Mtatiro: Madai ya Katiba Mpya nawaachia wapinzani

Agosti 11, 2018 aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alijitoa kwenye chama hicho na kujiunga na CCM. Uamuzi wake ulishtua wengi kutokana na alivyokuwa mkosoaji mkubwa wa CCM na Serikali. Katika mahojiano na Mwananchi amezungumzia masuala mbalimbali, ikiwamo hatima ya mambo aliyokuwa anayapigania.

Swali: Ulipoondoka CUF wapo waliochukulia kama usaliti wa mageuzi uliyokuwa ukiyapigania, nini maoni yako?

Jibu: Kwanza ni muhimu sana watu wakajua elimu ya siasa na utawala. Watu wengi wako kwenye siasa kwa malengo. Mimi natoka kwenye familia masikini, lakini Mungu amenijalia vipaji vya uongozi kwa hiyo kila nilikopita tangu shule ya msingi, sekondari mpaka chuo kikuu.

Baadaye nilitafuta chama cha siasa ili nikifanyie kuwa jukwaa la kusimamia ajenda. Kwa hiyo mimi nina ajenda ya kupambana na umasikini na ninaipigania.

Mwanzoni niliona CUF inaweza kuwa jukwaa zuri la kisiasa. Lakini nikilinganisha vyama leo unaona chama imara nchini ni CCM. Kina nguvu, kina ubora kuliko vyama vingine.

Nimekaa upinzani miaka 10, nilichojifunza ni ugomvi, matatizo, hakuna progress (maendeleo) kuna mapambano ya ndani kwa ndani. Yaani hakuna kitu kizuri nilichojifunza kwenye opposition (upinzani).

Nimefanya hiyo kazi kwa miaka 10, nikajiridhisha kuwa napoteza muda. Nikaona kuna chama bora na imara ambacho ni CCM. Kwa nini nisiingie niendelee kupambana na ajenda yangu?

Swali: Kinachoulizwa ni yale uliyokuwa ukihubiri ndiyo sasa umeyasaliti?

Jibu: Mara nyingi inachukuliwa kama usaliti, lakini ni kutokukomaa na kukosa elimu ya siasa na uongozi. Kwa watu wanaofahamu wanajua kwamba Donald Trump ni Rais wa Marekani kupitia Republican lakini ameshahama vyama mara tatu. Sasa utasema Trump ni msaliti?

Wewe utasema hivyo, lakini ndiye Rais wa Marekani, anatoa mchango wake katika kuiongoza Marekani.

Swali: Kabla hujahama chama ulihojiwa na polisi kuhusu andiko lako uliloweka Facebook. Je, wito ule ndiyo ulisababisha uhamie CCM?

Jibu: Hapo katikati hapakuwa na kitu chochote, nilikuwa kwenye tafakari kubwa. Nani wa kumbana Mtatiro? Polisi hawawezi.

Yaani kati ya vitu nimekuwa nikiviishi ni kutokuwa mwoga. Ingekuwa hivyo basi polisi wangekuwa wanamwita mtu anahamia CCM. Nadhani watu wote waliohamia CCM hawakubanwa na polisi.

Swali: Ilikuwaje?

Jibu: It was a very small case (ilikuwa kesi ndogo tu). Mimi niliitwa kuhojiwa kuhusu posti niliyoandika na nikawapatia polisi ufafanuzi kwamba nilichokuwa nakizungumzia ni kwamba ‘huyu kijana hakuwa anamlenga Rais Magufuli, alikuwa analenga kitu tofauti.’

Niliwaeleza “ninyi mnabeba ugomvi mnamkamata au hamtaki mtu atoe maoni tofauti na Rais, jambo ambalo ni uongo. Magufuli ni mwanasiasa wa muda mrefu anataka challenge (changamoto).

Kwa hiyo sasa kajambo kadogo tu kakitokea polisi wanakwenda wanakamata, niliwa ‘chalenji’ polisi, walinichia, nikarudi kwangu. Sikukaa mimi kituoni, nimeendelea na tafakari zangu. Baada ya wiki kadhaa ndiyo nikaondoka upinzani.

Kwa hiyo mimi niliondoka mwenyewe. Ilikuwa shock (mshtuko) kwa nchi. Viongozi wenyewe wakubwa wa CCM walinipigia na hawaamini.

Kuna kiongozi mmoja mkubwa alinipigia simu anauliza, Mtatiro umeondoka opposition? Nikamwambia nimeondoka, nimetafakari nikaona napoteza muda.

Swali: Uliwahi kugombea ubunge katika jimbo la Ubungo mwaka 2010 na ukakosa. Pengine ulitafakari ukaona urahisi wa kupata nafasi hiyo ni kwenda CCM?

Jibu: Si kweli. Nataka urejee kwenye nia yangu ni ipi? Kuisaidia Serikali kutafuta maendeleo na kutafuta jukwaa la kisiasa ambalo niliona limeyumba.

Nilijiunga na CCM kama mwanachama wa kawaida, hata kama Rais Magufuli asingeniteua kuwa mkuu wa wilaya ningeendelea kuwa mwanachama wa kawaida. Hata 2020 nisingegombea chochote, au nisingepata chochote ningekuwa mwanachama wa kawaida.

Swali: Kama uliingia CUF ili ukijenge kiwe chama kikubwa, ulishindwaje?

Jibu: Nimesaidia mabadiliko makubwa ndani ya CUF, hata hao wabunge 10 Tanzania Bara kwa kiasi kikubwa nilitoa mchango mkubwa kupatikana.

Hata hawa vijana kina Hamidu Bobali (Mbunge wa Nchinga), mara ya kwanza yuko chuo kikuu nikamwita nikamwambia utakwenda Lindi, kwa sababu nilikuwa najua anatoka kwenye jimbo lile ambalo mara kwa mara CUF walikuwa wanaweka mgombea wa darasa la saba na alikuwa hafanyi vizuri.

Nimefika pale ofisi za CUF nimekuta kuna darasa la saba na kidato cha nne ndiyo wamejaa, mpaka maofisa. Lakini naondoka kuna maofisa wa chuo kikuu. Kwa hiyo nilikuwa najenga uwezo wa CUF lakini niligundua imepoteza mwelekeo, nikaondoka).

Swali: Ukifuatilia kauli na misimamo yako wakati ukiwa upinzani, ulisisitiza katika mabadiliko ya Katiba, kwa sasa huoni tena umuhimu wake?

Jibu: Madai ya Katiba, maandiko na matamko mbalimbali yanayohusu misimamo ambayo mtu anayatoa, anatoa kwa sababu ana upande. Wewe ni mwanadamu lazima uwe na upande.

I was living in Rome (Nilikuwa naishi Roma), unapoishi Roma utaishi kama Waroma, ukienda China leo watu tangu asubuhi wanapika nyoka, huwezi kufa njaa, utakula nyoka, ukienda Israel wanapika viazi utakula viazi. Huwezi ukaenda ukasema siwezi kula.

Kwa hiyo wale waliokuwa na madai ya Katiba nimewaacha waendelee na madai ya Katiba, mimi kwa sasa nadai maendeleo. Nimekwambia malengo ya kujiunga na siasa ilikuwa ni maendeleo, hayo mengine nilikutana nayo tu kwenye vyama vya siasa. Chama kinakaa kikao kinaamua kwamba tuna msimamo wetu katika Katiba, kwa mfano ni serikali tatu, wewe ni kiongozi, mkitoka hadharani mtasema Serikali tatu.

Lakini hata katika nafasi yako hupendi, lakini utalisimamia lile jambo kama kiongozi na wenzio waone, hata kama hulipendi. Kwa hiyo tutafute majukumu ya mtu aliyekuwa kiongozi na mtu aliyeachana na upande huo.

Wewe unakuwa Mkristo unaamini Yesu ni Mungu, baadaye ukiona Ukristo haukufai ukaukiri Uislamu unakuta Yesu ni nabii, utaendelea kusema Yesu ni Mungu?

Swali: Tangu umeteuliwa kuwa DC Tunduru, umeionaje kazi hiyo mpya?

Jibu: Tunduru ni wilaya kubwa ina kilometa za mraba 18,700, ni eneo kubwa kuliko mkoa mzima wa Mtwara na wilaya zake.

Ni eneo kubwa la kiutawala ambalo mheshimiwa Rais aliniamini na kunikabidhi.

Bahati nzuri DC aliyenikabidhi alifanya vizuri kuna baadhi ya mambo aliyafanya vizuri na kuna mambo alinieleza kuwa ni pasua kichwa niyafanyie kazi.

Miongoni mwa mambo aliyonikabidhi ni elimu ya sekondari. Nilianzisha utaratibu mzuri na sasa tunafanya vizuri. Niliweka makambi ya vijana wa darasa la saba na darasa la nne Tunduru nzima.

Vijana wanaletewa mpaka maprofesa wanapatiwa ushauri juu ya mambo mbalimbali kwa sababu wapo katika maeneo ambayo wengine wanatelekezwa na wazazi.

Tumeanza vizuri. Kwa mfano katika elimu ya msingi, kati ya halmashauri nane, Tunduru tumekuwa wa pili kimkoa, shule ya msingi iliyokuwa ya tatu kitaifa imetoka Tunduru. Kabla ya hapo hali haikuwa nzuri.

Kwa upande wa shule za sekondari, katika halmashauri nane tumekuwa wa saba. Tumefanya vibaya sekondari, lakini hii 2019 tutafanya vizuri kwa sababu nimeweka mikakati.

Swali: Wilaya hiyo pia inalima korosho, umewasaidiaje wakulima katika kero zao?

Jibu: Korosho ina matatizo yake, kwanza wizi katika vyama vya msingi, wizi wakati zinasafirishwa, wakati zinapelekwa kwenye ghala kuu na tatizo la mwisho la kangomba.

Kwanza tumejipanga kuhakikisha vyama vyote vya msingi vinakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu zao la korosho.

Kwa hiyo kuna miongozo niliyoiandaa kwa Tunduru. Amcos fulani ya Tunduru mjini ajue masharti fulani, hiyo ndiyo nimeitumia kuandika miongozo kurahisisha.

Kwa mfano usafirishaji wa korosho kutoka kwenye ghala kuu kwenda ghala la chama cha msingi, korosho zimekuwa zikiibwa pale katikati, kwa mfano gari likiondoka zinahesabiwa tani 20 zikifika kule zinahesabika tani 15, tano zimeibiwa hapo katikati.

Kwa hiyo sasa hivi nimeanzisha utaratibu kwamba ghala likijaa la chama cha msingi, wanazipakia kwenye gari, lile gari haliondoki pale mpaka nipigiwe simu na nitatuma vyombo vyangu kuhakikisha.