MAKALA ZA MALOTO: Mwigulu anarudia makosa yaleyale ya Lowassa

Mpini hudanganya. Ukiushika huwezi kujua maumivu wanayopata walishika makali. Utawakata, watalia na unaweza kushangaa, wanalia nini?” Mshika mpini akigeuziwa makali ndipo hutambua maumivu yake.

Mpini ulimuongopea Omar Al Bashir alipokuwa Rais wa Sudan. Akawa anasweka wapinzani wake wa kisiasa kwenye gereza la mateso la Kober.

Al Bashir aliona malalamiko kuhusu gereza la Kober ni upuuzi mtupu. Ni kwa vile alikuwa ameshika mpini. Leo tunaelezwa al Bashir yupo gerezani Kober. Bila shaka naye analalamika gereza hilo ni jehahamu.

Watu walio madarakani hujisahau kwamba nao wanaweza kuwa upande wa pili. Matokeo yake hutunga sheria kandamizi wakidhani wao hazitawagusa.

Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda ‘KK’, alisaini sheria zenye kumpa mamlaka ya kumweka kizuizini mtu. Mwaka 1981 alipomweka mahabusu Fredrick Chiluba, hakuwaza kama nyakati zijazo Chiluba huyohuyo angekuwa Rais, kisha naye angemfunga. Baada ya Chiluba kushinda urais 1991, alitumia sheria zilezile kumweka kizuizini Kaunda.

Lowasa, Sumaye

Tangu Uchaguzi Mkuu 1995, vyama vya upinzani vimekuwa vikililia Tume huru za uchaguzi. Kwamba zilizopo, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hazikidhi viwango vya haki na demokrasia.

Fredrick Sumaye alikuwa Waziri mkuu 1995-2005, akafuatia Edward Lowassa 2006 - 2008. Vipindi hivyo Sumaye na Lowassa hawakujishughulisha na malalamiko ya wapinzani.

Kimsingi, hawakuona kasoro za tume za uchaguzi kama ambavyo wapinzani walilalamikia. Ni kwa sababu matarajio yao waliyaelekeza kuamini kuwa ndoto zao za kisiasa zingetimia ndani ya CCM.

Kimbunga cha Uchaguzi Mkuu 2015, kiliwafanya Sumaye na Lowassa wajikute wapo upinzani. Lowassa akawa mgombea urais wa Chadema, Sumaye akasimama kama meneja kampeni.

Matokeo yalipotoka na kuonyesha Lowassa ameshindwa, ndipo malalamiko kuhusu tume yakaibuka. Lowassa pia alimuunga mkono aliyekuwa mgombea urais wa CUF Zanzibar, Seif Sharif Hamad kulalamikia matokeo ya uchaguzi kufutwa.

Kimsingi mazingira ya tume ambayo Lowassa aliyakumbatia akiwa waziri mkuu ndiyo hayo ambayo aliyalalamikia akiwa upinzani. Kipindi akiwa kimya wapinzani wakilalamika, kama angewaza ipo siku atakuwa mpinzani, bila shaka angeshauri wapinzani wasikilizwe.

Ukiweka pembeni hilo la tume, mwaka 2014 wakati wa mchakato wa Katiba mpya, Lowassa alikuwa mwana CCM aliyeshiriki kubadilisha rasimu ya Tume ya Jaji Warioba kisha kupatikana Katiba Inayopendekezwa kupitia Bunge Maalum la Katiba.

Baada ya kuenguliwa CCM, Lowassa hakuwa rafiki tena wa matokeo ya Bunge la Katiba lililoongozwa na Samuel Sitta. Pengine Lowassa baada ya kuhamia Chadema alitamani muda urudi nyuma ili aitetee rasimu ya Katiba kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba.

Sakata la Mwigulu

Hivi karibuni, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa hukumu ya kihistoria, yenye kupiga marufuku wakurugenzi wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Uamuzi wa mahakama ulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa uwepo wa wakurugenzi kama wasimamizi wa uchaguzi unakiuka Katiba, inayotaka maofisa wa uchaguzi wasiwe na upande.

Mbunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba amekuwa akitetea mitandaoni uwepo wa wakurugenzi hao kama wasimamizi wa uchaguzi. Dhahiri, anaona sawa watu ambao mahakama imeridhika ni makada wa CCM, kusimamia uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi.

Mwigulu anatenda makosa yaleyale ya Lowassa na Sumaye kuona malalamiko ya kutaka tume huru hayana msingi. Anataka na yeye siku akiwa upinzani ahisi kudhulumiwa ushindi, ndipo alie kuwa wakurugenzi hawafai kusimamia uchaguzi. Sasa kwa kuwa yeye ni CCM anaona mkurugenzi kada wa CCM ni sawa kuwa msimamizi wa uchaguzi.