Nafasi ya mitandao ya kijamii katika kuleta mabadiliko

Wednesday May 29 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi

Matumizi chanya ya mitandao ya kijamii yanaweza kuchochea mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kupunguza umasikini katika jamii.

Pamoja na vijana ambao ndio watumiaji wakubwa, mitandao ya kijamii inawagusa watu wote. Inaondoa mipaka kati ya rika, rangi, itikadi, jinsia na hali zote za kiuchumi.

Taasisi ya Change Tanzania imeona fursa kubwa katika eneo hilo ikawakutanisha vijana zaidi ya 100 katika Kijiji cha Arusha, wengi kutoka vyuo vikuu ili kujadili nafasi yao katika kuchochea matumizi chanya ya mitandao ya kijamii.

Maria Sarungi, mkurugenzi wa Change Tanzania anasema mitandao ya kijamii, vijana wana fursa kubwa ya kuchochea mabadiliko katika jamii.

Bahati mbaya “vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii, kuandika mambo ambayo hayana tija kwao wala kwa taifa, kama kuweka picha, kusutana na hata kuandika mambo ambayo baadhi yamekuwa yakisababisha wanatiwa hatiani.”

Anasema vijana wanapaswa kuitumia mitandao ya kijamii kutetea maslahi yao, haki zao na kuiwajibisha serikali inapofanya makosa.

Advertisement

“Tunawaeleza kutumia mitandao kusaidia kuchochea maendeleo katika jamii na kuacha kubaki kuwa wasikilizaji au walalamikaji,” anasema.

Sarungi anasema hivi sasa matumizi ya mitandao hayazuiliki na kinachopaswa kufanywa ni kutolewa elimu ya matumizi chanya ya mitandao hiyo na si kuwa na sheria kali za kuifunga.

Kwa mujibu wa Sarungi, vijana ni sehemu muhimu ya kijamii, hivyo lazima wachangie mawazo na vitendo katika kuleta maendeleo.

“Change Tanzania inataka kuhakikisha vijana wanapata fursa ya kutafakari na kujua nafasi yao katika jamii... wanapaswa kuelewa haki yao na wananchi wanapaswa kuelewa haki zao na kuwa na matumizi chanya ya mitandao, kujua haki za binadamu na kutoa mawazo chanya kwa manufaa ya nchi,” anasema.

Si Sarungi pekee anayeona fursa hiyo, hata mwanasheria na mwanaharakati, Fatuma Karume anasema vijana wana fursa nzuri ya kuidhibiti serikali isiendelee kufanya mambo ambayo yanakiuka katiba ya nchi.

“Vijana wanapaswa kujua hii nchi ni yao, si ya rais, wana nguvu siku ya kupiga kura kufanya mabadiliko,” anasema Karume, rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS),

Anasema vijana na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kufahamu kuwa Taifa linapaswa kuongozwa kwa kuzingatia sheria, Katiba, mikataba ya kimataifa na si matakwa ya mtu mmoja.

“Serikali haitaki kufuata baadhi ya maamuzi ya mahakama za kimataifa, ikiwapo mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na mahakama ya Afrika ya Mashariki. Hili si jambo zuri, kuna kesi zinaamuliwa kama za kuruhusu mgombea binafsi, wanazipuuza,” anasema.

Anasema Taifa linapokubaliana na nchi nyingine za Afrika katika mikataba ya kuleta haki ni muhimu kufuata walichokubaliana na vijana wana fursa ya kusisitiza hilo kwa kuchochea mabadiliko, kudai utawala wa sheria na kutaka Katiba iheshimiwe.

“(Vijana) Wanapaswa kubadili mitazamo ya kijamii kuwa siasa ni uongo. Wanasiasa wanaongea mambo ya uongo majukwaani kwa kisingizio cha kisiasa.

“Utamkuta kiongozi wa kisiasa ukiwa naye, anaongea vizuri tu mambo mbalimbali, lakini akiwa jukwaani anaongea mambo ya ajabu. Ukimuuliza anasema ilikuwa ni siasa tu, sasa tunapaswa kuondoa jambo hili, kwani siasa si uongo,” anasema Karume.

M bali na wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, hapa viongozi wa dini wana kauli kuhusu vijana na mitandao.

Askofu Benson Bagonza anasema kundi la vijana likitumia vema mitandao ya kijamii na likishirikishwa, ni moja ya makomandoo katika vita dhidi ya ufisadi, rushwa na wizi wa rasilimali za taifa.

Askofu Bagonza anasema makomandoo wengine ambao wanaweza kushirikiana na vijana katika vita ya ufisadi iliyotangazwa na serikali ni vyombo huru vya habari, asasi za kiraia na taasisi zisizo za kiserikali; wengine vyama vya wafanyakazi, wanaharakati, vyama vya upinzani, Bunge huru na Katiba nzuri.

“Kuwapunguzia uhuru makomandoo hawa au kugombana nao badala ya kugombana na ufisadi, ni kutangaza kushindwa kabla ya mapambano kuanza,” anasema askafu huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe.

Askofu anaongeza “matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ni nyenzo nzuri ya utetezi katika jamii, lakini wasioliona hili ni wale wanaodhani kwa nafasi zao, hawahitaji kutetewa.”

Anasema mitandao ya kijamii ina nguvu ya udhibiti wa matumizi mabaya ya madaraka na madhambi mengine katika jamii,” anasema.

Anasema Taifa lilipopata uhuru mwaka wa 1961, Baba wa Taifa alitangaza maadui watatu wakubwa wanaolikabili ambao ni ‘umaskini, ujinga na maradhi.

“Nimeweka ujinga katikati ya umaskini na maradhi kwa makusudi. Sehemu kubwa ya umaskini wetu na sehemu kubwa ya maradhi yetu, vinabebwa na ujinga wetu,” alisema.

Alisema Taifa likifanikiwa kupunguza ujinga , sehemu kubwa ya umaskini na maradhi, vitashughulikiwa kwa urahisi zaidi na matumizi chanya na sahihi ya mitandao ya kijamii ni njia isiyoepukika ya kuuondoa au kuupunguza ujinga.

Faida za matumizi ya mitandao

Askofu Bagonza na Dk Azaveli Lweitama na Mwanaharakati Abdul Nondo wanasema kuna faida nyingi ambazo zinapatikana katika kuruhusu matumizi chanya ya mitandao kuliko kudhibiti mitandao.

“Wajinga wengi hujulikana wanapojieleza. Ili kuwasaidia hao, inabidi kuwaruhusu waseme ndipo tubaini ujinga wao na kuutafutia tiba. Kuzuia au kuthibiti uhuru wa kujieleza, ni kuuwekea mbolea ujinga ambao ni adui wa taifa na utaifa wetu,” anasema Askofu Bagonza.

Anasema hoja za wanasiasa na watawala wengi katika eneo hili kuwa uhuru una mipaka, ni makosa kwani uhuru ukiuwekea mipaka inayoonekana unakuwa si uhuru tena bali utumwa mstaarabu.

“Uhuru wenye mipaka si uhuru kamili. Tunaweza tusipende sana maoni yangu haya, lakini ujinga si tusi, na kila mtu ni mjinga kwa jambo asilolijua. Wanaosisitiza mipaka katika uhuru wa kujieleza ni “wajinga” katika dhana nzima ya uhuru kama mimi nilivyo mjinga wa kutoelewa wanaogopa nini,” anasema.

Akizungumzia uchumi wa soko akihusisha na mitandao ya kijamii anasema ili kufaidi uchumi wa soko. Soko ndilo kichocheo cha matumizi ya mitandao. Dunia nzima bila kutumia ngoma wala baragumu kuita watu wakutane chini ya mbuyu, inakutanishwa na mitandao ya kijamii.

Alisema hivi sasa watu hatari kuliko magaidi ni wale wanaodhani wanamiliki ukweli na kudhani wao ndiyo kipimo halisi cha uzalendo, usahihi, uadilifu na mamlaka ya mwisho.

Ni mitandao ya kijamii tu inayoweza kuiepusha dunia na watu hawa hatari wa kizazi hiki na kijacho.

Anasema kuna watu si wajinga, lakini pia si werevu, hawa nao dawa yao si kuwapuuza. Ni kuwaelimisha kupitia mitandao ya kijamii.

Dk Lwaitama anasema matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ni uwanja wa kubadilisha na ujinga na asiyeenda katika uwanja huo, anabaki na ujinga wa aina moja kwa muda mrefu.

Anasema mitandao ni jukwaa ambalo halina udhibiti ambalo watu wa kada mbalimbali wanakutana na kutoa maoni yao na ndio sababu mitandao ikitumika vizuri inaleta mabadiliko haraka katika jamii.

“Unaweza kudhibiti magazeti, televisheni na redio lakini huwezi kudhibiti mitandao kwani Tanzania si kisiwa duniani,” anasema.

Anasema vijana katika mataifa ya Misri, Algeria, Tunisia na karibuni Sudan wameweza kuitumia kuhamasishana kuleta mabadiliko katika mataifa hayo.

Profesa Lwaitama anasema hapa nchini, nguvu ya mitandao ya kijamii, imeibainika katika matukio ya kushambuliwa kwa Tundu Lissu, mbunge wa jimbo la Singida Mashariki na kutekwa na watu wasiojulikana Mdude Nyangali.

“Kama si kilele za mitandao ya kijamii inawezekana leo Mdude asingekuwa amepatikana,” anasema.

Wakili Shilinde Swedi anasema ni muhimu vijana na jamii kuungana kudai haki ikiwamo kufungua kesi za kimkakati kama alivyofanya Bob Wangwe kupinga wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi.

“Vijana wana mambo mengi yanawakera katika jamii, lakini hawachukui hatua. Wangwe ni mfano wa kuiga aliona wakurugenzi ni tatizo katika chaguzi akaenda mahakamani na ameshinda kesi,” anasema.

Kwa upande wake Nondo, anasema vijana wana wajibu wa kuongoza mapambano kupitia mitandao ya kijamii kudai haki na kuheshimu katiba.

Advertisement