwenda jela maisha kwa sababu ya kufanya plea bargain, akatoa siri za mtandao wake, akafungwa jela.

Jambazi aliyekuwa akitumia akili nyingi kupora benki, akiitwa Friday Night Robber, aliisumbua Marekani muda mrefu, alipokamatwa, alipewa ofa ya kutaja mbinu zake ili apate punguzo la adhabu.

Akahukumiwa miaka 15 jela. Mamlaka zilitaka kujifunza kuhusu akili na mbinu zake za uhalifu. Je, Serikali inataka kupata nini kwa ofa yake kwa washtakiwa uhujumu uchumi?

Advertisement