Nani ni nani kati ya CCM, CUF, ACT Wazalendo Zanzibar

Kwa muda mrefu, Zanzibar imekuwa na siasa kali hasa wakati wa uchaguzi mkuu. Vyama vya siasa vimekuwa vikichuana kila kimoja kikitaka kushika hatamu za uongozi katika visiwa hivyo maarufu kwa utalii duniani.

Vyama vya CCM na CUF ndivyo vilikuwa vikishindana kwa karibu kwenye chaguzi zilizopita za Zanzibar wakati vyama vingine kama Chadema na NCCR Mageuzi vikiwa na ngome kubwa zaidi upande wa Tanzania Bara.

Tukio la Januari 2001, bado halijafutika katika historia ya Zanzibar ambako vikosi vya jeshi la polisi vilitumia nguvu kuyavunja maandamano ya kisiasa yaliyoitishwa huko Zanzibar kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2000.

Vyama vya CCM na CUF ndivyo vilivyokuwa vikichuana vikali kwenye uchaguzi huo uliomuweka madarakani Rais Amani Abeid Karume ambaye wakati huo alipokea kiti hicho kutoka kwa Rais Salmin Amour. Mbali na chaguzi nyingine ule wa 2010 uliweka historia mpya visiwani humo ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kati CCM na CUF na Maalim Seif Sharif Hamad akawa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Hata hivyo, sasa mambo yamebadilika. Ule ushindani wa CCM na CUF unaweza usiwepo katika uchaguzi wa Oktoba kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya Maalim Seif kukihama chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo, Machi 18, 2019.

Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na ushindani mkali kati ya CCM na ACT Wazalendo ambacho kilianzishwa mwaka 2014, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Chama cha ACT Wazalendo kilianza kupata umaarufu Zanzibar baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu CUF, Maalim Seif kutangaza kuhamia ACT Wazalendo na safu yake ya viongozi upande wa Zanzibar. Chama hicho kiliendesha operesheni ya “shusha tanga, pandisha tanga,” kikiwa na lengo la kuvuna wanachama wapya ambao watakiwezesha kuhimili ushindani dhidi ya chama tawala.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe anasema wameandikisha wanachama kati ya Machi 2019 na Desemba 2019 baada ya operesheni ya “shusha tanga, pandisha tanga” huko Zanzibar, wameuza kadi za uanachama na wana kanzidata ya wananchama wao.

Zitto anasema ACT Wazalendo ndicho chenye wanachama wengi zaidi Zanzibar kuliko vyama vyote na hata uchaguzi ukiitishwa leo, wana uhakika wa kushinda kwa kura za wanachama wao pekee.

“Mimi nakwambia tuna wanachama 231,357 Zanzibar wakati CCM hawana wanachama 150,000 Zanzibar. “Sisi ukienda Vuga (zilipo ofisi za chama Zanzibar) utakuta mpaka picha za wanachama hao, tuna database (kanzidata) ya wanachama wetu wote, with phone numbers (na namba zao za simu),” anasema Zitto.

Mbali na takwimu za Zitto, hali halisi ya siasa za Zanzibar inakipa chama hicho nafasi ya kushindana na CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao. CUF ambacho kilitoa ushindani mkubwa kwenye chaguzi zilizopita huko Zanzibar sasa kimepoa, hata hivyo, bado mikakati yake haijawekwa wazi wakati uchaguzi mkuu wa Oktoba ukikaribia.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu madai ya Zitto kwamba ACT Wazalendo ndiyo inaongoza kwa kuwa na wanachama wengi Zanzibar, Katibu Mkuu wake, Khalifa Suleiman Khalifa anasema hana uhakika na suala hilo na kwa kuwa kila mtu ana uhuru wa kusema, basi Zitto aachwe aseme. Hata anapoulizwa kuhusu idadi ya wanachama wake visiwani Zanzibar, Khalifa anasema, “sisi hatutaki kusema idadi ya wanachama wetu, ni siri yetu wenyewe. Tusubiri uchaguzi mkuu tuone.” Licha ya ACT Wazalendo kudai kuwa na wanachama wengi, bado nguvu ya CCM haiwezi kubezwa.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Zanzibar, Abdalla Juma Saadala “Mabodi” akijibu hoja ya Zitto, alisema CCM Zanzibar inawanachama wengi zaidi bila kutaja idadi.

, alijibu “wengi zaidi”.

Hata hivyo, pamoja na kukosekana kwa takwimu za wanachama wa CCM Zanzibar, bado chama hicho ni kikubwa na kina nguvu za ziada kwa sababu ni chama tawala. ACT Wazalendo kinachotarajiwa kutoa ushindani mkali kinatakiwa kujipanga.