ANTI BETTIE: Nataka kuwa Freemason, nipe mchongo shangazi

Natamani kujiunga na Freemason, maana huko maisha ni nafuu na fedha nje nje. Tofauti na hapo mji umeshanishinda bora nirudi kijijini.

Nifanyeje kujiunga?

Aliyekuambia Freemason watu wanajiunga ni nani? Halafu umeshindwa kutumia akili ulizozaliwa nazo kutafuta maisha unatamani njia za mkato.

Wazo ulilonalo la kurudi kijijini ni zuri, lakini liboreshe kwa kujipanga unakwenda kufanya mini huko.

Watu wanaoishi kijijini waliojipanga na kuwekeza kwenye kilimo wana maisha mazuri na hawatamani kujazana mijini, hivyo jiandae ukalime achana na ndoto za kulala masikini kuamka tajiri.

Nimekinai penzi lake

Habari! Nimeoa huu mwaka wa pili. Cha ajabu siku hizi najilazimisha kukutana kimwili na mke wangu kwa sababu hanivutii na sisisimki tena hata akikaa bila nguo.

Nifanyeje?

Pole kwa tatizo hilo. Cha kufanya badili aina ya maisha, ikiwamo kujipunguzia kazi, kupata muda wa kufanya mazoezi na kupunguza msongo wa mawazo.

Jaribu pia kuwa karibu na mkeo na upunguze kulumbana, inawezekana mkifanya hivyo mnasemeana maneno makali yanayoishi kichwani mwako.

Lakini unaweza kubadili aina ya maisha, ikiwamo kulala eneo lile lile, kurudi muda ule ule tena ukiwa umechoka, inaweza kuchangia uone kila kitu ni cha kawaida.

Jambo lingine toka kwa ajili ya matembezi na mwenza wako, mkapate chakula cha jioni pamoja au msafiri kidogo nje ya maji, hii itasaidia kwa sababu mtapata wasaa wa kuwa peke yenu na kuzungumza mambo yenu hivyo itarudisha upendo.

Pia kwa upande mwingine kwa mwanamke kuolewa hakuna uhusiano wowote na kujibwetekea, mwanamke naye anatakiwa afanye vibweka vya kike umvutie mwenza wako, ikiambatana na usafi na kujipodoa.

Mwanaume anazungumza kama kasuku

Habari Anti!

Nikiri nampenda mume wangu. Tatizo linalonifikirisha nipumzike kuwa naye ni mdomo. Anazungumza kuliko flash disk yenye nyimbo 1,000. Akianza hamalizi.

Nifanyeje?

Kama unampenda bila shaka utamvumilia. Naomba nikukumbushe kuwa mapenzi ni kuvumiliana.

Ushauri wangu ni kumueleza wazi kuchoshwa kwako na uzungumzaji wake usio na kituo. Tena usisahau kumueleza na hatua unazofikiria kuchukua baada ya tabia yaje ya uzungumzaji usiokoma ambao sasa umekukifu.

Unaweza pia kuwatumia rafiki zake kusema naye juu ya tabia hiyo inayokukera.

Naamini atakusikia. Pia usikate tamaa, kumbadili mtu tabia siyo kazi rahisi hivyo.